Kongo kufanya Uchaguzi uliosubiriwa kwa muda mrefu
29 Desemba 2018Wahudumu waliopewa mafunzo ya kuendesha uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamo kwenye harakati za kukamilisha maandalizi ya uchaguzi uliosubiriwa kwa muda mrefu. Maandamano yaliyoitishwa na upinzani kabla ya uchaguzi hayakupata mwitikio mkubwa. Hofu imetanda kuelekea uchaguzi huo, baada ya tume inayosimamia uchaguzi CENI kutangaza kwamba baadhi ya majimbo yatafanya uchaguzi huo mwakani.
Hata hivyo uchaguzi utaendelea siku ya Jumapili Desemba 30 katika maeneo mengine ya nchi kama ulivyopangwa, na rais mpya anatarajiwa kutangazwa Januari 18. Kwenye jimbo la Goma, vijana walikabiliana na polisi. Katika mji wa Beni mtu mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi. Wakazi karibu milioni 1.2 katika maeneo ya Kivu ya Kaskazini, na Yumbi wataathirika kutokana na kuahirishwa kwa uchaguzi huo. Jumla ya wapiga kura milioni 40 wameandikishwa kupiga kura. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezihimiza pande zote kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unafanyika kwa utulivu.
Wagombea watatu ndiyo wanaoonekana kuongoza mstari wa mbele kati ya idadi jumla ya wagombea 21 wanaowania urais katika taifa hilo.
Emmanuel Ramazani Shadary, mwenye umri wa miaka 58, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wakati wa kipindi cha machafuko mwishoni mwa mwaka 2016, anatajwa kuwa ni kibaraka wa rais Joseph Kabila.
Shadary amewekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya kwa kuingilia kati mchakato wa uchaguzi alipokuwa waziri wa mambo ya ndani na pia kwa kuruhusu zoezi la kuwakamata watu walioandamana kupinga kucheleweshwa kwa uchaguzi. Shinikizo la kimataifa limeichukiza serikali ya Kongo, na hivyo waangalizi wa Umoja wa Ulaya na wengine wa nchi za Magharibi hawakualikwa kuleta waangalizi wao wakati wa kupiga kura siku ya Jumapili.
Felix Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 55, anatarajia kuwa atashinda uchaguzi huo na kuwa rais wa taifa hilo, jambo lililomshinda baba yake Etienne Tshisekedi, aliyekianzisha chama kikuu cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS), mnamo 1982. Felix Tshisekedi alichukua hatamu ya uongozi wa chama hicho baada ya baba yake kufariki dunia Februari 2017. Upinzani ulivurugika baada ya Felix Tshisekedi, mwana wa marehemu Etienne Tshisekedi alipoutelekeza muungano wa vyama vya upinzani na kuamua kusimama peke yake.
Martin Fayulu, mwenye umri wa miaka 62, ni mgombea watatu katika safu hiyo ya wagombea walio mstari wa mbele. Hakuwa mwanasiasa anayejulikana ila amepata umaarufu wiki chache kabla ya uchaguzi huo. Fayulu alianza kujulikana miaka miwili iliyopita kama mkosoaji mkubwa wa Kabila hasa pale alipolaumiwa kwa kung'ang'ania kubakia madarakani.
Magwiji wawili wa upinzani, makamu wa rais wa zamani Jean-Pierre Bemba na gavana wa zamani Moise Katumbi, wamenyimwa ruhusa ya kushiriki kwenye uchaguzi huo.
Mwandishi:Zainab Aziz/AFP/AP/APE
Mhariri: Jacob Safari