Kocha Polanski kuongoza mechi moja zaidi Gladbach
6 Oktoba 2025
Kocha wa Borrusia Mönchengladbach, Eugen Polanski, amesema atabaki kuwa kocha wa klabu hiyo inayokabiliwa na changamoto ya kusuasua angalau kwa mechi moja ya Bundesliga.
"Nimepokea ishara kwamba naweza kuendelea," Polanski alisema baada ya pambano la Jumapili usiku ambapo walitoka sare tasa na Freiburg.
Gladbach wako nafasi ya pili kutokea mkiani na ni timu pekee ya Bundsliga ambayo inasubiri kupata ushindi wa mechi msimu huu, ikiwa imeshapata sare tatu na kupoteza mechi tatu. Mechi inayofuata Gladbach watakwaana na Union Berlin ugenini mnamo Oktoba 17 baada ya kipindi cha mapumziko kupisha ratiba ya mechi za kimataifa.
Polanski kwa kawaida ni kocha wa timu ya vijana wa umri wa chini ya miaka 23 katika klabu ya Gladbach lakini akateuliwa kushikilia timu kubwa baada ya kocha wa zamani Gerardo Seoane kutimuliwa mwezi uliopita. Polanski amesimamia mechi zilizomalizikia sare dhidi ya Bayer Leverkusen na Freiburg, lakini pia akapoteza mechi dhidi ya Eintracht Frankfurt 6-4,ambapo Gladbach walikuwa nyuma 6-0 baada ya dakika 47 za pambano hilo.
Polanski alisema anatarajia kuendelea na klabu ya Gladbach akisema anapata uungwaji mkono mzuri sana kutoka kwa kila mtu, uongozi, timu ya kiufundi na kwa wachezaji.
"Kuna wiki mbili kabla pambano dhidi ya Union. Kutakuwa pengine na mazungumzo zaidi kabla kufikia wakati huo. Kwa sasa tunaelekeza nguvu wakati huu wa kipindi cha ratiba ya mechi za kimataifa, ni wapi tunapotaka kupalainisha na wachezaji wengine waliosalia, pamoja na mechi dhidi ya Union Berlin," alisema.
"Naisubiri kwa hamu mechi dhidi ya Union Berlin. Kuna mengi ya kufanya. Na kama hali itaendelea kwa muda mrefu zaidi, nitafurahi tena."
Kauli ya mwisho huenda ikatoka kwa mkurugenzi mpya wa michezo baada ya mkurugenzi wa zamani, Roland Virkus, kujiuzulu wiki iliyopita. Hili ni suala la kipaumbele kwa Gladbach kwa wakati huu, na mkurugenzi mtendaji Stefan Stegemann amezungumzia mazungumzo ya kutia moyo na wawaniaji wa nafasi hiyo.
Kiungo Philipp Sander amempongeza kocha Polanski akisema: "Ni mtu anayeingiiana na kuzungumza vyema na wachezaji, yeye mwenye akiwa aliwahi kuwa uwanjani muda si mrefu sana uliopita. Hali hiyo hujenga mazingira ya maelewano ya karibu, na nadhani ndio maana ana hisia nzuri sana kuhusu timu."
"Kuwa na mpango wa ulinzi au wa kushambulia ni jambo moja. Kuufanya mpango huo utoe matokeo ni jambo lingine. Nafikiri anaweka umuhimu mkubwa kwa jambo hilo. Na nafikiri tuko katika mkondo sahihi," alisema Sandner.