1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo na mahakama ya ICC zakubaliana kuimarisha ushirikiano

2 Juni 2023

DRC na mahakama ya ICC ICC zakubaliana kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana dhidi ya hatua ya kutochukuliwa sheria watu wanaohusishwa na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

DR Kongo Kinshasa | Besuch Chefankläger Internationaler Strafgerichtshof Karim Khan
Picha: Justin Makangara/AA/picture alliance

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita- ICC wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana dhidi ya hatua ya kutochukuliwa sheria watu wanaohusishwa na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Hatua hiyo imefikiwa jana kufuatia ziara ya siku nne ya Karim Khan mwendesha mashtaka mkuu wa ICC  nchini Kongo. Khan amesema pamoja na kuwepo ushirikiano mzuri kati ya taasisi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa bahati mbaya bado kuna visa vingi vya uhalifu na unyanyasaji dhidi ya wanaume na wanawake kubakwa.

"Lakini kwa bahati mbaya wasichana wengi, wavulana wengi na wanawake chungunzima  wanaendelea kunyanyaswa na kubakwa. Nimewaona waathirika wa visa hivyo. Nimewaona watoto waliobakwa na kujifungua watoto ambao nao pia walibakwa. Na mzunguko huo utaendelea ikiwa hatutojenga ushirikiano mpya,'' amesema Khan.

Mahakama ya ICC imekuwa ikifuatilia Kongo tangu mwaka 2002 na ilianzisha uchunguzi wake wa kwanza kaskazini Mashariki mwa jimbo la Ituri mwaka 2004. ICC na Kongo jana walisaini mkataba wa maelewano wa kushirikiana.