Kizungumkuti cha Ukraine Magazetini
26 Novemba 2013Tuanzie lakini Kiev ambako uamuzi wa serikali ya Ukraine wa kusitisha mazungumzo pamoja na Umoja wa ulaya umewaudhi wafuasi wa upande wa upinzani wanaoendelea kuteremka majiani kulalamika.Mhariri wa gazeti la "Sächsische Zeitung" anahisi uamuzi huo ni matokeo ya kishindo kinachoikaba serikali ya mjini Kiev.Gazeti linaendelea kuandika:"Kipi kingekuwa kibaya zaidi kwa Ukraine-uhusiano mbaya pamoja na Urusi au kuzipa kisogo nchi za magharibi?Kwa mtazamo wa muda mrefu ushirikiano pamoja na Umoja wa Ulaya unaweza pengine kuleta tija.Lakini matarajio pekee hayaisaidii pakubwa nchi hiyo.Haiwezi kufumba na kufumbua kujikomboa toka jirani yake mwenye nguvu.Kiuchumi na kijamii litakuwa balaa kwa Ukraine pindi Moscow ikipandisha bei ya gesi au ikizuwia bidhaa za Ukraine zisiingie nchini humo.
Ushawishi wa Urusi nchini Ukraine
Gazeti la "Der neue Tag" linahisi kenda haiko mbali na kumi.Gazeti linaendelea kuandika:"Umoja wa Ulaya unajipendekeza kwa kuahidi misaada, na Moscow inauma na kupuliza.Ukweli utajulikana ijumaa katika mkutano pamoja na wakuu wa Umoja wa Ulaya.Ikiwa mkondo wa mambo utaendelea kuelekea Moscow,itabainika pia nani mwenye usemi katika eneo la Ulaya ya mashariki.
Eti Ni Busara kuipa kisogo Afghanistan?
Afghanistan pia imegonga vichwa vya habari,wahariri wa magazeti wakijiuliza kuhusu hatima ya nchi hiyo baada ya vikosi vya kimataifa kuihama nchi hiyo mwishoni mwa mwaka 2014.Kuhusu kitandawili hicho linaandika gazeti la"Die Badische Zeitung".
"Hata kama hali haitakithiri,lakini picha ya haki za binaadam inayojitokeza hivi sasa miaka 12 baada ya kutimuliwa madarakani wataliban si ya kuridhisha.Wengi kati ya wenye usemi nchini humo hawatofautiani kimawazo na wataliban waliokuwa wakipigana nao.Yote hayo yanabainisha Afghanistan haistahiki kuachwa peke yake wanajeshi wa kimataifa watakapoondoka.Itahitaji kusaidiwa kwa miongo kadhaa tangu na Umoja wa mataifa mpaka na nchi za magharibi.Na hasa katika fani ya elimu.Afghanistan itakapozindukana na kutambua mengi kuihusu nchi hiyo yenyewe na ulimwengu kwa jumla,pengine zitatoweka pia wakati huo desturi mbaya zisizo thamini haki za binaadam.
Siku zinasogea Berlin
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu mazungumzo ya kuunda serikali kuu ya muungano mjini Berlin.Wajumbe wamesaliwa na hadi kesho mchana tu kukamilisha mswaada wa mkataba wa kuunda serikali kuu ya muungano.Eti watafaulu,linajiuliza gazeti la "Neue Osnabrücker"."Hata kama wawakilishi wa Sigmar Gabriel wanasisitiza asili mia 90 ya mswaada huo imekamilika,hata hivyo mada tete kadhaa bado hazijapatiwa ufumbuzi.Dhahir ni kwamba baada ya miezi miwili ya majadiliano muungano wa CDU/CSU na SPD unafujwa hata kabla ya kuundwa.Kiroja ni kwamba shaka shaka hizo zinatolewa wakati mmoja na mashirika ya wanauchumi na wafuasi wa mrengo wa shoto kutoka chama cha SPD.Wamesahau pengine kwamba muungano kama huu wa mwaka 1966-1969 ndio ulioisaidia Ujerumani kuepuka mgogoro mbaya kabisa wa kiuchumi kupiga barani Ulaya bila ya kuutaja ule wa mwaka 2005 hadi 2009 ambao ndio chanzo cha Ujerumani kuudhibiti ipasavyo mgogoro wa fedha ulioitikisa dunia nzima.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman