1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KOMBE LA AFRIKA LA MATAIFA MJINI TUNIS:

22 Januari 2004

JE,KAMERUN ITALITWAA KOMBE KWA MARA YA TATU MFULULIZO AU -MISRI ITAIPIKU GHANA NA KULITWAA KOMBE KWA MARA YA 5 ? NA RWANDA YAWEZA KUZUSHA MAPINDUZI JIONI HII KWA KUWALAZA WENYEJI TUNISIA ? -ISSA HAYATOU AMSHINDA ISMAIL BHAMJEE NA KUWA RAIS WA CAF

Firimbi inalia jioni hii mjini Tunis,kuanzisha Kombe la 24 la afrika la mataifa tangu lile la kwanza kabisa mjini Khartoum,Sudan, 1957. Wenyeji Tunisia wanaoandaa Kombe la Afrika mara ya tatu tangu 1965 walipoandaa kwa mara ya kwanza na Ghana kutoroka na Kombe, wanafungua dimba na Rwanda inayoshiriki kwa mara ya kwanza katika finali hizi.

Kombe hili la 24 linachezwa bila ya timu mbili maarufu ambazo daima hazikukosa kushiriki-Ghana na jirani zao Ivory Coast-zote zilitimuliwa nje katika kinyan'ganyiro cha kuaniab tikiti 16 za Kombe hili nchini Tunisia. Tunisia kama wenyeji sio tu wanatamani kutawazwa mabingwa kwa mara ya kwanza bali pia kunawirisha nafasi yao kuandaa kombe la kwa nza la dunia barani afrika hapo 2010.Uamuzi wapi kombe hilo litachezwa utakatwa hapo mei mjini Paris. Timu mbili-mabingwa wa zamani zinataka kuweka rekodi maalumu:wakati simba wa nyika-kamerun wanapania kutoroka na Kombe hili kwa mara ya tatu mfululizo-sifa ambayo haikufikiwa na timu yoyote hadi sasa,mafirauni wa Misri wanalitaka Kombe kwa mara ya tano na hivyo, kuvunja rekodi ya Black Stars Ghana .

Misri imetawazwa mabingwa 1957 na tena nyumbani cairo, 1959. Ikiteremka na mshambulizi wake hatari Ahmed Hossam anaeichezea Olympic Marseille ya Ufaransa, Misri inajinata ndie jogoo wa Afrika ya kaskazini.Walishinda tena kombe hili 1986 na mara ya mwisho 1998 huko Ougadagou,ilipozima vishindo vya Bafana bafana-Afrika kusini.

Simba wa nyika-kamerun chini ya kocha mjerumani Winfried Schäfer na wakiteremka tena na staili mpya jazi zao-kijani na nyeupe chini ya nahodha Rigobert Song,wanalitaka Kombe kwenda nalo tena Yaounde ambako limelala miaka 4 iliopita.kamerun ilitawazwa mabingwa 2000 mjini Lagos, na ikidai mramba asali harambi mara moja, ilionja tena utamu mwaka 2002 ikiwa njiani kwenda katika Kombe la dunia .sasa kama mabingwa wa Afrika na wa olimpik, simba wa nyika hawataki kuvuliwa taji.Kamerun hatahivyo,itakumbana na changamoto kali na hasa kutoka Misri iliopo kundi moja nao ,lakini pia Senegal inayopepea wakati huu bendera ya Afrika katika dimba la ulimwengu.Takriban timu yao nzima inacheza Ufaransa na Uingereza.
Kamerun itategemea tena mabao ya samuel Eto'o ,Djemba Djemba na Patrick Mboma.

Nigeria ikiongozwa mara hii na nahodha wao mwenye chenga maridadi na za ajabu J.J.Okocha,ilishindwa hata kuvuka duru ya kwanza pale Kombe hili lilipoaniwa Tunisia,miaka 10 nyuma.Mara hii Super Eageles wanataka kurekebisha madhambi yao ya miaka 10 nyuma. Kombe la Afrika la mataifa lililokua zamani likichafua kalenda ya Ligi za Ulaya,hatua kwa hatua limeanza kupata umaarufu na kuheshimiwa na ulimwengu wa dimba.hii inafuatia timu kama vile Kamerun na Nigeria na sasa Senegal kutoa wachezaji waliotia fora katika Ligi za nchi za nje kama zile za Ufaransa,Uingereza,Spain na Ujerumani-akina J.J.Okocha anaeichezea Bolton wonderes ya Uingereza,nwanko Kanu wa Arsenal London.

Klabu za Ufaransa ndizo zitakazochangia takriban robo ya wachezaji katika kinyan'ganyiro cha timu hizo 16.Wachezaji wanatoka takriban katika Ligi zote za dunia-kuanzia Japan hadi marekani,zile za uarabuni lakini zaidi kutoka Ufaransa na Uingereza na hii yabainisha mafungamano na dola za zamani za kikoloni. Timu zote 16 isipokua 2 tu Kenya na Rwanda zina mchezaji alao mmoja anaecheza Ufaransa.

Kombe la Afrika linaanza leo huku Ligi za Ulaya pia zikiendelea na nyengine kama Bundesliga ikikaribia kuanza mwisho wa mwezi.Miongoni mwa klabu za ulaya zilizoumia sana katika kutoa wachezaji wao ni Lens ya Ufaransa:Inamkosa nahodha wa Kamerun,Rigobert Song,John Utaka,pape Bouba Diop wa senegal na Adam Coulibaly.hao ni wachezaji 6 mashuhuri ambao lens haitaweza kuwatumia kati leo na Februari 14 litakapomalizika Kombe hili.

Klabu za Ubelgiji zinachangia wachezaji 29 na ligi ya Afrika kusini 24.Shauku ya Ligi ya uingereza Premier League kwa wachezaji wa kiafrika ikiongezeka ,kundi la wachezaji 23 linatoka Premier League.Linajumuisha mastadi kama El hadji Diouf mara 2 mchezaji bora wa mwaka wa afrika. Kombe hili la Afrika linaziwakilisha pia klabu zote maarufu kwa kutoa wachezaji:kuanzia manchester united,Arsenal london,Bolton Wonderes ,Liverpool za Uingereza, Celtic ya Uskochi hadi Ajax Amsterdam na Feynoord Rotterdam ya Holland.Nyengine ni Olympique Marseille ya Ufaransa,Steua Bucharest ya Romania.Tokyo verdi ya japan imechangia Patrick Mboma.

'Football made in Africa' ni bidhaa iliozagaa hadi Ligi ya Russia na mshambulizi Nkosinathi Nhleko ataiwakilisha Dallas Burn ya marekani. Lakini hata visiwa vidogo vya bahari ya Hindi vinachangia wachezaji katika Kombe hili la Afrika:Ceyschelles,kwani huko ndiko anakocheza beki mshahara wa Harambee Stars Moses Gikenyi.Yeye sio tu anaiwakilisha Kenya bali pia klabu yake St.Michel United.

Kwa ufupi,mabingwa watetezi Kamerun,Senegal,mali na Nigeria ndizo zinazochangia vikosi vikubwa vya wachezaji wa Afrika wanaosakata dimba nchji za n'gambo.Kwani kila moja ya nchi hizi imechagua wachezaji 20 kati ya vikosi vyao vya wachezaji 22 kutoka nje ya Afrika.Misri tu inajivunia wsachezaji 16 wa nyumbani katika kikosi chake cha wachezaji 22 na weengi wao wanatoka klabu bingwa Zamalek.

Katika dimba la ufunguzi leo, Rwanda inayocheza kwa mara ya kwanza katika Kombe hili inateremka na wachezaji wengi kutoka timu ya wanajeshi APR labda wanakusudia vita kweli.APR imechangia wachezaji 10 pekee lakini sio kusema rwanda inawakilishwa na APR katika Kombe hili. Rwanda iko kundi A na wenyeji Tunisia, Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na Guinea.Changamoto yake na Kongo yaeza kugeuka duru ya pili ya vita vya maziwa makuu.Changamoto hii itakua februari mosi.Sitapenda kuagua matokeo yake.

Kundi B:linajumuisha Senegal,Burkina faso,harambee Stars-Kenya na Mali. Kenya inarudi katika Kombe hili kwa mara ya 4 ikiwa jirani tanzania itanisamehe kuwakumbusha hayo.
Kundi C:Laingiza simba wa nyika-kamerun-Misri,Algeria na chipukizi Zimbabwe inayocheza kama rwanda kwa mara ya kwanza .

Nas Kundi D: laongozwa na Nigeria,lakini lina Bafana Bafana-Afrika Kusini,Morocco na Benin. Mechi zinachezwa katika viwanja 2 mjini Tunis,pasmoja na dimba la Ufunguzi, nyengine mjini Sfax,Sousse,Bizerte na katika mwambao wa pwani wa Monastir. Jumla ya viwanja 6 vinatumika kwa Kombe hili la 24 la Afrika na mechi 32 zitachezwa kabla hakuibuka mshindi hapo Februari 14 . Kanda ya Afrika mashariki na kati-CECAFA inawakilishwa na Kenya na Rwanda.Kutoka Kanda hii,Zanzibar ikiwakilishwa na mwenyekiti wa ZFA Ali fereji inatumai kurejea na uanachama wa CAF ikiwa kila kitu kitaenda sawa.
Kutoka kanda ya COSAFA kuna Bafana Bafana Afrika Kusini na Zimbabwe.
Ushindi wa Afrika Kusini utanyanyua heba na nafasi zake za kuchaguliwa hapo mei mjini Paris kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kuandaa Kombe la dunia la FIFA 2010,kufuatia lijalo hapa Ujerumani 2006.

Kombe la Afrika sio tu kinyan'ganyiro kati ya timu za afrika ya kaskazini na zile za kusini mwa Jangwa la Sahara na staili gani ya dimba ni bora zaidi,bali ni kocha gani anaibuka bingwa:je, wale wa Ufaransa kama Roger Lemmere anaeiongoza Tunisia-wenyeji au Winfried Schäfer kutoka Ujerumani mwenye dhamana ya kikosi cha Kamerun.Hata hatima yao kubakia kitini au itaamuliwa na matokeo ya Kombe hili.

Kuanzia leo ulimwengu mzima basi unakodoa macho Tunis,Mecca wakati huu ya kabumbu la Afrika. Mwishoe, Issa Hayatou wa Kamerun amechaguliwa tena mjini Tunis, rais wa CAF-shirikisho la dimba la Afrika.Hayatou amemshinda Ismail Bhamjee wa Botswana hapo alhamisi wazi kabisa na kuongeza kipindi cha 5 kama rais wa CAF.Mkamerun huyo ni makamo rais pia wa FIFA. Taarifa zaidi kutoka Tunis zasema: Kombe la Afrika na Umoja wa mataifa zitashirikiana wakati wa kinyan'ganyiro hiki kupiga vita umasikini barani Afrika na kuwazindua zaidi mashabiki juu ya hatari za UKIMWI.
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW