Kombe la dunia la wadia-Brazil itaifunga tena Ujerumani ?
12 Mei 2006Tukianza na Bundesliga-ligi ya Ujerumani,kinyan’ganyiro wakati huu uwanjani-siku ya mwisho ya msimu kimetuwama katika kuania nafasi ya pili ya ngazi ya Ligi baada ya Bayern munich,kwishatwaa ubingwa wiki iliopita. Pia mkiani mwa Ligi,timu mbili zinapapurana ili kujua ipi itazama daraja ya pili na ipi itaokoka shoka la Bundesliga- Wolfsburg na Kaiserslauten.
Hamburg ikicheza jumamosi bila ya jogoo lao kutoka Holland, Rafael van der Vaart inaumana na Werder Bremen kuamua nani ataibuka makamo-bingwa na kukata tiketi ya champions League-kombe la klabu bingwa barani ulaya msimu ujao.Kwani, timu 2 za kileleni huingia moja kwa moja katika kinyan’ganyiro hicho.
Mkiani mwa Ligi,baada ya Duisburg na FC cologne, kuzama daraja ya pili wiki iliopita,leo ama Wolfsburg au kaiserslauten itakua timu ya tatu.sitapenda kuagua ni ipi kwahivyo, uwanjani wakati huu timu hizo mbili zinapigana kufa kupona.
Tukifungua pazia la Kombe la dunia,kuna wachezaji 2 wa kiafrika ambao mara ya mwisho kuziwakilisha timu zao za Taifa ilikua miaka 8 iliopita.Wanataka lakini kurejea kuvaa jazi za taifa katika kombe hili la dunia:nao ni Bachirou Salou wa Togo ambayo inawasili keshokutwa Ujerumani ikiwa ya kwanza kati ya timu 31 za kigeni kuwasili.
Mwengine ni Eric Addo wa Black Stars-Ghana, anaeichezea PSV Eindhoven ya Holland.Wote wawili wanatazamiwa kuteuliwa katika kikosi cha taifa kwa kombe la dunia.Ni maajabu.
Wachezaji hawa 2 kutoka nchi hizi mbili jirani kabisa zilizichezea timu zao za taifa kwa mara ya kwanza 1998 katika kombe la Africa la mataifa.Salou alikua kileleni mwa maisha yake ya dimba wakati salou mwanzoni akiwa chipukizi.
Kurejea uwanjani kwa Baschirou Salou kunatukumbusha mkasa wa Roger Milla wa Kameroun katika kombe la dunia 1990 huko Itali na Kombe la dunia la 1994 nchini Marekani.
Wakati ule alikua ameshastaafu.Akiichezea Borussia Dortmund na Duisburg pamoja na Eintracht Frankfurt,kiroja cha mambo,salou mara nyingi akikwepa kwenda kuichezea timu ya Taifa.Kombe la dunia lakini, ni swali jengine,halina kijana au mzee.
Na mzee Roger Milla amekwisha thibitisha hayo.Akiwa na umri wa miaka 35,Salou ameteuliwa kuichezea Togo kesho katika mpambano wa kujiandaa na Kombe la dunia dhidi ya saudi Arabia huko holland.
Ado nae akiwa sasa na umri wa miaka 27,aliichezea Ghana mara 3 tu siku za nyuma.Mara zote hizo katika Kom,be la Africa la mataifa 1998 alipokua chipukizi akiichezea Brugge ya Ubelgiji.
Kocha wa Ghana Dujkovic amemtupia macho Addo mwaka huu na ameshamchezeshea katika mapambano 2 ya kirafiki.Beki huyu mshahara nae huenda akaitwa katika kikosi cha Black Stars cha wachezaji 23.
Tusubiri kuona maarifa ya wakongwe hao 2 wa Ghana na Togo yatazusha maajabu gani mwezi ujao.
Kocha wa mabingwa wa dunia-Brazil carlos Albertob Parreira alibashiri juzi alhamisi kwamba, Brazil itawafunga wenyeji Ujerumani ikiwa timu hizi mbili zitakutana katika Kombe hili lijalo la dunia.
“Itakuwa uzuri ikiwa zitakumbana tena kama katika finali ya 2002, lakini tutashinda tena.” Alisema kocha huyo wa Brazil.
Brazil iliikomea Ujerumani mabao 2:0 katika finali ya Kombe la dunia huiko Yokohama,japan,na ikailaza tena Ujerumani 3-2 katika kinyan’ganyiro cha Confederations Cup,mwaka jana hapa Ujerumani.
Kombe la dunia limeshaanza kueneza homa yake kila pembe ya dunia,mirini,mitaani na hata vijijini.
Katika kijiji cha Matemwe,kaskazini-mashariki mwa Zanzibar, homa ya kombe la dunia nay mjini Stone-Town, kununua TV na kuzipakia hadi kijijini Matemwe-aiambia Radio Deutsche welle –katibu wa klabu ya pangamagae ya kijijini,wilaya ya kaskazini kundi Nyage Haji.
Huko Matemwe, asema Kundi,kuna wazimu wa mpira kweli.Wao huklo kinyume na mashabiki wengi wa visiwani,wanaamini Ghana itatoroka na Kombe la dunia,licha ya kuwa inacheza kwa mara ya kwanza.
Kundi Nyange haji anafurahia kuwa timu ya taifa ya Zanzibar kwa muujibu wa fununu itafunga safari karibuni kuja tena Ujerumani na kuwapo huko wakati wa Kombe la Dunia litakapoanza.ZANZIBAR FOR FIFA-lilikuwa biramu lao walipokuja ‘Zanzibar Heroes’ mwaka jana Ujerumani na kucheza mechi kadhaa huko Hannover.Bado Zanzibar inapiga hodi kutaka uanachama wa FIFA.