Kolon. Siku ya vijana wa Kikatoliki inaendelea.
20 Agosti 2005Kiongozi wa kanisa Katoliki Pope Benedict wa 16 ambaye yuko mjini Kolon , Ujerumani akishiriki katika sherehe za siku ya vijana wa Kikatoliki duniani, anatarajiwa kukutana na kansela Gerhard Schröder pamoja na kiongozi wa chama cha upinzani Angela Merkel baadaye leo.
Kiongozi huyo wa kidini pia atakutana na viongozi wa jumuiya ya Waturuki Waislamu wanaoishi nchini Ujerumani .
Jana Ijumaa , Pope Benedict alifanya ziara ya kihistoria baada ya kutembelea Sinagogi mjini Kolon. Hiyo ni ziara ya pili inayofahamika kwa kiongozi wa kanisa la Kikatoliki kutembelea sehemu ya ibada ya Wayahudi.
Katika hotuba yake, Pope alishutumu mauaji ya maangamizi yaliyofanywa na Utawala wa Ujerumani wa Kinazi, na kuonya juu ya kurejea tena hali ya chuki dhidi ya Wayahudi.
Amesema kuwa kanisa Katoliki litapambana katika kuleta maelewano , maridhiano na amani.
Sherehe za siku ya vijana wa Kikatoliki duniani inatarajiwa kufikia kilele kesho kwa kufanya misa ya wazi.