1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la dunia: Ni Ufaransa na Croatia katika fainali

Sekione Kitojo
15 Julai 2018

Croatia inakwaana na Ufaransa mjini Moscow leo Jumapili (15.07.2018) ikijaribu kunyakua taji la kombe la dunia kwa mara ya kwanza,wakati  kikosi cha kocha Didier Deschamps kinalenga kupata taji lake la pili, tangu 1998.

Fußball WM 2018 Uruguay - Frankreich
Picha: Reuters/G. Dukor

Ufaransa  pia itaongezwa  nguvu kwa  kujaribu  kuweka  kando hali ya kukatisha  tamaa baada ya  kushindwa  katika  fainali  ya  kombe  la  mataifa ya  Ulaya  Euro 2016 dhidi  ya  Ureno mjini  Paris.

Ni fainali  ambayo  watu  wachache walitarajia wakati  tamasha  hilo  kubwa  la kandanda  duniani  lilipoanza wiki  nne  zilizopita. Croatia imeleta  furaha katika  taifa  hilo  la  Balkanambalo  lina  wakaazi milioni 4 tu kwa kuenda kinyume  na  hali  ya  kawaida  na  kusongambele  hadi  katika  fainali wakati mabingwa  watetezi Ujerumani , na  kisha  Argentina  na  Brazil  ziliangukia pua nchini  Urusi.

Shabiki wa Croatia akiwa amejipamba kwa rangi za bendera ya nchi yakePicha: Imago/V. Sharifulin

Wametiwa hamasa na mchezaji  wa  kati mtaalamu Luka  Modric wakati kocha  wake Zlatko  Dalic , ambaye aliichukua  timu  hiyo mwaka  jana tu wakati  kikosi  hicho  kikiwa  katika  hali  ya  mtafaruku, ameweza  kukiweka sawa  na  kucheza  vizuri.

Deschamps atakuwa  mtu  wa  tatu  kuweza  kushinda  kombe la dunia  akiwa mchezaji na  kocha, alikuwa nahodha  wa  timu  ya  taifa  ya  Ufaransa iliyobeba  kombe  la  dunia  mwaka  1998.

Kikosi chake cha timu  ya  taifa  ya  Ufaransa, kikiongozwa  na mshambuliaji wenye  umri  wa  miaka  19 Kylian Mbappe pamoja  na mchezaji mwenye uzoefu zaidi Antoine Griezmann, wanapigiwa  upatu  kushinda.

Paul Pogba hatimaye  amekuwa  kiongozi  katika  sehemu  ya  kati  kwa Ufaransa  na  N'Golo Kante ametimiza  wajibu  wake  kwa  kufanyakazi  bila kuchoka hali  ambayo  inawaruhusu  wenzake kung'ara, huku Samuel Umtiti na  Raphael Varane ni kitovu  cha  ngome imara.

Wachezaji wa Croatia wakipambana na wenyeji UrusiPicha: Reuters/M. Shemetov

Les Bleus

Les Bleus walikuwa  na  kibarua  kigumu  kupita  katika  awamu  ya  makundi, wakiiangusha  Australia na  Peru kwa  bao  moja  tu  na  kutoka  sare na Denmark katika  pambano  pekee  ambalo  lilitoka  sare  bila  ya  wavu kutikiswa  katika  mashindano  haya.

Na ghalfa  kikosi  hicho  kikaanza kucheza  vizuri, kikiiweka  kando Argentina katika  mchezo ambao  ulimtangaza  duniani  mshambuliaji Kylian Mbappe kwamba  yuko  tayari  kuingia  katika  jukwaa  la nyota  wa  kimataifa wakati alipopachika  mabao  mawili  na  kumfunika Lionel Messi.

Lakini  licha  ya  ushindi  wa  mabao 4-3, Ufaransa  ilicheza  kama kikosi  cha Deschamps, kikiwa  na  msisitizo mkubwa  katika  ulinzi.

Kocha Didier Deschamps (kushoto)Picha: picture-alliance/dpa/Kyodo/Maxppp

Uwanja  wa  Luzhniki wenye uwezo  wa  kuingiza watazamaji 80,000 utakuwa ndio  jukwaa  la  fainali  hii, lakini  sherehe  kubwa  zaidi  zitafanyika  mitaani katika  nchi  itakayoshinda.

Mamia  kwa  maelfu ya  watu  walimiminika  katika  mtaa  wa  Champs-Elysee mjini Paris baada ya ushindi  wa  Ufaransa  katika  nusu  fainali  dhidi  ya Ubelgiji na  matumaini  nyumbani  yako  juu.

Croatia imeonesha uwezo wa kupambana  zaidi  na kuhimili michezo mitatu ambayo  imekwenda  katika  dakika  za  nyongeza, bao  la  ushindi  la Mario Mandzukic katika  dakika  ya  109 lilitosha  kuwaangusha  England  katika nusu  fainali siku  ya  Jumatano.

Kocha Dalic  amesema yuko tayari kufanya  mabadiliko kwa  ajili  ya  fainali iwapo wachezaji  wake  watashindwa  kurejea  katika  hali  ya  kawaida kutokana  na majeruhi.

Ubelgiji iliyoshika nafasi ya tatu katika kombe la dunia 2018Picha: Reuters/G. Garanich

Jana Jumamosi(14.07.2018) Ubelgiji ilifanikiwa  kuchukua  nafasi  ya  tatu katika  fainali  hizi  za  kombe  la  dunia  kwa  kuiangusha  tena England kwa  mabao 2-0. 

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Caro Robi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW