1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo, Guinea zatinga robo fainali ya AFCON

29 Januari 2024

Mohamed Salah hatapata fursa ya kurejea katika tamasha la Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya timu yake ya Misri kuondolewa katika mashindano hayo kupitia mikwaju ya penalti dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Fußball Afrika Cup 2024 I Ägypten vs Kongo
Picha: Sia Kambou/AFP/Getty Images

Mabingwa mara saba Misri walipoteza kwa penalti 8 kwa 7 dhidi ya Wakongo baada ya mechi yao ya hatua ya 16 za mwisho kumalizika kwa sare ya 1 – 1 baada ya muda wa nyongeza.

Soma pia: Magoli 2 ya Lookman dhidi ya Kamerun yaipeleka Nigeria robo fainali

Meshack Elia aliiweka Kongo kifua mbele katika mji wa San-Pedro katika dakika ya 37, kabla ya Mostafa Mohamed kuisawazishia Misri kwa njia ya penalti katika dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza.

Mechi ya Kongo na Misri ilichezwa mjini San PedroPicha: Sia Kambou/AFP/Getty Images

Misri walipambana kwa kucheza pungufu uwanjani baada ya Mohamed Hamdy kuonyeshwa kadi ya pili ya njano katika kipindi cha kwanza cha muda wa nyongeza.

Kipa wa Misri Mohamed Abou Gabal, maarufu kama Gabasaki, alipoteza penalti yake, kabla ya kipa wa Kongo Lionel Mpasi kusukuma yake wavuni na kuipeleka Kongo katika robo fainali.

Ni mara ya kwanza kwa Kongo kushinda mechi ya mtoano katika mashindano hayo tangu walipofika nusu fainali katika mwaka wa 2015.

"Tulifanya sana mazoezi ya kupiga penalti katika siku chache zilizopita na nilijua ningehitajika kuwa tayari,” alisema Mpasi, mchezaji wa zamani wa Paris Saint-Germain ambaye sasa anachezea Rodez klabu ya ligi ya daraja la pili nchini Ufaransa.

"Wakati nilipouweka mpira kwenye eneo la penalti, nilijaribu kuwa mtulivu. Niliwaza kuhusu penalti niliyoipiga mazoezini na bahati nzuri ikaingia kambani.”

Guinea yailiza Guinea ya Ikweta

Salah alitarajiwa kurejea AFCON baada ya kupona jerahaPicha: Kim Price/CSM via ZUMA Press Wire/picture alliance

Timu ya kocha Sebastien Desabre itaelekea Abidjan kwa mtanange wa robo fainali Ijumaa dhidi ya Guinea, ambayo iliichapa Guinea ya Ikweta 1 – 0 katika mechi ya mapema. Wakati mechi ilionekana kuwa inaingia muda wa nyongeza, Mohamed Bayo alifunga bao katika dakika ya nane ya muda wa majeruhi na kuivunja mioyo ya Guinea ya Ikweta.

Ulikuwa ushindi wa kihistoria kwa Guinea, ambao hawajahi kushinda mechi ya mtoano ya AFCON.

"Ushindi huu una maana kubwa. Tulijua kuwa hili lingekuwa tukio la kihistoria,” alisema kocha wa Guinea Kaba Diawara, ambaye alitokwa na machozi baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa.

Wakati huo huo, Guinea ya Ikweta, ambayo ilishuhudia mchezaji wake wa kiungo cha kati Federico Bikoro akitimuliwa uwanjani katika dakika ya 55, itajiuliza ni nini kingetokea kama nahodha wao Emilio Nsue asingepoteza mkwaju wa penalti katikati ya kipindi cha pili.

Hii leo, wenyeji Cote d'Ivoire watakabana koo na mabingwa watetezi Senegal mjini Yamoussoukrou, baada ya Cape Verde kukuana na Mauritania mjini Abidjan.

Afp, ap, reuters, dpa