Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari laanza Bonn
27 Mei 2019Akiwakaribisha washiriki wa kongamano hili linalovikusanya vyombo vya habari, waandishi, mashirika ya habari na wawakilishi wa taasisi za kimataifa, Mkurugenzi Mkuu wa Deutsche Welle, Peter Limbourg, aliwaambia wageni hao kwamba ukweli ni kuwa kazi ya uandishi wa habari inazidi kuwa ngumu kila uchao.
"Sote tunajuwa hali ya uhuru wa habari na ufanyaji kazi kwenye vyombo vya habari inazidi kuwa ngumu kwa wengi wenu kote ulimwenguni," alisema Limbourg.
Kongamano hilo lilihutubiwa moja kwa moja na Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, ambaye aliungana na washiriki kwa njia ya video akiwa Berlin. Rais huyo wa shirikisho alizungumzia matokeo ya uchaguzi wa Bunge la Ulaya ambao ulivipandisha vyama vya siasa kali na kuanguka kwa vyama vya kihafidhina na vikongwe.
"Chaguzi hubadilika na wapigakura hubadilika. Matokeo ya mara hii pamoja na changamoto zake yanaonesha kuwa demokrasia inaimarika barani Ulaya, zaidi ya asilimia 60 walijitokeza kupiga kura zao. Huenda kampeni ilikuwa kubwa kwa wagombea, huenda pia kuna mambo ya kujifunza."
Maudhui kuu ya mwaka huu ni kuhamisha nguvu, ikiakisi namna ambavyo nguvu za kisiasa, kiuchumi na kijeshi zinavyohama hivi sasa duniani na katika kuhamishwa huko, taasisi za habari nazo zikijikuta mashakani.
Kwenye siasa, wanasiasa wa siasa kali za mirengo ya kushoto na wale wanaoelemea kwenye hamasa ya umma wanazidi kuja juu, huku wanasiasa wenye mitazamo ya mshikamano wa kijamii na kiliberali wakitegwa kando, ambapo kwenye uchumi, mataifa yaliyokuwa yakifahamika kuwa na nguvu pekee duniani yanaanza kuzidiwa nguvu na yale yanayoinukia, na kwenye tawala, serikali za kidikteta zikizidi kuongezeka.
Stephen Ouma Bwire kutoka Uganda alishiriki kongamano hili na kwake hii ni nafasi ya kujifunza namna mabadiliko haya yanavyoathiri kazi yake ya uandishi habari.
Jumla ya mada 30 zinajadiliwa kwenye kongamano la mwaka huu kuanzia zile zinazohusu moja kwa moja kazi za uandishi wa habari hadi zile za mahusiano ya kimataifa, chaguzi, teknolojia na uchumi. Zote chini ya mwangaza wa namna nguvu inavyohamishwa kutoka upande mmoja kwenda mwengine.