Kongo: Mapigano yaendelea kati ya waasi wa M23 na Maimai
9 Oktoba 2023Vyanzo mbalimbali vya ndani vimethibitisha kwamba mashambulizi hayo yalianza mapema asubuhi leo Jumatatu kutoka kwenye Milima ya Mulimbi na Kanaba inayouzunguka mji huo wa TONGO.
Katika eneo hilo waasi wa M23 walizishambulia kwa mabomu ngome za vijana hao wajiitao Wazalendo kabla ya wao kujibu mashambulizi kwa kuvurumisha makombora kuelekea ngome za M23.
Mwishoni mwa juma lililopita kushudiwa kwa mapigano makali baina ya pande zote mbili kurushiana risasikatika kijiji kidogo cha Kahunga, kilicho umbali wa kilomita tano kuelekea mji mkuu wa wilaya hiyo ya Rutshuru ambako pia kumetanda hali ya wasiwasi tangu jana hadi mchana huu.
Soma pia:Muda wa M23 kusalimisha silaha wakamilika bila matunda
Raia kwenye maeneo hayo, ambayo yako kwenye dhamana ya majeshi la Kenya na Sudan Kusini chini ya Kikosi Maalum cha Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanasema wanaishi kwa hofu.
Raia na wakaazi wanavishutumu vikosi hivyo vya Afrika Mashariki kumeshindwa hadi sasa kurejesha utulivu.
Utulivu na amani vyatoweka kwa wiki mbili
Raia katika mji wa kimkamkati wa Kitshanga, mji mwingine unaoshuhudia machafuko kwa wiki nzima sasa, wameshuhudia hii leo asubuhi msururu wa vijana wajiitao Wazalendo wakipiga risasi angani kama ishara ya ushindi wao dhidi ya M23.
Kundi la waasi wa M23 waliuacha mji huo baada ya mapigano yaliyodumu kwa masaa kadhaa siku ya Jumapili.
Katika tangazo lao mwanzoni mwa wiki iliyopita, jeshi la Kongo lilikanusha madai kwamba linaunga mkono mapigano hayo kati ya vijana hao Wazalendo na waasi wa M23 wanaopoteza sasa baadhi ya ngome zao wilayani Masisi na Rutshuru.
Soma pia:Kongo yaomba jumuiya kimataifa kuwawekea vikwazo wahusika wa uvamizi wa Rwanda nchini humo
Kundi hilo linalolinyooshea kidole cha lawama jeshi la Kongo kuwa kwenye mstari wa mbele katika mapigano hayo limekuwa likitaka kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya Kinshasa, ombi ambalo limetupiliwa mbali na utawala wa Rais Felix Tshisekedi.
Uporaji wa mifugo, mazao ya mashamba pamoja nakuawa kwa raia wakawaida ndio hali halisi ianayoshuhudiwa katika eneo zinazokumbwa na machafuko.