1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KOMBE LA UEFA NA TIMU 4 ZA UJERUMANI

5 Machi 2008

Klabu 4 za Ujerumani zinarudi uwanjani leo kuania Kombe la ulaya la UEFA 2 -Leverkusen na Bremen zikijua moja lazima iage mashindano.

Leverkusen ilipolazwa na Bochum 2:0Picha: AP

Baada ya firimbi ya mwisho kulia leo katika kombe la Ulaya la UEFA, timu 4 za Ujerumani-viongozi wa ligi-Bayern Munich,Bayer Leverkusen,Hamburg na Werder Bremen ,pengine hazitaingia zote duru ijayo ya robo-finali ya timu 8 za mwisho.Kwani mbili kati ya timu hizo 4 zinakutana leo wenyewe kwa wenyewe-nazo ni bayer Leverkusen na hamburg na mojawapo itaaga mashindano hii leo.Katika changamoto yao ya bundesliga kiasi cha mwezi mmoja uliopita,Hamburg na Leverkusen zilitoka suluhu bao 1-1.

Bayern munich-viongozi wa Bundesliga-Ligi ya Ujerumani wana miadi leo na Anderlecht nchini Ubelgiji wakati Werder Bremen wamewasili Glasgow,Scotland kwa changamoto na Glasgow rangers.

Mbali na timu 4 za Ujerumani, Uingereza pia ambayo klabu zake 2 zimetamba wiki hii katika champions League baada ya Arsenal kuwavua taji mabingwa AC Milan ya Itali na Manchester united kuipiga kumbo Lyon ya Ufaransa, ina nafasi nzuri ya mojawapo ya timu zake kutoroka na kombe hili la UEFA.Everton ina miadi na Fiorentina ya Itali wakati Tottenham Hotspurs inakumbana na PSV Eindhoven katika zahama nyengine ya mabingwa wawili wa zamani.Timu ya 3 ya uingereza Bolton Wanderers ,inachuana na sporting Lisbon ya Ureno.

Timu nyengine ya Ureno-Benfica Lisbon,inaikaribisha leo nyumbani Getafe ya Spian na kalenda ya mapambano ya jioni ya leo ya kombe hili la Ulaya la UEFA inakamilishwa na mkutano baina ya Olympic Marseille ya Ufaransa na St.Petersburg ya Russia.Duru ya pili ya timu hizi 16 itachezwa wiki ijayo.

Hamburg ilitamba mbele ya Bayer Leverkusen katika kile kinyan’ganyiro cha kufa-kupona cha kuania nafasi ya 3 katika ngazi ya Bundesliga jumapili iliopita ilipoikomea Eintracht Frankfurt mabao 4-1 wakati Leverkusen iliteleza kwa mabao 2-0 huko Bochum.Hatahivyo, kocha wa Hamburg Huub Stevens hadanganyiki,kwani anajua kuwa mla,mla leo,mla jana kala nini .

Mshambulizi wa Leverkusen na stadi wa zamani wa hamburg anajiwinda kabisa kwa changamoto hii kuiadhibu klabu yake ya zamani.Nae nahodha wa Hamburg mholanzi Rafael van der Vaart asema nafasi za ushindi leo dhidi ya Leverkusen ni nusu-kwa nusu.

Bayern munich inafuata mkondo wake wa kuja mwishoe kutwaa vikombe 3 msimu huu.Kombe la ubingwa wa Bundesliga, kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani na kombe hili la Ulaya la UEFA.Munich imeshindwa mara 1 tu na Anderlecht katika mapambano yao 6.

Munich inatamba wakati huu baada ya kuwakongoa meno mahasimu wao wakubwa katika Bundesliga hapo jumamosi Schalke 04.Munich lakini inabidi leo kucheza bila ya jogoo lao la Brazil na beki mshahara Lucio alieumia,lakini mchawi wao wa kati ya uwanja mfaransa Franck Ribbery,amerudi kuonesha ukorofi wake langoni mwa adui kama alivyitia adabu Schalke majuzi.

“Werder Bremen ni miongoni mwa majina makubwa katika dimba la Ulaya na ili kutamba mbele yao itatupasa tucheze uzuri kabisa”-asema mlinzi wa Glasgow rangers Kirk Broadfoot.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW