1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la klabu bingwa Afrika laendelea

Ramadhan Ali17 Julai 2006

Baada ya mahkama ya spoti nchini Itali kuiteremsha Juventus Turin daraja ya pili kwa kupangilia matokeo ya mechi,kocha wao mpya Mfaransa Didier Deschamps anasema itakua taabu sana kuirejesha klabu hiyo bingwa daraja ya kwanza mnamo muda wa mwaka mmoja.

Kocha wa Black Stars-Ghana-amejizulu wiki tu tangu kumalizika kwa kombe la dunia.

Katika changamoto za kombe la klabu bingwa barani Afrika, Hearts of Oak ya Ghana; ilizabwa mabao 2:0 nyumbani na enyimba ya Nigeria na Moro United ya Tanzania iliozabwa mabao 4:1 jana na Etoile du Sahel ya Tunisia,inajiwinda kufuta mabao hayo duru ijayo nyumbani katika kombe la CAF.

Michael Schumacher atamba katika mbio za magari Ufaransa:Hayo na mengineo.Ndio niliopwaandalia jioni hii:

Mwishoni mwa wiki,mahkama ya michezo nchini Itali iliiteremsha daraja ya pili klabu bingwa YA Itali-Juventus kwa kupangilia matokeo ya mechi na kuivua mataji 2 ya ubingwa ya miaka 2 iliopita.

Hii ni mojawapo ya hatua za kupitisha ufagio wa chuma kusafisha uchafu katika Seria A-Ligi ya Itali.Lazio Roma na Fiorentina pia kama Juventus; zimeteremshwa daraja ya pili wakati AC Milan imevuka salama na inabaki daraja ya kwanza isipokuwa imepunguziwa pointi 15 na haitacheza katika kinyan’ganyiro chochote cha vikombe vya ulaya .

Miongoni mwa adhabu kali zilizotolewa kwa wakuu wa vilabu binafsi ni ile aliopewa mkurugenzi mkuu wa Juventus; Antonio Giraudo aliepigwa marufuku kwa miaka 5 kwa kupangilia mechi.

Kocha mpya wa Juventus, mfaransa Didier Deschamps ,amesema itakua vigumu kuirejesha Juventus daraja ya kwanza mnamo muda wa mwaka mmoja.Kwani kuziba mwanya wa pointi 30 ili Juventus ipande ni kazi isiowezekana.

Katika dimba barani Afrika, Kocha wa Ghana aliewaongoza Black Stars katika Kombe la dunia,Serbian Ratomir Dujkovic ,amejiuzulu akitoa sababu za afya.Hii ni kwa muujibu wa shirikisho la dimba la Ghana .Mkataba wa miaka 2 wa mserbia huyo ulikua umalizike mwisho wa mwaka huu.Dujkovic aliondoka nchini Ghana ijumaa iliopita.Duru za habari zinasema kwamba kocha huyo ametakiwa kuwa kocha na timu za taifa za Serbia na hata Azerbaijan pamoja na klabu kadhaa za Mashariki ya kati.

Chini ya kocha Djukovic ,Ghana ikicheza mara ya kwanza katika Kombe la dunia ilikua timu pekee kati ya 5 za afrika kukata tiketi ya duru ya pili.Ilirudishwa nyumbani na Brazil baada ya kukomewa manao 3:0.Ghana lakini ilimudu kuitoa Jamhuri ya Czech na Marekani.

Katika changamoto za Kombe la klabu bingwa barani Afrika mwishoni mwa wiki, Hearts of Oak ya Ghana ilizubaa jana tena nyumbani na kuiachia enyimba ya Nigeria kuizaba mabao 2-0.Enyimba iliotwaa kombe hili la klabu bingwa barani afrika mara 2-2003 na 2004,ikiongoza kwa bao 1:0 katika kipindi cha mapumziko.

Hearts of oak,mabingwa wa kombe hili miaka 6 nyuma walicheza mpambano huu huko Obuasi kutokana na marekebisho yanayofanyiwa uwanja wa Taifa mjini Accra ikijiandaa Ghana kwa changamoto za Kombe la Afrioka la mataifa 2008.

Tayari jumamosi, mabingwa watetezi Al Ahli ya misri walishindwa kwa mara ya kwanza katika bara la afrika na CS Sfaxien ya Tunisia.JS Kavylie ya Algeria .

Ama katika kinyan’ganyiro cha Kombe la shirikisho la dimba la Afrika-Etoile du sahel ya Tunisia iliikumta jana Moro United ya Tanzania kwa mabao 4:1.Moro inasema haijasalim amri na hivyo inajiwinda kupanda mlima kilim,anjaro duru ijayo nyumbani.Itapaswa Moro United-asema muandishi wetu mjini Dar-es-salaam, kufuta ushindi huo wa Etoile kwa mabao 4:0.

Wanariadha wa Afrika walitamba mwishoni mwa wiki katika mashindano ya kimataifa ya riadha mjini Roma,Itali:

Kenenisa Bekele wa Ethiopia alinguruma kama simba katika mbio za masafa ya mita 5000.Mqatar wa asili ya Kenya, Saif Saeed Shaheen, alibidi kuridhika na nafasi ya pili.Isaac Sangok wa kenya alimaliza watatu.

Upande wa wanawake katika masafa haya, ushindi pia ulikwenda kwa Ethiopia:Tirunesh Dibaba alichukua nafasi ya

kwanza ,akifuatwa na Meseret Defar huku Gelete Burika akichukua nafasi ya tatu.

Katika changamoto ya mita 1500,mkenya Daniel Kipchirchir Komen ambae amempiku Rashid ramzi wa bahrein.Adil Kaouch wa Morokko alikuja watatu.

Ushindi mwengine wa Kenya ulikuja katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi,Paul Kipsiele aliwaongoza wakenya wengine 2 kuchukua nafasi ya kwanza,yapili na ya tatu kama desturi yao.Richard Matelong alikuja nafasi ya pili wakati Brimin Kipruto alichukua nafasi ya tatu.

Ujerumani imetwaa kombe la kwanza la ubingwa wa hoki duniani kwa wanawake hapo jana baada ya kuilaza China kwa mabao 3-2 huko Amsterdam.Taji hilo linaongezea medali ya dhahabu waliopata katika michezo ya Olimpik mjini Athens,Ugiriki.

Holland ilichukua medali ya shaba ikiachia China ile ya fedha.

Katika mbio za magari za Formula 1 za Grand Prix nchini Ufaransa, michael schumacher wa Ujerumani alinyakua ushindi wake 8 na hivyo amepunguza mwanya wake wa pointi kutoka Alonso kuwa pointi 17.Alonso ana pointi 96 wakati schumacher anaendesha motokaa za fararri ana pointi 79.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW