Klopp alalamikia VAR Premier League
21 Oktoba 2019Katika ligi ya England, Premier League, Manchester United jana ilifikisha mwisho mwanzo mzuri wa Liverpool wa asilimia 100 katika ligi hiyo , pamoja na mfululizo wa ushindi wa michezo 17, kwa kutoka sare ya bao 1-1 uwanjani Old Trafford jana Jumapili.
Hata hivyo ulikuwa mchezo mwingine katika Premier League uliokuwa na utata wa VAR, hali itakayoendelea kuchochea mijadala juu ya mfumo huo ulioanza kutumika msimu huu.
Matokeo hayo yanapunguza uongozi wa Liverpool dhidi ya timu iliyoko nafasi ya pili Manchester City hadi pointi sita na kikosi cha Juergen Klopp hakikuwa katika hali yake bora. Lakini kocha huyo wa Liverpool Juergen Klopp analalamikia uamuzi wa refa pamoja na VAR, baada ya Marcus Rashford kupachika bao mnamo dakika ya 36 ya mchezo..
"Sina hakika kama atakiri, lakini refa Martin Atkinson , mliona mara tu, alianza kukimbia na aliona kuwa litakuwa goli. Na wakafunga na haraka akaonesha VAR. Kwa hiyo wasaidizi wangu walikuwa tayari wamesimama, na kusema , tulieni. VAR inachunguza. Na nilikuwa na hakika ya asilimia 100 kwamba VAR italikataa. lakini kwa sasa bila shaka tunamatatizo. Kwa hiyo refa aliuacha mpira uendelee kwa kuwa ana VAR, lakini VAR inasema hakuna hakika, kwa hiyo sio faulo kwa hiyo siwezi kulikataa."