Kongamano la vyombo vya habari kuangazia usumbufu na ubunifu
14 Juni 2021Kongamano hilo linaloandaliwa kwa njia ya video, linawaleta pamoja wataalamu wa masuala ya habari na wadau mbali mbali kote duniani. Tofauti na mwaka uliopita, kongamano hilo la 14 lililoanza leo na kutarajiwa kukamilika hapo kesho, litaangazia kwa undani jinsi uandishi wa habari unavyoendelea katika enzi hii ya upotoshaji wa habari na iwapo kunaweza kupatikana njia ya kurekebisha hali ilivyo na kuangazia ukweli na usahihi.
Warsha hiyo ilifunguliwa na hotuba kutoka kwa wakuu mbali mbali wanaomjumuisha Merkel, mgombea wa ukansela wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, Armin Laschet pamoja na mgombea ukansela wa chama cha kijani Annalena Baerbock.
Hotuba ya mkurugenzi mkuu wa DW
Katika hotuba ya ufunguzi, mkurugenzi mkuu wa shirika la DW Peter Limbourg aliwakaribisha washiriki wote na kusema kuwa kongamano hilo ni la kimataifa huku kukiwa na washirika kutoka mataifa 120 kote duniani. Aliongeza kuwa kwa sababu muhimu, usumbufu na ubunifu ni suala ambalo linahusisha kila mmoja duniani. Limbourg amesema kuwa kwa sasa kuna mabadiliko katika tasnia ya uandishi wa habari kutokana na teknolojia ya kidigitali na mitandao ya kijamii. Ameongeza kuwa, yanayopaswa kuulizwa ni kwa njia gani watu wanataka kushughulikia mabadiliko hayo, uwezekano wa kiufundi na kwa malengo gani.
Wakati huo huo Merkel amesema kuwa katika jamii zinazozingatia demokrasia ambazo ziko wazi kwa maendeleo, swala linalopaswa kuzingatiwa ni kwamba uhuru una maana gani haswa? Merkel ameongeza kuwa hii inajumuisha jinsi uhuru unavyolindwa na haki za kimsingi.
Kulingana na Merkel, katika sekta ya kidijitali pamoja na isiyokuwa ya kidijitali, kuna kipimo katika uhuru wa kujieleza kama aina nyingine ya uhuru iwapo haki za kimsingi na uhuru wa wengine utakiukwa. Ameongeza kuwa kutafuta usawa kati ya kulinda haki binafsi kwa upande mmoja na uhuru wa kusambazwa kwa data kwa uvumbuzi unaotegemea data sio rahisi. Merkel amesema kuwa mada hiyo ya mwaka huu ya usumbufu na ubunifu, inawahusisha watu wengi kote duniani kutokana na utata unaozunguka mazingira ya uanahabari kutokana na teknolojia za kidijitali na mitandao ya kijamii.
Noel Curran, mkurugenzi mkuu wa Umoja wa utangazaji barani Ulaya, amesema kuwa kongamano hilo la mwaka huu pia litaangazia kutafuta suluhisho la kuimarisha uandishi wa habari na kwamba mtindo mmoja angalau linapohusika bara Ulaya ni kuimarisha mashirika ya habari ya umma. Curran ameiambia DW kwamba wakati wa vikwazo vya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona, vyombo vya habari vya umma vilijiboresha na kutoa habari za kuaminika, elimu na burudani iliyohitajika kwa sana na kwamba takwimu zinaonesha kuwa idadi kubwa ya watu ilijitokeza kutazama vipindi vya mashirika hayo.