1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombora latua sokoni na kuua 12 Somalia

Aboubakary Liongo13 Desemba 2007

Nchini Somalia watu 12 wameuawa baada ya kombora kuvurumishwa katika soko kuu mjini Mogadish.

Wanamgambo wa kiislam wakishambulia majeshi ya serikali mjini MogadishuPicha: AP

Shambulizi hilo likuja muda mfupi tu baada ya maafisa wa serikali ya mpito ya Somalia kutoka taarifa ya kwamba wanamgambo wa kiislam wenye msimamo mkali wamejikusanya upya tayari kwa mashambulizi makali.

Kabla ya shambulizi hilo, Mkurugenzi katika wizara ya usalama wa taifa, Sheikh Qasim Ibrahim Nur alisema ya kwamba serikali ya mpito ya Somalia haina uwezo wa kupambana na wanamgambo hao wa kiislam pamoja na kuidhibiti nchi yote.

Amesema kuwa asilimia 80 ya eneo lote nchini Somalia si salama na haliko chini ya udhibiti wa serikali.

Kombora hilo lililipuka katika soko la Bakara , ambalo ndiyo soko kuu kwa mahitaji ya wakaazi wa Mogadishu.

Mbali ya vifo hivyo vya watu 12 wengine zaidi ya 40 walijeruhiwa na kwa mujibu wa mashuhuda idadi ya waliyokufa inaweza kuongezeka.

Osman Abdulahi ambaye dereva wa teksi anasema kuwa alishuhudia miili ya watu ikitapakaa chini na wengine wakitokwa na damu baada ya shambulizi hilo.

Dr Hassan Osman Isse wa Hospitali kuu ya Medina amesema kuwa idadi ya majeruhui ni kubwa na wengine 19 wako katika hali mbaya.

Taarifa nyingine zinasema ya kwamba mapema leo hii wanamgambo hao wa kiislam wamefanya mashambulizi kadhaa katika maeneo ya jirani ya kusini na kaskazini mwa Mogadishu, lakini hakuna taarifa za maafa.

Wanamgambo wa kiislam wanapambana na serikali ya mpito kutaka kushika tena hatamu baada ya kufurushwa mjini Mogadishu na majeshi ya Ethiopia yanayoisadia serikali hiyo mwaka jana .

Serikali ya mpito ya Somalia iko madarakani, likiwa ni jaribio la 14 la kutaka kurejesha utawala wa sheria toka kupinduliwa kwa Siade Barre mwaka 1991.Toka wakati huo Somalia imejikuta katika umwajikaji damu mkubwa.

Makundi ya haki za binaadamu nchini Somalia yanasema kuwa mwaka huu peke yake zaidi ya watu elfu 6 wameuawa na wengine zaidi ya laki saba wameyakimbia makazi yao kutoka na mapigano hayo.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa mzozo wa kibinadaamu nchini Somalia ni mkubwa kabisa barani afrika na kwamba zinahitajika kiasi cha dola millioni mia 4 kwa ajili ya kuwasaidia wahanga.

Wakati huo huo maharamia wawili wa kisomali wanaotuhumiwa kuteka meli ya Japan wamekatwa huko kaskazini mashariki mwa Somalia.

Meli hiyo iliyokuwa imebeba kemikali ilitekwa nyara na maharamia hao kwenye pwani ya Somalia wiki sita zilizopita ikiwa na mabaharia 22 na kuachiwa huru jana.

Pwani ya Somalia ni eneo la hatari kabisa la maji duniani kwa utekaji nyara meli.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW