Kombe la Dunia 2026: Je, Ulaya inaweza kuongoza mgomo?
22 Januari 2026
Kadiri uhusiano kati ya Ulaya na Marekani unavyoendelea kuzorota, wito wa nchi za Ulaya kugomea Kombe la Dunia la 2026 unaanza kupata uzito. Wanasiasa, makundi ya mashabiki na viongozi wa soka ni miongoni mwa wanaoamini kuwa hatua za serikali ya Rais Donald Trump — hususan kuhusiana na Greenland — zinafanya ushiriki wa Ulaya katika mashindano hayo kuwa wa kutatanisha.
Kwa kuzingatia historia ya Trump ya kubadilisha misimamo ghafla katika masuala mbalimbali, serikali za Ulaya zinaonywa kuwa tayari kwa hali yoyote ile, licha ya matamko ya baadaye kuwa muafaka kuhusu Greenland ulikuwa umefikiwa ndani ya Jumuiya ya NATO. Vivyo hivyo, mashirikisho ya soka barani Ulaya yanapaswa kuwa tayari kwa uwezekano huo.
Mogens Jensen, mbunge wa chama kikubwa zaidi bungeni Denmark, Social Democratic, na msemaji wa masuala ya utamaduni, vyombo vya habari na michezo, aliliambia DW kuwa Denmark — ambayo Greenland ni sehemu yake — bado haijatoa wito wa kugomea mashindano hayo.
"Kwa chama changu na kwa mtazamo wangu binafsi, tunaamini kuwa mgomo ni miongoni mwa zana za mwisho kabisa zinazopaswa kutumiwa,” alisema.
Hata hivyo, aliongeza kuwa hali hiyo inaweza kubadilika iwapo Trump atachagua kutumia nguvu za kijeshi.
"Nitakuwa mkweli: ndiyo, kama hilo litatokea, basi mjadala wa mgomo utakuwa muhimu sana,” Jensen alisema muda mfupi kabla ya Trump kupanda jukwaani katika mkutano wa Davos. "Inawezekana kabisa ikiwa hali itageuka kuwa mzozo wa kweli. Natumaini kwa dhati haitafikia hatua hiyo.”
Ripoti kutoka vyombo mbalimbali vya habari zinaeleza kuwa viongozi wa soka barani Ulaya, kupitia UEFA, walifanya mkutano Jumatatu uliowakutanisha wakuu wa mashirikisho kadhaa ya soka. Katika mkutano huo, ushuru wa asilimia 10 uliowekwa na Trump kwa nchi nane za Ulaya kutokana na suala la Greenland ulitajwa kuwa miongoni mwa hoja kuu.
Kati ya nchi hizo nane, Norway, Uholanzi, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza (kupitia England na Scotland) tayari zimefuzu kwa Kombe la Dunia la 2026. Denmark, Sweden na Ireland ya Kaskazini bado ziko kwenye hatua ya mchujo, huku Finland ikiwa tayari imeshindwa kufuzu.
Suala la mgomo halihusishi wanasiasa wa Denmark pekee. Nchini Ujerumani, baadhi ya viongozi wa kisiasa pia wameanza kulizungumzia. Roderich Kiesewetter wa chama tawala cha CDU, ambaye ni mjumbe wa kamati ya masuala ya nje, alisema kuwa hata hatua ya kijeshi huenda isiwe lazima ili kuhalalisha mgomo.
"Ikiwa Trump atatekeleza vitisho vyake kuhusu Greenland na kuanzisha vita vya kibiashara dhidi ya Umoja wa Ulaya, ni vigumu kufikiria nchi za Ulaya zikishiriki Kombe la Dunia,” aliambia gazeti la Augsburg Allgemeine.
Kwa upande wake, Waziri wa Michezo wa Ujerumani, Christiane Schenderlein, alisisitiza kuwa uamuzi wa kushiriki au kugomea mashindano makubwa ya michezo uko mikononi mwa mashirikisho ya michezo, si wanasiasa. "Maamuzi kama hayo yanapaswa kufanywa na mashirikisho ya michezo pekee,” alisema.
Hadi sasa, Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB) halijajibu ombi la DW kutoa maoni yake kuhusu suala hilo.
Hasira za mashabiki zaibua wito wa mgomo
Teun van de Keuken, raia wa Uholanzi, alisema amekata tamaa na kile anachokiona kama ukimya wa kisiasa mbele ya vitisho vya mwanachama mmoja wa NATO dhidi ya mwingine, pamoja na sera nyingine za Trump. Kutokana na hali hiyo, alianzisha ombi la kusisitiza mgomo nchini Uholanzi, ambalo tayari limekusanya zaidi ya sahihi 135,000 na linaendelea kuongezeka.
"Mashirikisho ya michezo mara nyingi husema hayataki kuchanganya michezo na siasa. Tatizo ni kwamba siasa tayari zimeingia kwenye michezo, na lazima uchukue msimamo,” alisema van de Keuken.
Kwa sasa, anatafuta njia ya kulipeleka ombi hilo kwenye jukwaa la kimataifa na kutumia kile anachoamini kuwa ni kutoridhika kwa mashabiki wengi kuhusu mashindano hayo.
Baadhi ya mashabiki wanaamini kuwa FIFA imekuwa karibu sana na Trump, jambo linaloifanya ipuuze misingi ya kutokuwa na upendeleo wa kisiasa. Wengine wana hofu kuwa Kombe la Dunia linaweza kutumiwa kama jukwaa la propaganda.
Mashaka haya yanaongezeka zaidi kutokana na ongezeko kubwa la bei za tiketi, ambazo sasa ni mara nne hadi tano zaidi ya zilivyokuwa wakati Kombe la Dunia lilipofanyika Qatar. Mashabiki wengi wanasema soka linageuzwa kuwa mchezo wa matajiri, huku mashindano makubwa yakizidi kuwafukuza watu wa kawaida.
Je, Ulaya inaweza kuungana ikihitajika?
Katika mazingira haya, UEFA inatarajiwa kufanya mkutano mwingine hivi karibuni, ambao huenda ukawa wa kihistoria. Ulaya ina timu 16 kati ya 48 zitakazoshiriki Kombe la Dunia la 2026, pamoja na vilabu vyenye nguvu zaidi duniani. Ikiwa bara hilo litaamua kugomea, athari zake zinaweza kuitikisa dunia nzima ya soka.
Ingawa kumekuwepo na maoni tofauti kutoka kwa wanasiasa wa Uingereza, Ufaransa na nchi nyingine — baadhi wakiunga mkono na wengine wakipinga mgomo — mabingwa wa Ulaya, Uhispania, huenda wakawa miongoni mwa nchi zitakazoongoza hatua yoyote ya pamoja.
Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sánchez, alikuwa miongoni mwa viongozi wachache waliotaka Israel iondolewe kwenye mashindano ya kimataifa ya michezo mwaka jana. Aidha, Uhispania na Uholanzi zilikuwa miongoni mwa nchi zilizogomea shindano la Eurovision kufuatia vita vya Gaza.
Hata hivyo, Rais wa Shirikisho la Soka la Norway, Lise Klaveness, alisisitiza kuwa mgomo hauwezi kufanywa na nchi moja pekee.
"Ikiwa mgomo utafanyika, lazima uwe wa pamoja, wa bara zima, alisema.
https://p.dw.com/p/57CdG