1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
KandandaKimataifa

Hatua ya makundi yafungwa kwa rekodi, drama na mshangao

28 Juni 2026

Hatua ya makundi ya Kombe la Dunia 2026 imefungwa baada ya mechi 72 zilizovunja rekodi. Lionel Messi ameendelea kung'ara, mataifa ya Afrika yameweka historia, huku drama ya dakika za mwisho ikihitimisha awamu hiyo kwa ki

Kombe la Dunia 2026 | Kombo ya Mbappé, Messi na Haaland wakicheza
Mchanganyiko wa picha unaowaonyesha Kylian Mbappé wa Ufaransa (kushoto), Lionel Messi wa Argentina (katikati) na Erling Haaland wa Norway wakicheza katika mashindano ya Kombe la Dunia, Jumatatu, Juni 22, 2026Picha: AP Photo/picture alliance

Hatua ya makundi ya Kombe la Dunia 2026 imehitimishwa baada ya mechi 72 za kusisimua zilizochezwa kwa siku 17, huku timu 48 zikichujwa na kubaki 32 zitakazowania ubingwa katika hatua ya mtoano.

Mashindano hayo yamefuta hofu kwamba ongezeko la timu lingeathiri ubora wa mchezo. Badala yake, yameshuhudia rekodi mpya, matokeo ya kushangaza na ushindani mkali katika makundi yote.

Mchezo wa mwisho wa hatua hiyo ulimalizika kwa drama kubwa baada ya mshambuliaji wa Austria, Saša Kalajdžić, kufunga bao la kusawazisha 3-3 dhidi ya Algeria katika dakika za mwisho kabisa za muda wa nyongeza.

Bao hilo halikuokoa Austria pekee, bali pia lilihitimisha rasmi hatua ya makundi na kufunga pazia la awamu iliyokuwa imejaa hisia, furaha na majonzi kwa timu mbalimbali.

Mabingwa watetezi Argentina, Ufaransa na wenyeji Mexico walimaliza hatua ya makundi kwa ushindi wa mechi zote tatu na kutuma ujumbe kuwa bado ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.

Lionel Messi wa Argentina akipiga shuti langoni huku Kevin Danso, Nicolas Seiwald, David Alaba na Konrad Laimer wa Austria wakitazama wakati wa Kombe la Dunia 2026 katika Uwanja wa AT&T mjini Dallas, Marekani, Juni 22, 2026Picha: Stefan Koops/EYE4IMAGES/NurPhoto/picture alliance

Messi aendelea kuandika historia

Lionel Messi ameendelea kuthibitisha ubora wake licha ya umri wa miaka 39. Nahodha huyo wa Argentina ndiye kinara wa mabao wa mashindano hadi sasa akiwa na mabao sita.

Mbali na kuwania kiatu cha dhahabu kwa mara ya kwanza, Messi ameweka rekodi ya mabao 19 katika historia ya Kombe la Dunia na kuwa mchezaji wa kwanza kufunga katika mechi saba mfululizo za fainali za Kombe la Dunia tangu mwaka 2022.

Cristiano Ronaldo wa Ureno, mwenye umri wa miaka 41, naye ameandika historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga katika mashinda sita tofauti ya Kombe la Dunia.

Luka Modrić wa Croatia, mwenye miaka 40, pia amejiunga na orodha ya wachezaji wakongwe waliofunga mabao, huku Kylian Mbappé, Ousmane Dembélé, Erling Haaland na Vinícius Júnior wakifikisha mabao manne kila mmoja.

Makipa Unai Simón wa Hispania na Raúl Rangel wa Mexico nao wameonyesha kiwango bora baada ya kumaliza hatua ya makundi bila kuruhusu bao lolote.

Cristiano Ronaldo ameweka rekodi ya kufunga bao katika mashindano sita tofauti ya Kombe la DuniaPicha: Leo Barrilari/Sports Press Photo/IMAGO

Afrika yaweka rekodi mpya

Bara la Afrika limeandika historia kwa kupeleka timu tisa katika hatua ya 32 bora, idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea katika Kombe la Dunia.

Cape Verde, inayoshiriki kwa mara ya kwanza, imekuwa moja ya hadithi kubwa za mashindano baada ya kutoka sare na Hispania, Uruguay na Saudi Arabia na kufuzu hatua ya mtoano.

Kipa Vozinha amekuwa mmoja wa nyota wa timu hiyo na sasa anatarajia kukutana na Lionel Messi na Argentina. Amesema kucheza dhidi ya Messi ni ndoto ya kila mchezaji wa soka.

Morocco pia imeonyesha kuwa mafanikio yake ya kufika nusu fainali mwaka 2022 hayakuwa ya bahati. Sare dhidi ya Brazil imeongeza matumaini ya kufanya vizuri zaidi mwaka huu.

Ghana iliizuia England kwa sare ya bila mabao, huku Côte d'Ivoire ikiwapa wakati mgumu Wajerumani kabla ya kufungwa mabao 2-1 katika dakika za mwisho.

Mlinda mlango wa Cape Verde Vozinha amekuwa mmoja ya vivutio vikubwa zaidi vya michuano ya mwaka huu, huku timu yake ikitinga hatua ya mtoano katika mara yake ya kwanza ya kushiriki Kombe la DuniaPicha: Amanda Perobelli/REUTERS

Changamoto na drama nje ya uwanja

Licha ya mafanikio ya baadhi ya timu, mataifa mengine yalikumbwa na changamoto kubwa nje ya uwanja. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliwasili mashindanoni huku ikikabiliwa na mlipuko wa Ebola nchini.

Iran ndiyo iliyokumbana na mazingira magumu zaidi. Timu hiyo ililazimika kuhamisha kambi yake kutoka Marekani kwenda Mexico kutokana na mvutano wa kisiasa kati ya Tehran na Washington.

Pia ilikabiliwa na masharti makali ya kuingia Marekani kwa ajili ya mechi zake, kabla ya kuondolewa kwa uchungu baada ya bao lake dhidi ya Misri kufutwa kupitia VAR katika dakika za mwisho.

Kocha Amir Ghalenoei alisema timu yake haikuathiriwa tu na mazingira ya kisiasa, bali pia ilikosa bahati uwanjani.

Iran ndiyo iliyokumbana na mazingira magumu zaidi katika Kombe la Dunia mwaka huu, na iliaga mashindano hayo huku ikilalamika kutotendewa hakiPicha: Carlos Barria/REUTERS

Mtoano waanza kwa presha mpya

Mashindano pia yameshuhudia rekodi mpya ya mahudhurio ya mashabiki viwanjani, huku karibu mechi zote zikichezwa mbele ya viwanja vilivyojaa.

Paraguay ilipata habari mbaya baada ya Miguel Almirón kuwa mchezaji wa kwanza kutolewa nje kwa kadi nyekundu chini ya sheria mpya zinazokataza kufunika mdomo wakati wa mabishano na mpinzani.

Ujerumani, iliyopata ushindi mkubwa zaidi wa mashindano kwa kuichapa Curaçao mabao 7-1, imefuzu lakini bado haijawashawishi wengi kuwa ndiyo timu ya kutwaa ubingwa.

Sasa hatua ya mtoano inaanza ambapo hakuna nafasi ya kufanya makosa. Timu 32 zilizosalia zitapambana kwa siku 10 zijazo kuelekea fainali ya Julai 19, huku kila mechi ikiwa ya kufa au kupona.

Kama alivyosema mkurugenzi wa michezo wa Ujerumani, Rudi Völler: "Kila kitu sasa kiko hatarini; ama unasonga mbele au unarudi nyumbani."

KAtika mechi ya kwanza ya hatua ya mtoano, Canada iliipiku Afrika Kusini kupitia bao la dakika za majeruhi na hivyo kusonga mbele katika hatua ya 16 bora.Picha: Daniel Cole/REUTERS
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW