1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la klabu bingwa la Afrika-Bundesliga

Ramadhan Ali12 Februari 2007

Simba ya Tanzania yapigwa kumbo nje ya vikombe vya CAF na Ronaldinho arudi kutamba katika La Liga.Ronaldo aichezea AC Milan kwa mara ya kwanza.

Katika Kombe la CAF-shirikisho la dimba la Afrika, simba ya Tanzania, imeshindwa kunguruma mbele ya Textile pingue ya msumbiji,Wizara ya ndani ya Afrika Kusini imemsimamisha kazi kocha wa Bafana Bafana-mbrazil Carlos Parreira kwa kuwa hana kibali cha kufanya kazi nchini.Rekodi 2 za riadha zawekwa katika mashindano ya ukumbini-indoors huko Karlsruhe,kusini mwa Ujerumani.

LIGI BARANI ULAYA:

Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich, waliitandika jana Armenia Bielefeld bao 1:0 na kumpa kocha wao mpya na wa zamani ottmar Hitzfeld, makaribisho mazuri nyumbani.

Roy Makaay aliufumania mlango wa Bielefeld tayari mnamo dakika ya 8 ya mchezo na sasa Munich iko nafasi ya 4 ya ngazi ya ligi inayoongozwa na Schalke 04,ikifuatwa na Werder Bremen.Mara tu firimbi ya mwisho kulia, kocha wa Bielefeld alijiuzulu.

Katika Premier League-Ligi ya Uingereza,Manchester United, imeilaza Charlton Athletic kwa mabao 2:0 na kuseleleza mwanya wake wa pointi 6 kutoka mabingwa Chelsea walioilaza Middlesbrough 3-0.

Taarifa kutoka London, zasema serikali ya Uingereza itaungamkono ombi lolite madhubuti la chama cha mpira cha UIngereza kutaka kuandaa Kombe la dunia 2018-hii ni kwqa muujibu wa waziri wa fedha Gordon Brown.

Katika La Liga-ligi ya Spain, Ronaldinho,amerudi tena kutamba alipotia mabao 2 kuipa ushindi FC Barcelona dhidi ya Racing Santender.

Huko Itali, Ronaldo aliingia uwanjani kwa mara ya kwanza kuichezea AC Milan lakini katika uwanja uliojaa nusu mashabiki wa san Siro .AC Milan iliikomea Livorno mabao 2:1.Inter Milan ilishinda mabao 2:0 bila taabu nyumbani mwa Chievo Verona.

Katika Ligi ya Ubelgiji, Anderlecht imesawazisha pointi kileleni na Racing Genk baada ya kutoka suluhu 2:2 na Bruges.

Timu ya Taifa ya Afrika Kusini, ilimuajiri aliekua kocha wa Brazil Carlos Parreira kuwa kocha mpya ili kuiandaa kwa kombe lijalo la dunia 2010 nyumbani.Ilifanya yote isipokuwa ilisahau kumpatia ruhusa ya kufanya kazi nchini.

Wizara ya ndani ya Afrika kusini kwahivyo, imekipiga faini chama cha mpira cha Afrika kusini dala 2,800 kwa madhambi hayo na imemtaka kocha huyo wa Taifa, Carlos Parreira kusimamisha kazi kwavile, hana hati ya kumruhusu kufanya kazi.

Katika changamoto za vikombe vya klabu bingwa barani Afrika, mjini Brazzaville,Etoile du Congo ilitamba kwa mabao 2:0 mbele ya Canon Yaounde wakati mjini Freetown,Sierra Leone, FC Kallon kama ilivyoahidi imewika tena mbele ya Ocean Boys ya Nigeria kwa bao 1:0.

Katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,TP Mazembe ilinguruma kwa mabao 4:2 mbele ya Police ya Botswana.

Katika changamoto ya kombe la CAF Simba ya Tanzania nayo ilishindwa kunguruma mbele ya wanamsumbiji Textile Pangue baada ya kutoka suluhu duru iliopita bao 1:1 kama vile mwanamichezo wetu Gorge Njogopa anavyosimulia kutoka Dar-es-salaam:

Ama msiba sawa na huo umezisibu pia timu za Afrika ya kati: Bakari Ubena mwanamichezo wetu huko anaripoti kutoka Bujumbura kwamba, timu zote 2 za Burundi zimeweka matanga kwa huzuni ya kupigwa kumbo na mapema .Vitalo ilikandikwa bao 1:0 na Zamalek ya Misri wakati St.Eluoi Lupupo ya J.K.Kongo imechapwa mabao 2:0 na APR –timu ya Jeshi la Rwanda.

Katika mashindano ya riadha ya ukumbini-indoors mjini Karlsruhe,kusini mwa Ujerumani,Muamerika mzaliwa wa Kenya, Bernard Lagat alishinda mbio za mita 1000 kwa muda wa dakika 2:18.12 sek.

Mkenya Isaac Songok aliwika katika mbio za mita 3000 akifuiatwa nafasi ya pili na mkenya mwengine Boniface Songok.Ahmed Baday wa Morokko alimaliza watatu nyuma ya wakenya hao 2.

Rekodi 2 za dunia ziliwekwa katika mashindano hayo ya ukumbini:

Bingwa wa olimpik wa China wa masafa ya mita 110 kuruka viunzi Liu Xiang, aliweka rekodi mpya ya bara la Asia kwa mbio za masafa ya mita 60.

Timu ya wanariadha wakike ya Russia iliweka rekodi ya dunia katika masafa ya mita 800X4.Muda wao ulikuwa dakika 8:18.54.