1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kompany asema rekodi ya mabao si muhimu

9 Februari 2026

Ushindi wa 5-1 wa Bayern Munich dhidi ya TSG Hoffenheim Jumapili uliwapelekea kufikia mabao 79 kutokana na mechi 21 za ligi.

Wachezaji wa Bayern wakimpongeza Luis Diaz baada ya kufunga bao
Wachezaji wa Bayern wakimpongeza Luis Diaz baada ya kufunga baoPicha: Bernd Feil/MIS/IMAGO

Ila kocha Vincent Kompany anasema kuivunja rekodi ya mabao 101waliyoiweka Bayern katika misimu ya awali, si suala lililo akilini mwake.

"Kwa sasa hilo si muhimu kwangu," Kompany aliwaambia waandishi baada ya kufikisha mwisho msururu wa mechi mbili bila ushindi. Ushindi huo dhidi ya Hoffenheim uliwapelekea Bayern kuwa pointi sita mbele ya Dortmund iliyo kwenye nafasi ya pili.

Luiz Diaz alifunga hat-trick yake ya kwanza kama mchezajiwa Bayern katika mechi hiyo lakini Hoffenheim watalaumu kipigo hicho kikubwa kutokana na kadi nyekundu aliyooneshwa mchezaji wao Kevin Akpoguma na kuwapelekea wasalie wachezaji kumi uwanjani.

Diaz ambaye ni raia wa Colombia, ndiye aliyesababisha mikwaju miwili ya penalti ya Bayern iliyofungwa na Harry Kane na kumpelekea Muingereza huyo kufikia mabao 24 ya Bundesliga huku Diaz akiwa kwenye nafasi ya pili na mabao 13.

Rekodi ya ufungaji mabao ya Bundesliga ya mabao 101 katika msimu mmoja iliwekwa na Bayern katika msimu wa mwaka 1971-72  na Bayern ya sasa katika msimu wa mwaka 2019-2020, ilikosa kuifikia rekodi hiyo kwa bao moja tu, kwani walifunga mabao 100 huo msimu.

Haya yakiarifiwa, huenda Bayern Munich wakaamua kuiahirisha mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho na RB Leipzig kwasababu ya mgomo wa usafiri wa umma mjini Munich.

Uamuzi kuhusiana na suala hilo unatarajiwa kutolewa Jumatatu, huku afisa mkuu mtendaji Jan-Christian Dreesen akiwaambia waandishi wa habari wakiona mechi bado inaweza kuchezwa basi wataiandaa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW