Kizaazaa katika robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika
5 Februari 2012Kesho jumapili katika mji mkuu Libreville wenyeji Gabon watakabiliana na Mali kabla ya Ghana kugaragaza na Tunisia mjini Franceville. Waandalizi wa mechi hizo wameanza kuwapa mashabiki tiketi za bure ili kuvijaza viwanja ambavyo vimeshuhudia uhaba wa mashabiki. Tikezi za bila malipo zinapewa wanafunzi na wafanyakazi na pia kutakuwa na huduma za uchukuzi bila malipo. Mchuano wa nyumbani wa jumapili kati ya Gabon na Mali tayari umeuza tiketi zote.
Masaibu ya Ballack katika klabu yake ya Leverkusen yaendelea
Mkurugenzi wa spoti wa klabu ya Bayer Leverkusen Rudi Voeller anatishia kumpiga marufuku wakala wa mchezaji Michael Ballack dhidi ya kuingia katika uwanja wa klabu hiyo ya ligi ya Ujerumani BUNDESLIGA huku uhusiano baina ya pande hizo mbili ukiendelea kutokota. Voeller aliyajibu kwa ghadhabu matamshi ya wakala wa Ballack kuwa mteja wake anatumiwa kama kisingizio ili kukwepa matatizo ya klabu hiyo. Voeller alidai kuwa nahodha huyo wa zamani wa timu ya Ujerumani ana jukumu la kuzungumza mwenyewe na wala sio kumtuma Becker ambaye ni wakala wake kuzungumza kwa niaba yake. Voeller pia alimshtumu meneja mkurugenzi wa klabu hiyo Wolfanga Holzhaeuser kwa kusema kuwa uhamisho wa Ballack katika klabu hiyo haujaleta mafanikio yoyote.
Kwingineko nyota wa Ufaransa Frank Ribery ameishtumu klabu yake ya Bayern Munich kwa kushindwa kuwasajili wachezaji wapya na akasema viongozi hao wa ligi ya Ujerumani walikosa nafasi murwa ya kukiimarisha kikosi chao. Bayern watacheza wanakibarua kikali wanapojaribu kuwakabili Borussia Dortmund na Schalke ambao wanawapa upinzani mkali. Ribery ana jeraha la mgongo alilopata mwanzoni mwa wiki na anasema Bayern wangefaa kukiimarisha kikosi chao wakati wa kipindi cha uhamisho cha mwezi wa Januari. Kocha Jupp Heynckes na afisa mkuu mtendaji Karl-Heinz Rummenigge wamesema viongozi hao wa ligi wana kikosi thabiti kwa sasa jambo ambalo Ribery anatofautiana nalo. Bayern watacheza dhidi ya FC Basel katika mechi za raundi ya kumi na sita ya ligi ya mabingwa barani ulaya Uefa msimu huu, na Ribery amesema wangali kileleni na anahisi wanaweza kushinda mataji yote matatu.
Terry apokonywa unahodha wa timu ya Ujerumani
Kule Uingereza John Terry amepokonywa unahodha wa timu ya taifa kwa mara ya pili kutokana na wasiwasi kuhusiana kesi inayoendelea mahakamani ya ubaguzi. Terry anashtumiwa kwa kumtolea matamshi ya kibaguzi beki wa Queens Park Rangers Anton Ferdinand. Chama cha soka nchini uingereza kimethibitisha kupitia taarifa kuwa mwenyekiti wa FA uingereza David Bernstein aliwasiliana na Terry kwa njia ya simu akimwambia kuhusu uamuzi huo wa FA.
Nchini Uhispania Barcelona wanataraji kukamilisha msururu wa kutoka sare kwa kuwazaba Real Sociedad nyumbani Camp Nou hii leo jumamosi. Mabingwa hao wa ulimwengu wametoka sare mechi zao tatu za mwisho dhidi ya Valencia na Real Madrid katika kombe la Mfalme na pia Villareal katika La Liga. The Catalans wako pointi saab nyuma ya viongozi Real MADRID na wanaonekana kuchoka kisaikolojia na pia kimwili. Beki Gerad Pique anasema ratiba yao imekuwa ngumu lakini wameizoea hali hiyo. Kuna pia majeruhi kikosini huku wachezaji David Villa, Ibrahim Affelay, Andreu Fontas, Andres Iniesta na Pedro wakiwa mkekani pamoja na Seydou Keita ambaye anawakilisha Mali katika dimba la mataifa ya Afrika.
Vurugu za Misri
Shirikisho la soka ulimwenguni FIFA limeitisha ripoti kamili kutoka kwa serikali ya Misri kuhusiana na ghasia zilizozuka baada ya mchuano wa soka mjini Port Said ambapo watu 74 waliuwawa. Takriban watu 1,000 walijeruhiwa katika vurumai hizo siku ya jumatano wakati mashabiki walipouvamia uwanja baada ya timu mwenyeji al-Masry kuishinda ile ya mjini Cairo al-Ahly, ambayo ni klabu iliyofana sana barani afrika. Tukio hilo lilikuwa mkasa mbaya zaidi wa soka nchini Misri na bodi ya shirikisho la soka nchini humo FA imepigwa kalamu na waziri mkuu Kamal al Ganzouri.
Shirikisho la soka ulimwenguni FIFA limemchagua afisa wa Karibik Horace Burrell katika kamati yake inayoandaa mashindano ya Olimpiki, wiki tatu baada ya kumaliza adhabu yake kutokana na utovu wa maadili. Burrell alipoteza nafasi yake baada ya jopo na kinidhamu la FIFA kumpiga marufuku ya miezi mitatu kufuatia uchunguzi kuhusu madai ya ulaji rishwa kutoka kwa aliyekuwa mgombea wa urais wa FIFA Mohammed Bin Hammam na makamu wa rais Jack Warner.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu