Utengenezaji wa kofia za vitho
16 Februari 2019Kofia hizo huvaliwa pamoja na kanzu ambazo aghalabu ni utaratibu wa waislamu. Ufundi wa kofia za vitho ni ujuzi unaopatikana visiwani kama vile Lamu, Pate, Faza, Mombasa na hata Zanzibar. Kofia hushonwa kwa mkono na huchukua muda wa kiasi ya miezi mitatu kukamilika.
Ufundi wa kofia za vitho ni ujuzi unaopatikana visiwani kama vile Lamu, Pate, Faza, Mombasa na hata Zanzibar. Kofia hushonwa kwa mkono na huchukua muda wa kiasi ya miezi mitatu kukamilika.
Kanzu hukamilishwa na kofia
Maisha kisiwani Lamu ni ya mwendo wa aste aste. Kila Ijumaa wanaume huvalia kanzu na kofia za vitho ili kuelekea msikitini kwa sala maalumu ya mwisho wa wiki. Kofia hizo hulikamilisha vazi la kanzu ambalo ni utamaduni ulio na asili yake kwenye mataifa ya Arabuni. Kofia yenyewe inaanza kwa mshadhari na vipande viwili vya kahafu na kile cha juu. Je, kofia hizo hushonwa vipi?
Tima Fakii ni mwenyekiti wa kikundi cha Kandahar cha wanawake wanaoshona nguo na kofia za vitho. Alisema, "Kwanza naanza kuwachorea maua kwa mkono na kalamu kisha waanza kutengeza vitho. Kuna kofia ya kuanzia yaitwa bulbul mthanga, ya kitho kimoja kimoja."
"Changamoto zake ni kazi ya tabu na inachukua muda kushona na pia vidole vinachafuka kwani sindano inakudunga ila pesa yake ni nzuri," aliendelea kueleza.
Mwiba wa Nungu
Nakshi za mshadhari hutegemea ujuzi na ubunifu wa mshonaji. Hatua ya kutia uzi inafuatia ili kuipa kofia umbo zuri. Uzi wenyewe ni mahsusi kwa nakshi na ni wa rangi tofauti tofauti. Mwiba wa nungu ndio unaotumiwa kutoboa vishimo vidogo vinavyojulikana kama vitho.
Zahara Suleiman ni mkaazi wa mtaa wa Kashmir kisiwani Lamu na mshonaji wa kofia za vitho. Alifafanua umuhimu wa mwiba huo katika taaluma nzima. "Hatua ya kwanza naliangalia ua kisha nakupa bei. Natumia uzi ambao ni wa kitambara, tunaita lasi. Kuna sindano yake tunayotumia kushonea kitho ili kipendeze. Hii tundu kuna mwiba wa nungu yaani kidungumaria ndiyo tunatumia kuzibulia," alieleza.
Kupiga dondo
Ili kofia ipendeze, sharti ishonwe kwa mkono. Kila nafasi inajazwa kwa kuufuata mshadhari. Baada ya hapo kila kipande cha kofia kinapigwa dondo ili isifurefure. Kuzuua ndio hatua ya mwisho inayovitoboa vitho vya kofia. Wanaume wanaovaa kofia za vitho wanasemaje kuhusu utamaduni huu?
Sheikh Abubakar Din wa msikiti wa Riadha kisiwani Lamu alisisitiza. "Kofia ya vitho ni fahari ya mswahili yeyote. Ikiwa ina vitho vidogo zaidi ndipo ustadi wa mshonaji unakuwa bayana kadhalika mshadhari mzuri. Utamaduni huu wa wazee wetu umehifadhiwa na kitengo cha kuhifadhi turathi za kitaifa, NMK. Kimesaidia sana katika hilo."
Kulingana na utaratibu, mteja wa kofia ya vitho hukabidhiwa amana yake ikiwa vipande viwili ili kuifuta dhana kuwa ilishavaliwa na mtu mwengine. Hatimaye mteja anaunganisha mshadhari na kahafu na kofia iko tayari kuvaliwa.
Mwandishi: Thelma Mwadzaya, DW, Nairobi
Mhariri: Josephat Charo