1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano la Usalama lafanyika Addis Ababa

14 Aprili 2016

Kongamano kuhusu usalama lililopewa jina Tana, linafanyika Addis Ababa Ethiopia. Litajadili masuala muhimu yanayoathiri mahusinao kati ya Afrika na mataifa mengine ya dunia kuhusiana na ajenda ya usalama wa dunia.

Al-Shabaab Kämpfer in Mogadishu
Njia za kupambana na wanamgambo wa kundi la al Shabaab zitajadiliwaPicha: picture-alliance/AP Photo/AP Photo/F. Abdi Warsameh

Kauli mbiu ya kongamano la Tana mwaka huu ni Afrika katika ajenda ya kimataifa ya usalama, lengo likiwa ni kutafuta sababu kwa nini changamoto za kiusalama barani Afrika zinavutia hisia kubwa katika ngazi ya kimataifa, ilhali uzoefu wa bara lenyewe na jinsi linavyoendesha masuala ya usalama bado havijatambuliwa sana kimataifa.

Ni dhahiri leo, kuliko wakati mwingine wowote ule, kwamba Afrika inahitaji kuungana na kuzungumza kwa kauli moja kama inataka kuwa na ushawishi na kuyalinda masilahi yake katika mijadala ya kimataifa kuhusu usalama. Kwa mara nyingine tena Kongamano la Tana litawapa fursa viongozi wa serikali na mataifa ya Afrika, maafisa wa vyeo vya juu wa serikali pamoja na watu mashuhuri, wasomi, viongozi wa sekta binafsi na wadau wengine, kulijadili kwa kina jukumu la bara la Afrika katika masuala ya usalama wa kimataifa.

Kauli mbiu hiyo ni muafaka, hususan wakati huu ambapo Afrika inaathiriwa na mitihani ya kiusalama. Bara hilo halikabiliwi tu na matatizo makubwa ya kiusalama, bali pia iko mstari wa mbele katika kutafuta njia za kukabiliana na matatizo ya kiusalama, ambayo yamesababisha hali ya wasiwasi ulimwenguni kote - kuanzia mizozo kuhusu raslimali hadi uhamiaji, mizozo ya ndani na changamoto za kusaidia operesheni za pamoja za kulinda amani.

Afrika yatakiwa kuwa na sauti moja

Masuala ya usalama hujadiliwa katika mikutano rasmi ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, mashauriano kati ya viongozi wa mataifa makubwa na makongamano maalumu ya kimataifa kuhusu kwa mfano mabadiliko ya hali ya hewa, mzozo wa kiuchumi, mazingira, mzozo wa chakula, nishati, usambazaji wa silaha za nyuklia na silaha za kibayolojia. Katika baadhi ya mikutano hii Afrika huonekana kama eneo la kitisho kwa usalama wa kimataifa, umasikini, rushwa, ugonjwa wa ukimwi na virusi vinavyosababisah ugonjwa huo vya HIV, uhamiaji na matatizo mengine.

Wajumbe waliohudhuria kongamano la Tana (20.03.2015)Picha: DW/T. Getachew

Sauti ya Afrika haijawahi kuwa sehemu ya mazungumzo ya aina hiyo kwa sababu kadhaa, zikiwemo za kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kiteknolojia, ambazo zinavuruga uwezo ya bara hilo katika ngazi ya kimataifa. Ndio maana kuna haja ya Afrika kuandaa mkakati wa pamoja kuelekea ajenda za kigeni kuhusiana na usalama wake.

Kongamano la Tana 2016 mjini Addis Ababa linafanyika wakati bara la Afrika likiwa limejumuishwa katika mfumo wa usalama wa dunia. Mada muhimu kwa wadau wa Afrika na wa kimataifa ni ugaidi, itikadi kali za kisiasa na kidini, uharamia, ulanguzi wa dawa za kulevya na biashara haramu ya usafirishaji wa binaadamu na pia uthabiti wa mataifa ya Afrika, utawala bora na usimamizi mzuri wa masuala ya usalama.

Mwandishi: Josephat Charo/www.tanaforum.org

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi