Kombe la Dunia: Morocco ina mengi ya kuthibitisha
5 Juni 2026
Morocco imejikuta katikati ya utata baada ya kuandaa toleo la hivi karibuni la Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) — miaka mitatu baada ya Simba wa Atlas kuingia kwenye historia kama timu ya kwanza ya Afrika kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia la 2022.
Safari ya kushangaza ya Morocco hadi nusu fainali katika mashindano ya Qatar — ikiwa na ushindi wa hatua ya mtoano dhidi ya Uhispania na Ureno, mataifa ambayo ufalme huo utaandaa nayo Kombe la Dunia la 2030 —uliibua hamasa kwa mashabiki na kuleta mshikamano barani Afrika.
Lakini fainali yenye vurugu ya AFCON dhidi ya Senegal mwezi Januari bado iko kwenye kumbukumbu, baada ya Morocco kutangazwa bingwa miezi miwili baada ya kufungwa 1-0 katika muda wa nyongeza.
Bingwa wa Afrika?
Senegal awali ilikabidhiwa kombe la AFCON baada ya kuifunga Morocco Januari 18 mjini Rabat. Lakini Shirikisho la Soka Afrika (CAF) liliinyang'anya Senegal taji hilo Machi 17 baada ya kuamua kwamba Senegal ilipaswa kupoteza mchezo huo kwa sababu wachezaji wake walitoka nje ya uwanja kupinga uamuzi wa penalti ya dakika za mwisho kabla ya kurejea baadaye kumalizia mchezo.
Uamuzi huo uligeuza ushindi wa Senegal wa 1-0 katika muda wa nyongeza kuwa ushindi wa mezani wa 3-0 kwa Morocco.
Senegal imekata rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) yenye makao yake Uswisi. Timu hiyo pia ilipiga gwaride la kombe hilo mjini Paris.
Sherehe za Morocco zimekuwa za chini kwa sababu rufaa hiyo bado haijatoa uamuzi.
Wachezaji wa Morocco watakuwa na afueni kuachana na siasa za nje ya uwanja na kurejea kucheza soka baada ya athari zote za uamuzi wa kipekee wa CAF.
Simba wa Atlas watamenyana na mabingwa mara tano Brazil katika uwanja wa New York New Jersey Juni 13, kisha Scotland katika uwanja wa Boston siku sita baadaye. Mchezo wao wa mwisho wa Kundi C utakuwa dhidi ya Haiti mjini Atlanta Juni 24.
Mafanikio katika mashindano haya yanayoandaliwa na Canada, Mexico na Marekani ni muhimu kwa taifa ambalo limewekeza pakubwa katika kujijenga kama nguvu ya soka duniani. Uandaji wa Kombe la Dunia 2030 ni sehemu tu ya mkakati huo.
Mabadiliko ya benchi la ufundi
Kocha Walid Regragui, aliyekiongoza kikosi cha Morocco, kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022 muda mfupi baada ya kuteuliwa, alijiuzulu baada ya AFCON mwezi Januari — miezi michache kabla ya CAF kuwatangaza Morocco kuwa mabingwa.
Licha ya mafanikio makubwa ya Kombe la Dunia, Regragui alikosolewa kwa mtindo wa uchezaji wa timu na pia kwa matokeo hafifu katika AFCON ya 2023 nchini Ivory Coast.
Mohamed Ouahbi, aliyeliongoza timu ya vijana ya Morocco chini ya miaka 20 kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia cha Vijana mwaka 2025, alichukua nafasi yake na kuiongoza timu kupata sare dhidi ya Ecuador na ushindi dhidi ya Paraguay katika mechi za maandalizi mwezi Machi.
Kwa sasa, macho yote yanabaki kwa Morocco — taifa lililojenga hadhi mpya katika soka la dunia, lakini linaloingia Kombe la Dunia likiwa na maswali mengi kuliko majibu. Je, Simba wa Atlas wataweza kugeuza sintofahamu ya miezi iliyopita kuwa nguvu ya ushindi? Au je, mizigo ya migogoro, majeraha na mabadiliko ya benchi la ufundi itawapunguzia kasi?
Majibu yote yatapatikana uwanjani, ambako siasa, rufaa na kumbukumbu za AFCON hazitakuwa na nafasi. Ni dakika tisini tu zitakazoamua hadithi mpya ya Morocco — iwe ya kujenga upya hadhi yao, au kuanguka chini ya matarajio ya bara zima.