Klopp azima rekodi ya Man City kutofungwa
15 Januari 2018
Manchester City katika Premier League nchini England imeshuhudia rekodi yake ya kutofungwa ikisitishwa jana Jumapili wakati FC Liverpool iliweka kando kuondoka kwa mchezaji wake nyota wa kati Philippe Coutinho na kupata ushindi mtamu wa mabao 4-3.
Arsenal ambayo inasua sua msimu huu ilikubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Bournemouth , wakati matatizo ya kocha Arsene Wenger yakizidi kutokana na kukaribia kuondoka katika kikosi hicho mshambuliaji nyota Alexis Sanchez. Kwingineko Chelsea ilishikwa shati na kutoka sare ya bila kufungana na Leicester City wakati Harry Kane wa Tottenham amevumisha kimbunga na kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Everton na West Bromwich Albion ilipata ushindi wake wa kwanza katika Premier League kwa kuishinda Brighton kwa mabo 2-0.
Kocha mkuu wa Machester City Pep Guardiola amewapa changamoto wachezaji wake kutumia kipingo walichopokea kutoka kwa Liverpool cha mabao 4-3 kuwa ni tahadhari ya kujilinda dhidi ya kubweteka. Kikosi cha Guardiola kilipokea kipigo dhidi ya Liverpool na kusitisha rekodi yao ya kutofungwa katika Premier League iliyfikia mwisho katika uwanja wa Anfield.
Licha ya mabao ya dakika za mwisho ya Bernardo Silva na Ilkay Gundogan yaliyoweka heshima kidogo katika muonekano wa matokeo hayo, lakini kocha huyo wa Man City Guardiola hakuwa na malalamiko juu ya kikosi chake kupata kipigo cha kwanza tangu Aprili 5 dhidi ya Chelsea.
Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp anaamini kwamba mchezo huo ulikuwa bora kabisa msimu huu , umeonesha haja ya kutohofia wakati timu inapokumbana na timu yenye uwezo mkubwa kama City.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / ape /
Mhariri: Yusuf , Saumu