1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVisiwa vya Comoros

Komoro yataka rais wa zamani ahukumiwe kifungo cha maisha

24 Novemba 2022

Waendesha mashtaka nchini Comoro wametaka aliyekuwa rais wa nchi hiyo Ahmed Abdallah Sambi ahukumiwe kifungo cha maisha jela katika kesi ambayo inasikilizwa bila ya Sambi kuweko mahakamani.

Hammer Gerichtssaal Gericht Richter-Hammer
Picha: Adrian Wyld/empics/picture alliance

Rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 64 na ambaye anashtakiwa kwa uhaini ni mpinzani mkubwa wa rais wa sasa Azali Assoumani. Anakabiliwa na mashataka yanayohusiana na tuhuma za uuzaji wa hati za usafiri za Comoro kwa watu wasiokuwa na nchi wanaoishi kwenye mataifa ya kiarabu ya Ghuba.

Mwendesha Mashtaka wa serikali Ali Mohamed Djounaid ameiambia mahakama maalum  inayohusika na masuala ya usalama wa nchi kwamba Sambi ameyahujumu mamlaka aliyopewa na Wakomoro na kwahivyo anapaswa kufungwa kifungo cha maisha jela.

Hukumu inatarajiwa kutangazwa Novemba 29.

Itakumbukwa kwamba rais huyo wa zamani Ali Abdallah Sambi aliyeingoza nchi hiyo ndogo ya visiwa kati ya mwaka 2006 na 2011 alipitisha sheria mnamo mwaka 2008 ya kuruhusu kuuzwa kwa hati za kusafiri yaani Paspoti  za Comoro kwa ada ya kiwango kikubwa cha fedha.

Soma pia: Mahakama yathibitisha ushindi wa Azali Assoumani

Rais wa zamani wa Comoro Ahmed Abdallah Mohamed Sambi Picha: picture-alliance/ dpa

Mwanasheria mmoja wa Togo Eric Emannuel Sossa ambaye ni miongoni mwa waendesha mashtaka  anasema utawala wa Sambi ulitowa haki ya kuuza uraia wa Comoro kwa majambazi  kwa namna ambayo ni sawasawa na mtu kuuza karanga.

Kiongozi huyo wa zamani wa Comoro kwahivyo anatuhumiwa alijilimbikia mamilioni ya dola chini ya mpango huo. Hata hivyo wakili wake raia wa Ufaransa Jean-Gilles Halimi amesema hakuna ushahidi wa kuwepo fedha hizo kwasababu hakuna akaunti yoyote iliyopatikana.

Bwana Sambi amekataa katakata kuhudhuria vikao vya kesi inayomkabili wakati ambapo wakili wake akisema hakuna hakikisho kwamba kesi hiyo itaendeshwa kwa usawa na haki.

Alijitokeza mahakamani mnamo siku ya Jumatatu tu akiwa pamoja na mawakili wake waliomtaka jaji ajiondowe kwasababu huko awali alishiriki kwenye jopo lililopitisha uamuzi wa  kumshtaki Sambi.

Tayari rais huyo wa zamani ameshatumikia kifungo cha miaka 4 jela na alikuwa katika kifungo cha nyumbani  kwa tuhuma za kuvunja sheria. Miezi mitatu baadae aliswekwa kizuizini kusubiri kesi inayohusu kujilimbikizia mali,rushwa na udanganyifu katika kile kinachoitwa kashfa ya kuuza uraia kwa maslahi ya kiuchumi.''

Soma pia:Ishara za kuivamia Anjouan huko Comoro zaanza 

Akashtakiwa kwa uhaini. Miongoni mwa wanaoshatakiwa kwenye kesi hiyo ni mfanyabiashara Mfaransa mwenye asili ya Kisyria Bashar Kiwan ambaye anaituhumu serikali kwamba inataka kumshinikiza kutoa ushahidi dhidi ya rais huyo wa zamani na badala yake apewe msamaha.

Hata hivyo ofisi ya rais Azali Assoumani imekanusha tuhuma hiyo lakini upande wa utetezi umeliambia shirika la habari la AFP kwamba unadhamiria kufungua malalamiko kuhusu kuingiliwa kwa mashahidi.

Nchi hiyo ya visiwa inajumuisha visiwa vitatu Anjouan,Ngazija na Moheli  na inakabiliwa na miaka chungunzima ya hali ya umasikini na mikwamo ya kisiawa ikiwemo kushuhudia mapinduzi kiasi 20 au majaribio ya mapinduzi tangu ilipojipatia uhuru wake mwaka 1975 kutoka Ufaransa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW