1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kocha wa Dortmund Klopp asema haendi kokote

1 Desemba 2014

Masaibu ya Borussia Dortmund yanaendelea baada ya kupewa kichapo cha magoli mawili kwa sifuri na Eintracht Frankfurt. Matokeo hayo yamewaacha mabingwa hao wa mwaka wa 2011 na 2012 katika nafasi ya mkia

Fußball Bundesliga 13. Spieltag Borussia Dortmund gegen Eintracht Frankfurt
Picha: Getty Images/M. Hangst

Maswali sasa yameibuka kuhusu hatima ya kocha Jurgen Klopp. Lakini baada ya mechi hiyo, Klopp alisema hana mipango yoyote ya kung'atuka kutokana na matokeo hayo mabaya.

Ni mara ya kwanza tangu msimu wa 2007 na 2008, ambapo Dortmund wameshikilia mkia lakini Klopp ambaye pia aliiongoza klabu hiyo katika fainali ya Champions League miezi 18 pekee iliyopita, amesema wako tayari kujinyanyua upya na kusonga mbele.

Alipoulizwa kama alikuwa na fikra zozote za kuondoka, Klopp aliiambia televisheni ya Sky kuwa na namnukuu “kama ni suala la bahati pekee na iwe ni kocha mpya atatimiza hilo, basi niileze hivyo na kisha nitaondoka. Lakini kama hakuna yeyote atakayejitokeza na kuniambia kuwa kuna mtu atakayeweza kuimarisha matokeo, basi siwezi kuondoka”. Mwisho wa nukuu.

Kikosi cha Dortmund kinahitaji kutafuta ufumbuzi wa migogoro yao uwanjaniPicha: Getty Images/M. Hangst

Klopp anasema hajamzuia yeyote lakini hawezi kung'atuka kama hakuna suluhisho bora. Na kwa sasa hilo ni jukumu lake na analikubali. Dortmund, ambao tayari wamefuzu katika duru ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, sasa wamepoteza mechi nane kati ya 13 msimu huu. Huku wakiwa na safu dhaifu ya ulinzi, ukosefu wa mabao na msururu wa majeruhi, wakiwemo Marco Reus na mabeki Mats Hummels na Sokratis Papastathopolous, BVB wameshinda mechi moja tu kati ya kumi za Bundesliga na wana points 11 pekee.

Bayern yapepea

Na wakati Klopp na vijana wake wakiendelea kuyumbayumba kwa kushika mkia, katika upande wa juu wa msimamo wa ligi, Bayern Munich wanaendelea kupaa. Vijana hao wa kocha Pep Guardiola wanaanza mwezi wa Desemba wakiwa kileleni na pengo la points saba na wanaonekana tayari kuwa katika usukani wa kuchukua taji jingine la Bundesliga, licha ya kuwa kuna miezi mingine sita iliyosalia katika msimu huu. Arjen Roben aliifungia Bayern goli pekee na la ushindi dhidi ya Herth Berlin.

Nambari mbili Wolfsburg ilipata ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya nambari tatu Borussia Moenchegladbach. Kichapo hicho kimewaweka Gladbach katika nafasi ya tano ya msimamo wa ligi wakati kukiwa na pengo la points 13 dhidi yao na viongozi Bayern.

Leverkusen waliwazidi nguvu Cologne katika mchuano wa Rhine derbyPicha: Patrik Stollarz/AFP/Getty Images

Werder Bremen ilipata ushindi wa mabao manne kwa sifuri dhidi ya Paderborn na kusonga hadi nafasi ya 14 wakati kaimu kocha Viktor Skripnik akipata ushindi wake wa nne katika mechi tano tangu alipochukua usukani kutoka kwa Robin Dutt aliyepigwa kalamu.

Schalke na Bayer Leverkusen pia zilipata ushindi mnono katika mechi zao. Baada ya kichapo cha magoli matano kwa sifuri dhidi ya Chelsea katika Champions League, Schalke ilijinyanyua na kuibambua Mainz magoli manne kwa moja huku mshambuliaji wa Uholanzi Klaas-Jan Huntelaar akitikisa wavu mara tatu. Ushindi huo umeisogeza katika nafasi sita ya msimamo wa ligi

Leverkusen nayo iliinyamazisha Cologne kwa kuibamiza mabao matano kwa moja na kuruka hadi nafasi ya tatu. Josip Drmic na Karim Bellarabi walifunga magoli mawili kila mmoja. Hakan Calhanoglu aliongeza la tano. Huyu hapa Drmic

Hoffenheim walivuka hadi nafasi ya saba baada ya kupata ushindi wa mabao manne kwa matatu dhidi ya Hanover, ambao wameanguka katika nafasi ya nane. Katika emchi nyingine, Augsburg ilitoka nyuma na kuizaba Hamburg mabao matatu kwa moja na kusonga juu angalau kwa muda katika nafasi ya nne.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW