1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kichapo cha 5-0 dhidi ya PSG chamuondoa De Zerbi Marseille

11 Februari 2026

Kocha wa Marseille Roberto De Zerbi ameondoka kwenye klabu hiyo ya Ufaransa katikati ya machungu ya kipigo cha aibu cha mabao 5-0 dhidi ya PSG.

Ligi ya Mabingwa ya UEFA 2026 | Club Brugge dhidi ya Olympique Marseille | Kocha Roberto De Zerbi akiwa katika mkutano na waandishi wa habari
Kocha wa Marseille Roberto De Zerbi ameondoka kwenye klabu hiyo ya Ufaransa kufuatia matokeo mabayaPicha: Nicolas Tucat/AFP

Klabu ya Marseille, mabingwa mara tisa wa Ufaransa imesema Jumatano kwamba wameachana na kocha huyo kufuatia makubaliano ya pande zote mbili.

Kipigo cha aibu cha Jumapili kwenye uwanja wa Parc des Princes, kiliwafanya mabingwa watetezi PSG kujiimarisha kileleni kwa pointi mbili dhidi ya Lens baada ya mzunguko wa 21, huku Marseille ikiwa nafasi ya nne baada ya kichapo hicho. 

"Kufuatia mashauriano yaliyohusisha wadau wote katika uongozi wa klabu - mmiliki, rais, mkurugenzi wa mpira wa miguu na kocha mkuu - iliamuliwa kumbadilisha kongozi wa kikosi cha kwanza," Marseille alisema. "Huu ulikuwa uamuzi wa pamoja na mgumu uliochukuliwa baada ya kuzingatiwa kwa kina, kwa maslahi ya klabu na ili kushughulikia changamoto za michezo ya mwisho wa msimu."

Klabu ya Marseille ilitolewa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufungwa 3-0 wiki mbili zilizopita.Picha: Nicolas Tucat/AFP

De Zerbi awaomba radhi mashabiki wa Marseille

Kuondoka kwa De Zerbi kunafuatia pia kipigo kingine cha mabao 3-0 dhidi ya Club Brugge, wiki mbili zilizopita, matokeo yaliyoitupa nje klabu ya Marseille kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

De Zerbi, aliyewaomba radhi mashabiki wa klabu hiyo ya Marseille baada ya kichapo cha wapinzani wao wa jadi PSG, alijiunga na Marseille mwaka 2024 baada ya kuifundisha klabu ya Brighton kwa misimu miwili. De Zerbi aliiongoza Marseille na kumaliza nafasi ya pili msimu uliopita.

Marseille iliyotawala soka la ndani mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990, haikutangaza mara moja mtu atakayerithi mikoba ya De Zerbi kabla ya mchezo wa ligi siku ya Jumamosi dhidi ya Strasbourg. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW