1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano la kiuchumi mjini Davos

Oumilkher Hamidou2 Februari 2009

Viongozi wakuu wa kiuchumi na kiisiasa wamekutana ,matokeo yake ni nini?

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akihutubia katika kongamano la DavosPicha: AP


Baada ya siku tano za majadiliano kongamano la kiuchumi ulimwenguni limemalizika bila ya kufikiwa makubaliano juu ya namna ya kuupatia ufumbuzi mzozo wa kiuchumi.Lakini ndo kusema kongamano hilo halikufanikiwa?

Yoyote yule aliyetegemea kuona hatua madhubuti za kuufumbua mzozo wa kiuchumi ulimwenguni zinapitishwa pamoja pia na kubuniwa ratiba ya kutiwa njiani hatua hizo,basi hatakosa kusema mkutano huo mkubwa kabisa wa Davos umekwenda kombo.Kwasababu hata baada ya mkutano huo wa kilele kumalizika,bado watu wanajikuta pala pale kama walivyokua kabla ya mkutano huo kuitishwa katika mji huo wa milimani wa Uswisi;haijulikani vipi ulimwengu utaweza kujikwamua toka mzozo huu wa kiuchumi.


Ni sawa kabisa,mapendekezo hayajakosekana:Kansela Angela Merkel ametetea umuhimu wa kubuniwa baraza la kiuchumi la kimataifa,litakalogeuka kua taasisi ya kiuchumi,kama lilivyo baraza la usalama la umoja wa mataifa mataifa.


Wanauchumi waliojipatia umashuhuri kutokana na makadirio yao ya kutisha,yaliyojitokeza kuwa sawa,Nouriel Roubini na Nassim Taleb wanashauri benki zitaifishwe.Nae waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown,sawa na washiriki wengineo mkutanoni,anashauri ziimarishwe taasisi mbili za fedha za kimataifa yaani benki kuu ya dunia na shirika la fedha la kimataifa-IMF.


Lakini hakuna yeyote aliyeshauri mikakati yote hiyo itatiwa njiani vipi au itadumu muda gani.Kuna sababu ya hali hiyo nayo ni kwamba mengi kati ya mapendekezo hayo yanapingana,kana si kwa sehemu basi yanapingana moja kwa moja.Kwa namna hiyo njia zozote za kutaka kuupatia ufumbuzi mzozo wa kiuchumi zinajitokeza kua batil;maridhiano jumla hayawezi kupatikana.


Hata hivyo mtu anaweza na anabidi pia kutamka kwamba kongamano hilo la kimataifa la kiuchumi haikua kazi bure;mtu anaweza hata kusema,limefanikiwa.Yeyote yule aliyeshuhudia jinsi mameneja na wanasiasa walivyokua wakijadiliana na kubishana,yeyote yule aliyejionea kwa macho yake jinsi viongozi wakuu wa kiuchumi na mawaziri walivyokua wakijaribu kuelezana jinsi mzozo wa kiuchumi unavyoendelea,yeyote yule aliyetambua jinsi viongozi waliohudhuria kongamano hilo walivyoingiwa na hofu na kutaka kujua nini cha kufanya,basi mtu kama huyo hatakosa kugundua pia kwamba "wakati tuu haukua bado muwafak".


Badala ya kupitisha mkakati madhuhubuti kwa siku za mbele,viongozi mjini Davos wamejishughulisha zaidi na kutathmini,kupima na kujaribu kupeana moyo.Kwa mara ya kwanza tangu mzozo ulipozuka wanauchumi na wanasiasa wamekutana katika eneo hilo la milimani la Uswisi kubadilishana maoni-kwa hivyo mtu anaweza kusema kongamano la kiuchumi limegeuka uwanja wa kupima hali ya mambo namna ilivyo.


Kwa mtazamo wa watu wanaosumbuliwa na shida za kiuchumi kote ulimwenguni,matokeo hayo hayatoshi.Lakini bila ya kujua kwa kina hali ikoje,hakuna tiba inayoweza kusaidia.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW