1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika Kusini

Kiwingu cha vita Ukraine chazidi kutanda Afrika

27 Februari 2026

Afrika Kusini imeripoti raia wake wawili kuuawa Ukraine, huku mahakama ya Nairobi ikimshtaki mshukiwa kwa kusafirisha Wakenya 25 kwenda Urusi kupigana, katika ishara ya kuongezeka kwa athari za vita hivyo barani Afrika.

Ukraine, Mkoa wa Kharkiv 2026 | Wanajeshi wa Ukraine wakijiandaa kufyatua kombora kwa kutumia haubitsa ya Bohdana.
Vita vya uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine vimedumu kwa miaka minne sasa na bado hakuna dalili ya kumalizika hivi karibuni.Picha: Vyacheslav Madiyevskyy/REUTERS

Serikali ya Afrika Kusini imethibitisha kuwa raia wake wawili wameuawa katika vita vya Ukraine. Wizara ya Mambo ya Nje imesema watu hao ni tofauti na kundi la Waafrika Kusini 17 waliodanganywa kujiunga na jeshi la Urusi na ambao wengi wao tayari wamerudishwa nyumbani. Haijafafanuliwa ni lini au kwa mazingira gani vifo hivyo vilitokea.

Wizara hiyo imesema inaendelea kuchunguza mitandao inayohusika na uajiri wa raia kwa njia ya udanganyifu. Urusi kwa upande wake imekanusha kuhusika katika uajiri haramu wa raia wa Afrika kupigana nchini Ukraine. Hata hivyo, Kyiv imekuwa ikidai kuwa maelfu ya Waafrika wamejiunga na majeshi ya Moscow.

Nchini Kenya, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma imemshtaki Festus Arasa Omwamba kwa tuhuma za kusafirisha Wakenya 25 kwenda Urusi kwa madhumuni ya unyonyaji. Kulingana na mashtaka, 22 waliokolewa kabla ya kusafiri huku watatu waliokwenda walijeruhiwa katika mapigano kabla ya kurejea nyumbani. Mshtakiwa amekana mashtaka hayo.

Ripoti ya Idara ya Kitaifa ya Ujasusi ya Kenya imeeleza kuwa mawakala wa uajiri walishirikiana na baadhi ya maafisa wa viwanja vya ndege na wahamiaji kuwezesha safari hizo. Ubalozi wa Urusi mjini Nairobi umekanusha kuhusika katika uajiri huo, lakini umesema raia wa kigeni wanaweza kujiunga kwa hiari na majeshi ya Urusi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, amesema Wakenya 27 wameokolewa baada ya kukwama Urusi. Ameeleza kuwa anapanga kufanya ziara nchini Urusi mwezi Machi kujadili suala hilo. Tukio hili limeongeza wasiwasi kuhusu usalama na ulinzi wa vijana wa Afrika wanaovutwa katika vita vya kigeni.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW