1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KOMBE LA DUNIA 2006

28 Machi 2005

KINYAN’GANYIRO CHA TIKETI ZA FINALI YA KOMBE LA DUNIA 2006 NCHINI UJERUMANI

KANDA YA AFRIKA:I.COAST,NIGERIA,SENEGAL,AFRIKA KUSINI ZAENDELEA KUTAMBA

MASHABIKI WAZUSHA FUJO BAMAKO BAADA YA BAO LA DAKIKA YA MWISHO KUITOA MALI

NA MASHABIKI WA UJERUMANI KUTIA DOA KOMBE LA DUNIA 2006 ?

Mwishoni mwa wiki ilikua kinyan’ganyiro cha kuania Tiketi 31 za Kombe la dunia kanda mbali mbali duniani.Wenyeji Ujerumani walitolewa jasho na Slovenia jumamosi katika dimba la kirafiki na walimudu ushindi wa bahati tu wa bao 1:0-bao lililotiwa na Lukas Podolski wa FC Cologne mnamo dakika ya 27 ya mchezo.

Uligonga vchwa vya habari si ushindi huo wa Ujerumani dhidi ya Slovenia,bali fujo zilizofanywa na mashabiki wa Ujerumani kabla ya mechi hiyo ya kirafiki hapo jumamosi:

Shirikisho la dimba la Ujerumani DFB lilichukua hatua haraka kuomba radhi kwa Slovenia baada ya mashabiki wa Ujerumani kuvunja madirisha ya magari na ya mikahawa huku wakitoa matamshi ya kikabila katika mji wa Celje nchini Slovenia masaa kabla mechi kuanza.Machafuko zaidi yalizuka uwanjani ambako mashabiki wa Ujerumani walivurumisha uwanjani aina ya fashfashi na kupambana na Polisi wa Slovenia.

Kulizuka pia mapigano baina ya wajerumani na waslovenia nje ya Uwanja baada ya kumalizika mechi hiyo-kwa muujibu wa wakuu wa Ujerumani walivyoarifu.Polisi 2 wa Slovenia na mjerumani mmoja walijeruhiwa.

Wakuu wa Ujerumani waliarifu kwamba, walijua kuna kikundi cha wahuni wa kijerumani kati ya 200 na 250 na waliwaonya Polisi wa Slovenia.Ripoti za vyombo vya habari zinasema hasara waliotia mashabiki hao wa kijerumani imefikia Euro 12.500.

Franz Beckenbauer, mwenyekiti wa Tume ya maandalio ya kombe lijalo la dunia hapa Ujerumani, amesema kwsamba ushirikiano baina ya wakuu wa Ujerumani na Slovenia haukuwa mzuri.

Ujerumani kama mwenyeji wa Kombe lijalo la dunia 2006,haingependa kupata sifa mbaya wakati huu kuhusu mashabiki wake baada ya mkasa wa marifu na mchezo wa kamari.

KOMBE LA DUNIA 2006 KANDA YA AFRIKA:

Fujo pia limezuika katika kinyan’ganyiro cha kanda ya Afrika kuania tiketi za Kombe la dunia.Fujo lilizuka uwanjani jana na kusababisha mpira kuvunjwa kabla ya firimbi ya mwisho wakati wa mechi kati ya Mali na Togo.

mechi hiyo ikavunjwa huku maalfu ya mashabiki yakiuvamia uwanja mjini Bamako baada ya Togo kuufumania mlango wa Mali dakika ya 90 ya mchezo na kutia bao la ushindi kufanya 2:1 na kuiweka Mali ikuburura mkia wa kundi la kwanza.Polisi ikatumia hewa ya kutoa machozi na virungu kuwatawanya mashabiki waliokua wakimiminika majiani kandoni mwa Uwanja wa dimba wa bamako.magari kadhaa yalihujumiwa na watu wengi walijeruhiwa.

Chanzo cha fujo hilo lote ni bao la dakika ya mwisho ya mchezo (dakika ya 90) alilopachika Cherif Maman.Mali ikiongoza kwa bao 1-o kufuatia bao la Soumaila Coulibaly.Salifou Moustafa akaswazisha kwa Togo mnamo dakika ya 80.Ushindi huuumeiweka Togo safu moja na Senegal na zambia katika kinyan’ganyiro kikali kabisa cha kuania tiketi ya Kombe la dunia kutoka kundi hili.

Katika chgangamoto nyengine, bmabao 2 kutoka mshambulizi wa Chelsea ya uingereza,Didier Drogba yaliibakisha kileleni Ivory Coast.Tembo hao waliikanyaga benin kwa mabao 3:0 na sasa wanaongoza kundi lao la 3 kwa pointi 4 wakifuatwa na simba wa nyika-Kameroun.

Kameroun ilitia bao la dakika ya mwisho kuitoa Sudan kwa mabao 2:1.Ikicheza na wachezaji 10 tu kuanzia kipindi cha pili,Sudan ilizima vishindo vyote vya simba wa nyika, hadi muda wa kufidia pale Achille Webo alipotia tia bao lililowaokoa simba wa nyika na kubakisha tumaini la kukata tiketi yao ya 5 ya kombe la dunia.Hatahivyo, Kamerun ina kazi ngumu kuziba mwanya wa pointi 4 kati yake na Ivory Coast.

Angola ilizabwa mabao 2:0 na Zimbabwe mjini Harare.Nigeria lakini iko kileleni baada ya kuirarua Gabon kwa mabao 2:0 mjini Port hercourt.

Black Stars-Ghana ambayo kati ya wiki iliopita ilitoka suluhu na Harambee Stars-Kenya, mjini Nairobi, kama simba wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,zimeachwa nyuma na wenzao.Kongo imetoka sare bao 1:1 na Ghana mjini Kinshasa.Alikua Shabani Nonda aliewapatia simba wa Kongo bao lao.sare hii imeziacha Ghana na Kongo kila moja na pointi 9-pointi moja kuliko visiwa vya Cape Verde na tatu kutoka walipo bafana Bafana-Afrika Kusini.

Duru ijayo ya kinyan’ganyiro cha tiketi 5 za Afrika kwa Kombe lijalo la dunia kitakua Juni 3-5 na ni mshindi tu wa kila kundi ndie atakaetoroka na tiketi ya kuliwakilisha bara la Afrika hapa ujerumani katika Kombe la Dunia 2006.

Ama katika kanda ya Amerika Kusini,Argentina imebakia kileleni baada ya kutoka nyuma bao 1 na kuilaza mwishoe Bolivia 2:1 mjini La Paz.

Argentina inaongoza kanda ya Amerika kusini kwa pointi 2 ikifuatwa na mabingwa wa dunia Brazil.

Brazil ilitokwa na jasho kabla kuitoa Peru kwa bao 1:0.Mshambulizi wao Kaka alitia pia bao dakika za mwisho kuipatia Brazil pointi 3 na uwezekano wa kuja Ujerumani mwakani kutetea taji lake la dunia.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW