1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kofi Annan akabiliwa na kibarua kigumu Kenya

Josephat Charo16 Januari 2008

Bunge lamchagua spika wake

Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi AnnanPicha: AP

Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan anakabiliwa na kibarua kipya nchini Kenya huku bunge la kumi la nchi hiyo likiwa limeanza kukutana kwa mara ya kwanza hii leo. Ziara ya Kofi Annan mjini Nairobi inafanyika wakati chama kikuu cha upinzani cha Orange Democratic Movement, ODM, kikiwa kimeitisha maandamano ya siku tatu kupinga ushindi wa rais Mwai Kibaki.

Bwana Kofi Annan alikubali mwaliko wa rais wa Ghana, John Kufuor, ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, aongoze jopo la wapatanishi watakaosaidia juhudi za kuleta amani nchini Kenya. Hata hivyo, kanuni za kibarua cha bwana Annan zinakabiliwa na utata. Chama cha ODM kinataka wapatanishi wa kimataifa kuutanzua mzozo wa kisiasa uliopo, lakini upande wa serikali ya rais Mwai Kibaki hautaki mwanadiplomasia yeyote wa kigeni afanye lolote mbali na kuongoza mazungumzo.

´Tunamtaka bwana Annan aongoze juhudi za upatanisho akifahamu kwa kina uzito wa tatizo lililopo, ´ amesema katibu mkuu wa chama cha ODM, profesa Anyang Nyong´o, katika taarifa yake aliyoisoma kwa wabunge wa chama hicho.

Mawaziri wa rais Kibaki hawataki kukubali aina yoyote ya mazungumzo na upinzani. Ikizingatiwa matamshi makali na ya kutojali ambayo wamekuwa wakiyatoa, huenda mawaziri hao wakawa wanapania kuizuia timu ya bwana Annan isifaulu kufanya kazi yake.

Waziri wa barabara na ujenzi, bwana John Michuki, amesema Kofi Annan haendi mjini Nairobi kwa sababu wamemualika, akisisitiza kwamba walishinda uchaguzi na haoni sababu ya mtu yeyote kuongoza mazungumzo ya kugawa madaraka.

Insert O-ton Michuki.

Inaonekana kwa mara nyingine tena vita vimetangazwa huku Kenya ikijiandaa kwa wimbi la pili la ghasia na machafuko. Makao makuu ya chama cha ODM, Orange House katika eneo la Kilimani, yamejaa wafanyakazi wa chama wakipanga kufanya maandamano licha ya hatua ya serikali kuyapiga marufuku maandanao hayo.

Tume mbili za hadhi ya juu zilizojaribu kuumaliza mgogoro wa kisiasa nchini Kenya, zilishindwa wiki iliyopita wakati rais wa Ghana, John Kufuor na naibu waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani anayehusika na mswala ya Afrika, Jendayi Frazer, walipolazimika kuondoka mjini Nairobi bila mafanikio yoyote.

Kofi Annan anatarajiwa kuanza awamu ya tatu ya mazungumzo akiongoza timu ya wajumbe watatu wa Umoja wa Afrika, wakiwemo pia Bi Graca Machel, mke wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, na rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa.

Je kuna matumaini gani ya bwana Annan kuweza kuwaleta pamoja rais Kibaki na mpinzani wake Raila Odinga, jambo ambalo lilimshinda John Kufuor na Jendayi Frazer? Chama cha ODM kikiwa hakijaridhika kimewataka wadhamini wa kimataifa wasitishe misaada ili kuishinikiza serikali ya rais Kibaki ikubali upatanisho wa kimataifa.

Rais Kibaki alidhamini ukurasa mzima wa magazeti ya Jumapili iliyopita akidai chama cha ODM kilifanya njama ya kuvuruga juhudi za rais John Kufuor kuongoza mazungumzo. Taarifa hiyo ya serikali pia iliuita msimamo wa chama cha ODM kuwa udanganyifu.

Rais Kibaki ameonyesha mwenendo wa ujanja kukwamisha juhudi za upatanisho. Wakati Jendayi Frazer alipokwenda Nairobi baada ya machafuko kuzuka, rais Kibaki aliapishwa kabla mazungumzo kufanyika. Naye rais John Kufuor wa Ghana alipowasili kujaribu kuzipatanisha pande zinazozozana, rais Kibaki alitangaza nusu ya baraza lake la mawaziri.

Ili bwana Annan aweze kupunguza tofauti kati ya pande mbili nchini Kenya, atatakiwa ashughulikie maswala mawili muhimu. Kwanza mzozo wa kisiasa nchini Kenya hautakiwi utengwe mbali na janga la kibinadamu lililoibuka nchini humo. Pili, sifa ambayo Kenya imejipatia baada ya miaka ya kuonekana kama mfano mzuri wa uthabiti, huenda ikabadilika na kusababisha hali ngumu ya kiuchumi kwa nchi inayotegemea sana utalii na misaada ya kigeni.

Kuna uwezekano mkubwa wa machufuko kutokea tena na watu wengi zaidi kuuwawa. Itachukua mda mrefu kwa Kenya kuondokana na vifo na tatizo la maelfu ya watu kulazimika kuyakimbia makazi yao.

Kofi Annan atahitaji kuongeza shinikizo ambalo limewekwa na Marekani, Uingereza na nchi nyingine za kigeni dhidi ya rais Kibaki. Maneno makali yaliyotolewa na wizara ya mambo ya ndani ya Marekani Jumapili iliyopita kwamba haitakuwa na uhusiano wa kawaida na Kenya mpaka mazungumzo ya kuumaliza mzozo yafanyike, yanatakiwa yarudiwe na bwana Kofi Annan.

Nchi nyingi za Ulaya zimepiga marufuku raia wao wasisafiri kwenda Kenya. Ikiwa serikali ya Kibaki haitobadili msimamo wake na kukubaliana na upinzani, Kenya itatengwa kimataifa na pengine kuwekewa vikwazo. Itakuwa ujinga kudhamni kwamba wapambe wa rais Kibaki hawafahamu hatari zilizopo. Ujumbe wa Kofi Annan utakuwa umefanya kazi yake ikiwa utaudhihirishia utawala wa Kenya kwamba gharama ya kupuuza vitisho hivi vya ndani na shinikizo kutoka nje ni kubwa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW