1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Mataifa ya Afrika-Misri

Charles Hilary8 Februari 2006

Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika,kule Misri sasa kinachosubiriwa ni fainali itakayopigwa siku ya Ijumaa tarehe 10 mwezi huu katika uwanja wa Cairo.

Tunisia na Nigeria robo fainali.
Tunisia na Nigeria robo fainali.Picha: PA/dpa

Fainali hiyo itazikutanisha moja ya timu itakayowakilisha Afrika katika kombe la dunia,Ivory Coast na wenyeji Misri,ambapo Ivory Coast ilipata tiketi hiyo kwa kuifunga Nigeria bao moja kwa sifuri,il-hali Misri waliibugiza Senegal mabao 2-1.

Tukiangalia matukio baada ya mechi za nusu fainali,mshambuliaji hatari wa wenyeji Misri,Mido,ametimuliwa kutoka kikosi cha timu ya Taifa ya Misri kinachoshiriki mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika na amesimamishwa timu ya taifa kwa kipindi cha miezi sita kufuatia kubishana na kocha wake Hssan Shehata.

Ahmed Hossam Mido alimtolea maneno machafu kocha wake Shehata na kuonesha hasira baada ya kutolewa katika mechi ya nusu fainali walipocheza na Senegal na nafasi yake ikachukuliwa na Amr Zaki ambaye dakika moja tu tangu alipoingia aliweza kupachika bao la pili na la ushindi kwa Misri,lililoipeleka hatua ya fainali.

Mido alimtolea matusi mazito kocha wake Shehata baada ya kutolewa nje.Kwa maana hiyo sasa mshambuliaji huyo hatocheza mechi ya fainali siku ya Ijumaa baina ya Misri na Ivory Coast.

Kwa upande wa Senegal,mshambuliaji wa timu hiyo Diouf amesema kwamba Senegal ilitaka kuondoka katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Misri wakiwa kifua mbele,licha ya kutolewa kwa mara ya pili kwenye mashindano kama hayo tena kutokana na utata wa mwamuzi wa mchezo huo.

Kufungwa kwa Senegal mabao 2-1 na Misri,kulichangiwa sana na refarii kutoka Cameroon Divine Evehe,ambaye alikataa kuipatia Senegal mkwaju wa penalti,ambapo ilionekana dhahiri mshambuliaji wa Senegal Diomansy Kamara akiangushwa ndani ya eneo la hatari dakika za mwishomwisho za mchezo.

Kwa Diof pamoja na wachezaji wenzake wa Senegal,jambo kama hilo ilionekana wamelizoea kwani ilishawatokea miaka miwili iliyopita nchini Tunisia,ambapo walifungwa bao moja kwa sifuri na wenyeji.

Kocha wa Senegal wa wakati huo Guy Stephen alitoa shutuma za kutolewa hatua ya robo fainali kutokana na refarii kuvurunda baada ya kutotoa adhabu ya free kick kutokana na Diof kuchezewa madhambi katika eneo la lango la Tunisia.

Wakati huo Diof alipewa kadi nyekundu baada ya kuonekana alichochea fujo za wachezaji wake.

Kwa upande mwengine wezi walivamia vyuma vinavyokaliwa na wachezaji wa timu ya taifa ya Nigeria na kufanikiwa kuondoka na maelfu ya dola za wachezaji hao pamoja na mali nyingine za wachezaji.

Kiungo wa timu hiyo anayechezea pia Marseille,Wilson Oruma ameripoti kuibiwa dola 6,000,wakati golkipa Dele Aiyenugba ambaye pia huchezea klabu ya Enyimba alidai ameibiwa dola 2,500.Wachezaji wengine wa Nigeria waliarifu kuibiwa simu zao za mkononi na vitu vingine.

Tukio hilo lililotokea katika hoteli ya Hilton Green Plaza mjini Alexandria na tayari linashughulikiwa na polisi.

Nigeria inasubiri kupambana na Senegal kesho katika kumtafuta mshindi wa tatu mjini Cairo,baada ya timu zote kutolewa katika hatua ya nusu fainali hapo jana.