Kombe la Dunia 2010 laanza Afrika Kusini.
11 Juni 2010MILANGO IWAZI CITY STADIUM:
Milango ya City Stadium,Johannesberg, imeshafunguliwa hivi punde kwa Kombe la kwanza kabisa la dunia barani Afrika,miaka 80 tangu lilipochezwa kwa mara ya kwanza mjini Montevideo,Uruguay, 1930 nyumbani mwa timu inayoteremka pia leo uwanjani baada ya Bafana Bafana kucheza na Mexico ,ikiwa na miadi na makamo-bingwa wa dunia,Ufaransa.
BILA MANDELA UWANJANI:
Wakati mashabiki waliosubiri kwa hamu kuu siku hii ya historia wakimiminika uwanja City Stadium,Johannesberg,nje ya Soweto,huku wakipepea bendera za Afrika kusini na kupuliza matarumbeta ya Vuvuzela,mtu aliechangia mno kuja Kombe hili Afrika Kusini na Afrika kwa jumla, mzee Nelson Madiba Mandela,hatakuwapo uwanjani alaasiri hii kinyume na ilibvyotarajiwa :Mjukuu wake wa miaka 13 ,Zinani Mandela,amefariki dunia jana usiku wakati akirudi kutoka burdani ya kufungua Kombe la dunia.
Hatahivyo, bila ya Mandela uwanjani na licjha ya msiba huo, watoto wake Bafana Bafana, wanajua mpambano wa leo, ni wa kufa-kupona,kwani, sio tu wanatetea heba ya Afrika kusini, bali ya Afrika nzima,wakiwa mojawapo ya timu 6 za Afrika.Pili, Bafana Bafana ,wanaelewa itakuwa aibu kubwa kwa mwenyeji kuaga mashindano ya Kombe la dunia katika duru ya kwanza.
"Waliosema haliwi,limekuwa":Kombe la dunia, limewasili Afrika tena kwa kishindo.Uwanja wa City Stadium, ukichukua mashabiki 94,700, unatazamiwa kujaa pomoni leo,kwani," leo ni leo na asemae kesho-muongo".
BAFANA BAFANA NA MEXICO:
Mzigo mzito wa kikosi cha kocha Carlos Parreira, anao mchezaji wa kiungo Louis Pienaar,stadi pekee wa Bafana Bafana, anaetamba kila mara katika Ligi ya ulaya:Ni yeye msimu huu alieteuliwa "mwanasoka wa mwaka wa Everton" na kuna uvumi huenda akahamia Chelsea au hata Manchester United.
Mexico,inadai hata vuvuzela,zihanikize namna gani uwanjani hivi punde, wameapa kuwatilia Bafana Bafana, kitumbua chao mchanga.Wamexico, wanadai hata uwanja mzima ukisheheni mashabiki wanaopuliza vuvzela, watayazima .Wanasema kila timu ina wachezaji 11 na sio vuvuzela 1000.
Changamoto hii kati ya Bafana Bafana na Mexico, inatanguliwa hivi punde na burdani ,itayoingiza wachezangoma wa kiafrika na muziki ukiongozwa na mwimbaji mashuhuri R.Kelly.Shabiki mmoja ambae tangu asubuhi ya leo amepiga kambi City Stadium,alisema,
"Nimekuja hapa mapema ili nijionee kila kitu kuhusu siku hii ya kihistoria nataraji itakuwa siku ya kupendeza."
WAGENI WA NJE:
Mashabiki 300,000 kutoka nchi za nje , wanatarajiwa Afrika kusini kwa kombe hili la dunia litakalojionea mechi 64 kuanzia leo hadi Julay, 11 siku atakayotawazwa bingwa.Miongoni mwa waheshimiwa katika ufunguzi hivi punde, ni makamo-rais wa Marekani,Joe Biden,rais wa Mexico Felipe, Calderon na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.
Nani atashinda leo:Afrika kusini au Mexico ?
Mara nyingi mpambano wa ufunguzi, humalizika suluhu,lakini Bafana Bafana,hawataki chochote kasoro ya ushindi ili vuvuzela zihanikize Afrika nzima jioni hii.
Mwandishi: Ramadhan Ali/DPAE
Uhariri: Josephat Charo