1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kofi Annan akutana na Assad

29 Mei 2012

Rais Assad wa Syria amekutana na mjumbe maalum wa kimataifa, Kofi Annan, kufuatia mauwaji ya Houla yaliyolaaniwa kimataifa na ambayo serikali ya mjini Damascus inawatupia lawama wanamgambo wa kiislamu.

Mjumbe maalum wa kimataifa Kofi Annan (kushoto) na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Syria Walid MoallemPicha: picture-alliance/dpa

Mjumbe maalum wa kimataifa, Kofi Annan, amewasili Damascus jana kwa lengo la kuuokoa mpango wa amani unaoungwa mkono na Umoja wa mataifa na Jumuia ya Nchi za Kiarabu-Arab League. Wiki sita tangu ulipoanzishwa, mpango huo haukusaidia kusitisha umwagaji damu uliofuatia vuguvugu la wapenda mageuzi lililoanza kwa amani miezi 14 iliyopita .

Kofi Annan ameyataja mauwaji ya hivi karibuni ya Houla ambapo zaidi ya watu mia moja wameuwawa "kuwa ni msiba" ambao madhara yake ni makubwa."

Waasi wanahisi juhudi za Umoja wa mataifa za kutaka silaha ziwekwe chini,zimeshindwa. Hata hivyo, mjumbe huyo maalum wa Umoja wa mataifa na Jumuia ya Nchi za Kiarabu, Kofi Annan, anasisitiza:

"Ninaamini tume ya umoja wa mataifa ndio pekee inayoweza kurejesha utulivu nchini. Ninataraji serikali na makundi yote ya upande wa upinzani yataitambua hali hiyo na kuitumia fursa hii japo ndogo ya kudhamini amani.

Haijulikani hasa nini katibu mkuu huyo wa zamani wa Umoja wa mataifa Kofi Annan na rais Bashar al Assad wamekizungumzia hii leo.

Wadadisi wanaamini, hata hivyo, mazungumzo yao yamegubikwa na shinikizo linalozidi kuongezeka kumaliza umwagaji damu nchini Syria.

Kofi Annan akizungumza na waandishi habari mjini DamascusPicha: picture-alliance/dpa

Kofi Annan atazungumza pia na mashirika ya huduma za jamii na wawakilishi wa makundi ya upande wa upinzani.

Mjumbe huyo wa kimataifa anapanga kuzungumza na waandishi habari leo jioni.

Wakati huo huo, raia wasiopungua sita wameuwawa leo hii kufuatia mapigano katika sehemu mbali mbali za Syria.

Australia imemfukuza balozi wa Syria nchini humo kama jibu kwa mauwaji ya Houla.

Shirika la habari la Ujerumani-DPA- limenukuu duru za kuaminika kutoka Uturuki zikisema huenda nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wakapitisha hatua kama hiyo ya Australia.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov (kulia) na mwenzake wa Uingereza William HaguePicha: AP

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Sergei Lavrov, ameonya mzozo wa Syria unaweza kuathiri vibaya eneo lote la mashariki ya kati, ikiwa hautapatiwa ufumbuzi.

Akizungumza na waandishi habari mjini Moscow, waziri Lavrov amesema tunanukuu: " jumuia ya kimataifa inapaswa kwa pamoja kuwajibika zaidi, kuepuka kunyunyizia mafuta katika cheche za moto na badala yake kuzileta katika meza ya mazungumzo pande zote zinazohusika", mwisho wa kumnukuu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Sergei Lavrov.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters,/AFP

Mhariri: Miraji Othman