1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano la ulinzi wa mazingira COP16 laanza Colombia

22 Oktoba 2024

Kongamano kubwa zaidi la ulinzi wa mazingira duniani COP16, limeanza mjini Cali nchini Colombia kwa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka na ufadhili ili kurekebisha uharibifu mkubwa wa bioanuwai .

Rais wa Colombia Gustavo Petro ahutubia wakati wa ufunguzi wa kongamano la COP16 mjini Cali nchini Colombia mnamo Oktoba 20, 2024
Kongamano la COP16 mjini Cali nchini ColombiaPicha: Fernando Vergara/AP/dpa/picture alliance

Takriban wajumbe 23,000, ikiwa ni pamoja na mawaziri 100 wa serikali na wakuu wa nchi kadhaa, waliidhinishwa kuhudhuria kongamano hilo kubwa zaidi la bioanuwai litakaloendelea hadi Novemba 1.

COP16 inajukumu la kutafuta njia za kufanikisha mafikiano ya COP15

Likiwa na kaulimbiu ya "Amani na mazingira," kongamano hilo lina jukumu la dharura la kutafuta mbinu za ufuatiliaji na ufadhili ili kuhakikisha malengo 23 ya Umoja wa Mataifa yaliyokubaliwa katika kongamano la COP15miaka miwili iliyopita yanafikiwa ifikapo mwaka 2030 ili kusitisha na kurekebisha kupotea kwa mazingira asili.

Kongamano lafunguliwa chini ya ulinzi mkali

Kongamano hilo lilifunguliwa chini ya ulinzi wa polisi na wanajeshi zaidi ya 10,000 wa Colombia baada ya kundi la wapiganaji wa EMC walio katika vita na serikali kuwaambia wajumbe wa kigeni kutohudhuria na kuonya kutofanyika kwa mkutano huo.

Wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, waakilishi wa Umoja wa Mataifa pamoja na wa mataifa waliwahimiza washiriki wa kongamano hilo kutoka takriban nchi 200 kuchukuwa hatua za haraka kuchangisha mabilioni ya dola kukomesha uharibifu wa mazingira asili .

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: William Volcov/ZUMA Press Wire/picture alliance

Huku takriban viumbe milioni moja vinavyojulikana kote duniani vikikadiriwa kukabiliwa na hatari ya  kuangamizwa, waziri wa mazingira wa Colombia ambaye pia ni rais wa COP16 Susana Muhamad aliwaonya wajumbe hao kwamba sayari ya dunia haina muda wa kupoteza.

Yalioafikiwa katika kongamano la COP15

Miaka miwili iliyopita, nchi zilipitisha mkataba wa kihistoria wa Mfumo wa Dunia waBioanuwaiwa Kunming-Montreal na orodha ya malengo 23 ya kusaidia kukomesha kupotea kwa mazingira asili kufikia mwaka 2030. COP16 imepewa jukumu la kutafakari jinsi ya kutekeleza makubaliano hayo, yaliojumuisha kutafuta dola bilioni 200 kwa mwaka za uhifadhi.

Ulimwengu umepoteza mwelekeo kutimiza malengo ya 2030.

Siku ya Jumapili usiku, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, aliwatahadharisha wajumbe hao wa COP16 katika ujumbe kupitia video kwamba ulimwengu umepoteza mwelekeo katika kutimiza malengo ya 2030. Alisema wajumbe lazima waondoke kwenye mkutano huo na uwekezaji mkubwa mpya .

Mjumbe mkuu wa Brazil Andre Correa do Lago, aliliambia kongamano hilo kwamba ukosefu wa ufadhili kwa mfuko ulioko, kunaibua wasiwasi kwamba hautaweza kufikia malengo ya mfumo huo uliopitishwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW