1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Mataifa ya Afrika sasa nusu fainali

6 Februari 2012

Mashindano ya kandanda ya Kombe la Mataifa ya Afrika sasa yameingia nusu fainali baada ya michuano ya robo fainali ya mwisho wa wiki, huku waandalizi wa mashindao hayo, Gabon na Guinea ya Ikweta, zikiyaaga.

Mechi ya Tunisia na Ghana
Mechi ya Tunisia na GhanaPicha: dapd

Tunisia na Sudan pia zimefunga virago kurudi nyumbani. Guinea ya Ikweta ilikandikwa nyumbani na Cote d´Voire Jumamosi mabao matatu kwa bila huku Didier Drogba akiuona wavu mara mbili. Zambia nayo ikaiadhibu Sudan pia mabao 3-0 .

Jumapili (05.02.2012) Gabon nayo ikasalimu amri pia nyumbani mjini Libreville baada ya kutolewa kwa mikwaju ya penalty na Mali mabao 5-4 baada ya kuwa sare 1-1 katika dakika 120 za kumsaka mshindi, zikiwemo 30 za muda wa ziada.

Katika robo fainali nyengine jana usiku Ghana liitandika Tunisia mabao 2-1 baada ya kuongezwa wakati. Timu hizo zilimaliza dakika 90 za kawaida zikiwa sare 1-1. Bao la ushindi la Ghana lilipatikana katika dakika zile dakika 30 za nyongeza, wakati mlinda mlango wa Tunisia alipojaribu kuudaka mpira wa juu kutoka wingi ya kulia na mpira huo kumtoka ukishukia mguuni mwa nahodha wa Ghana, John Mensah aliyeuweka wavuni. Ghana itacheza nusu fainali na Zambia hapo Jumatano wakati Cote d´Ivoire itaumana na Mali. Michuano ya jana ilitazamwa na wengi barani Afrika.

Kandanda na ghasia za uwanjani

Ulimwengu wa kandanda hadi sasa ungali umegubikwa na matukio ya wiki iliopiata nchini Misri ambapo watu karibu 73 waliuawa katika ghasia zilizozuka mjini Port said katika pambano kati ya Al Masry na Al Hilal- kila mbili zenye uhasama mkubwa wa soka. Tukio hilo lilishuhudiwa na mamilioni kote duniani .

Ghasia uwanjani nchini Misri.Picha: dapd

Tukio hilo pia limekumbusha baadhi ya majanga yaliotokea miaka ya nyuma katika mchezo huu unaopendwa na wengi duniani. Katika janga kubwa kabisa la mchezo wa soka kuwahi kushuhudiwa, watu 340 walikufa mjini Moscow, Oktoba 20, 1982 na kwa muda wa miaka saba vyombo vya habari nchini Urusi vikawa vikikumbusha juu ya janga hilo lililotokaea katika pambano la Kombe la Shirikisho la vyama vya Kandanda barani Ulaya (UEFA) kati ya Spartak Moscow ya Urusi na Harlem ya Uholanzi katika uwanja wa Luizhniki. Balaa hilo lilitokea palipozuka hali ya kuakanyagana pale mashabiki walipokuwa wakijaribu kurudi uwanjani wakati Spartak ilipofunga bao katika dakika ya mwisho

Katika hali kama hiyo kwenye pambano la soka kati ya mahasimu wawili nchini Scotland Celtic na Rangers watu 66 walikufa Januari 2, 1971.

Kabla ya janga baya la Moscow, lililokuwa baya zaidi hadi wakati huo lilikuwa lile la mjini Lima Peru 1964 ambapo mashabiki 318 wa soka walikufa na mamia kujeruhiwa wakati bao la kusawazisha katika dakika za nyongeza lilipoakataliwa katika pambano kati ya Peru na Argentina kuwania kushiriki katika michezo ya Olimpiki.

Kwa upande wa ghasia zilizotokea Misri, hizo si za kwanza nchini humo. Itakumbukwa mashabiki 49 walikufa walipokuwa wakijaribu kuingia uwanjani katika pambano la Zamalek na Dulkla Prague ya Chekoslovakia ya zamani.

Pia si janga la kwanza barani Afrika. Watu 43 walikufa nchini Afrika kusini 1991 katika mechi baina ya Kaizer Chiefs na Orlando Pirates , Balaa baya zaidi barani humo ni lile la May 2001 pale watu kiasi ya 120 walipokufa katika tukio la kukanyagana uwanjani kwenye mji mkuu wa ghana - Accra.

Maandamano ya Wamisri dhidi ya vifo vya uwanjani.Picha: REUTERS

Wachambuzi wanasema bado kuna haja ya vyama vya soka barani Afrika kwa kushirikiana na vyombo vya dola vinavyosimamia ulinzi kuchukua hatua za ziada kulinda usalama viwanjani. Mashinadano yanayoendelea ya Kombe la Kandanda la Mataifa ya Afrika huko Guinea ya Ikweta na Gabon yamedhihirisha juu ya umuhimu huo.

Siku ya ufunguzi ilishuhudia hali mbvaya pale ulipozuka mtafaruku awakati mashabiki walipojaribu kuingia uwanjani. Chanzo kilikuwa ni kufunguliwa mlango mmoja tu uwanjani kwa mashabiki wote hali iliozusha purukushani. Hadi wiki ijayo mashabiki walikuwa wakilalamika kwamba polisi wameshindwa kuidhibiti hali hiyo.

hali hiyo hasa ni mjini Bata , Guinea ya Ikweta nchi ambayo inashirikiana na Gabon kama waandalizi wa mashindano hayo. Mashabiki wanasema baadhi ya mashabiki wamekuwa wakishikana koo na walinzi.

Wakati wa pambano moja wapo shabiki mmoja alijikuata akikumbwa na msongamano huo na akalalamika. "Kuna milango mitatu uwanjani lakini wanafungua mlango mmoja tu wakati ambapo kuna maelfu ya watu wanmaotaka kuingia, badala yake wanawapiga watu, ni mbaya sana."

Serikali ya Guinea ya Ikweta iliomba msaada wa polisi 150 kutoka Angola lakini tatizo ni lugha. waangola wanazungumza Kireno na lugha ya taifa Guinea ya Ikweta ni Kihispania. Hata hivyo hali iliboreka wakati wa michuano ya robo fainali mwishoni mwa juma .

Ligi ya kuu ya Ujerumani - Bundesliga

Mabingwa watetezi Dortmund imechukua uongozi kutoka kwa Bayern Munich baada ya kuitandika Nürenberg 2-0. Bayern imeteremka nafasi ya pili kutokana na mechi yake dhidi ya Hamburg kumalizika sare 1-1.

Wachezaji wa Kaiserslautern Köln ya Bundesliga.Picha: dapd

Nafasi ya tatu ni Schalke iliotoka sare na Mainz pia 1-1. Schalke na Bayern zina pointi sawa 41 kila moja, pointi mbili nyuma ya Dortmund huku Bayern ikiwa na wingi wa magoli. Borussia Monchengladbach iliorudi nyumbani bila kufungana na Wolfsburg iko nafasi ya nne ikiwa na pointi 41.

Katika mechi nyengine Bayer Leverkusen ilitoka sare 2-2 na Stuttgart, sawa na matokeo ya pambano kati ya Hoffenheim na Augsburg. Ama na pia Freiburg dhidi ya Werder Bremen Köln ikaitandika Kaisrslautern bao 1-0

Timu zinazokabiliwa na hatari ya kushuka daraja ni Kaisrslautern, Augsburg na Freiburg inayokamata mkia katika nafasi ya 18.

Ligi kuu ya England

Nchini Uingereza, katika pambano la aina yake la ligi kuu ya England- Premier League,Manchester United ilifanya kazi ya ziada na kuilazimisha Chelsea sareya mabao 3-3 baada ya United kuwa nyuma kwa mabao matatu kwa bila.

Ligi Kuu ya Uingereza, Permier League.Picha: dapd

Bila shaka lilikuwa ni pigo kwa Chelsea pamoja na kwamba imegawana pointi na mahasimu wao. Leo Tottenaham Hotspurs itatoana jasho na Liverpool wanaofahamika kwa mashabiki Afrika mashariki kama Bwawa la maini.

Manchester City ndiyo inayoongoza ligi hiyo kwa pointi 57, pointi mbili zaidi ya Manchester United. Tottenham iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi 49 ikifuatiwa na Chelsea kwa pointi 43 katika nafasi ya nne.

Wakati huo huo kuna fununu kuwa Kocha maarufu wa kilabu yaArsenal ya mjini London Aresen Wenger huenda akachukua nafasiya Laurent Blanc kuwa kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa baada ya mashindano ya kombe la Ulaya 2012 .

Ubondia:

Katika ubondia, Julio Cesar Chavez Jr amelitetea taji lake la uzani wa kati middleweight akimshinda mpinzani wake dhidi ya Marco Antonio Robio kwa pointi baada ya kumalizika raundi zote huko Texas nchini Marekani, mahala ambako baba yake Chavez alipigana na Pernell Whitaker 1993 -pambano lililomalizika sare. Chavez , baba anayefahamika kwa jina la Julio Ceasar Sr, sio tu ni bingwa zamani wa dunia mara sita, lakini anazingatiwa kuwa bondia bora kabisa kuwahi kuonekana kutoka Mexico.

Mabondia katika Michezo ya Jumuiya ya Madola.Picha: AP

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri: Saumu Mwasimba

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW