Kombe la Dunia laanza rasmi, Brazil yaishinda Croatia
13 Juni 2014Polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi na risasi za mipira dhidi ya waandamanaji wanaopinga mashindano hayo mjini Sao Paulo.
Lakini mabingwa hao mara tano wa kombe la dunia Brazil waliwashangaza mashabiki wao baada ya kufungwa goli ambalo limetokana na mchezaji wa Brazil dakika 11 tu tangu kuanza mchezo huo wa ufunguzi katika uwanja wa Corinthians mbele ya mashabiki 61,600 ikiwa ni pamoja na wakuu wa nchi 12.
Marcelo akaribia kuangua kilio
Mlinzi Marcelo alikaribia kutiririka machozi baada ya kuusindikiza mpira katika wavu wake kutokana na krosi iliyopigwa na Ivic Olic wa Croatia. Lakini mshambuliaji shujaa wa Brazil Neymar alisawazisha katika dakika ya 29 ya mchezo huo. Brazil ikashinda kwa mabao 3-1.
Polisi wa Brazil walijenga ukuta mduara wa chuma kuzunguka uwanja huo kuwazuwia waandamanaji kusogelea eneo hilo ambalo tamasha hilo kubwa la kandanda litaendelea kwa muda wa wiki nne, ambapo Brazil imetumia kiasi ya dola bilioni 11 kutayarisha.
Lakini waandamanaji waliokuwa na nia ya kuchafua sherehe hizo wakivalia mashati meusi na kujifunika nyuso zao waliwasha moto kwa kutumia takataka , kilometa chache kutoka katika uwanja huo baada ya polisi wenye silaha kujaribu kutuliza ghasia katika saa kabla ya kuanza kwa ufunguzi wa fainali hizo.
Maandamano yaendelea
Matayarisho ya kombe la dunia yamechafuliwa na miezi kadha ya maandamano, yakiakisi hasira za umma kuhusiana na matumizi ya fedha za maandalizi.
Lakini mji wa Sao Paulo na miji mingine kwa kiasi kikubwa ilikuwa tulivu wakati mchezo ulipoanza. Bendera za rangi ya njano na kijani zilipepea katika majengo mengi.
Lakini waandamanaji ambao walisababisha vurugu kubwa wakati wa kombe la mabara , Confederations Cup, mwaka jana wameapa kuandamana katika uwanja wa Sao Paulo.
Kocha Kovac akasirishwa na penalti
Kocha wa Croatia Niko Kovac ambaye alikuwa na hasira amesema mwamuzi kutoka Japan aliyesimamia pambano hilo la jana alikuwa hayuko katika kiwango chake, baada ya kutoa penalti kwa Brazil ambayo imebishaniwa na kubadilisha kabisa mwelekeo wa mchezo huo wa ufunguzi.
Croatia ambayo iko katika nafasi ya 18 ya orodha ya FIFA ya timu bora duniani , ilikuwa ikijaribu kuzuwia na kuwatuliza Brazil katika kipindi cha pili hadi pale refa Yuichi Nishimura alipoamua upigwe mkwaju wa penalti baada ya mshambuliaji wa Brazil Fred kuanguka wakati akipambana na mlinzi wa Croatia Dejean Lovren.
"Iwapo kuna mtu ameona kuwa ile ilikuwa penalti, anyooshe mkono. Siwezi kunyoosha mkono. Sikuona penalti, amesema kocha Kovac.
Kabla ya mchezo huo shabiki huyu aliifagilia Brazil na kusema:
"Brazil ina nafasi nzuri sana. Kikosi chake ni kizuri sana, upande wa mashambulizi na ulinzi pia."
Jioni ya leo(13.06.2014) Simba wa nyika , Cameroon , wataingia uwanjani kupambana na Mexico katika mchezo mwingine wa kundi A, wakati mabingwa watetezi Uhispania inaanza kampeni ya kurelijesha taji hilo mjini Madrid kwa kupambana na Uholanzi katika mchezo wa kundi B.
Mwandishi: Sekione Kitojo/AFPE
Mhariri:Josephat Charo