1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamno la kujadili Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini

Sylvia Mwehozi
6 Aprili 2019

Mfalme Abdullah wa Jordan ametoa wito wa uwekezaji zaidi wa kigeni katika Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini, akisema unahitajika ili kutengeneza "mustakabali wa baadae" wa ukanda huo uliokumbwa na migogoro.

Jordanien World Economic Forum on the Middle East and North Africa 2019
Picha: Reuters/M. Hamed

Akiwahutubia wanasiasa, wafanyabiashara na wawakilishi wa asasi za kiraia wapatao 1,000 katika ufunguzi wa Kongamano la Uchumi Duniani (WEF), kuhusu Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini nchini Jordan, Mfalme Abdullah amesema "kinachotokea katika ukanda wetu kinaathiri ulimwengu mzima".

"Hali yetu ya kiuchumi inatia moyo", alisema Abdullah, lakini akiongeza kuwa uchumi wa Jordan umekabiliwa na changamoto nyingi wakati taifa hilo "lilipofanya jambo sahihi kushughulikia wakimbizi". Jordan inawahudumia wakimbizi karibu milioni 1.3 kutoka Syria.

Ili kufufua uchumi wake, serikali ilichukua hatua kadhaa za kubana matumizi katika siku za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kupunguza ruzuku katika bidhaa za msingi kama vile mkate, ili kufufua uchumi na kupunguza pengo la upungufu wa bajeti.

Mfalme Abdullah wa Jordan na katibu mkuu Antonio Guterres Picha: Reuters/M. Hamed

"Mageuzi yako mbioni ili kuunga mkono na kuboresha mazingira ya biashara", alisema Mfalme huyo katika kongamano linalofanyika karibu na bahari iliyokufa yaani Dead Sea.

Kongamano hilo la siku mbili, linajadili ukosefu wa ajira, migogoro, maendeleo ya kiuchumi na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo hayo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov wote watahudhuria kongamano hilo.

Mkutano huo umefanyika wakati kunafanyika machafuko ya kijeshi nchini Libya, pamoja na vuguvugu la kudai demokrasia nchini Algeria lilomlazimisha Rais Abdelaziz Bouteflika kung'oka madarakani baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa miaka 20.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW