Kongo na Rwanda kuijumuisha Marekani kufufua sekta ya madini
14 Septemba 2025
Kwenye rasimu ya mktababa huo wa kiuchumi iliovujishwa, Kongo na Rwanda zimekubaliana juu ushirikiano wa kiuchumi, ambao ni sehemu ya makubaliano ya amani yaliotiwa siani na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili. Chanzo kimoja kutoka serikali ya nchi hizo kililiambia shirika la habari la Reuters kuwa rasimu hiyo kwa sasa inajadiliwa na wadau mbalimbali, wakiwemo wasekta binafsi, benki za kimataifa, na mashirika ya wafadhili kutoka nchi nyingine.
Maafisa wa Kongo na Rwanda wanatarajiwa kukutana mapema Oktoba ili kukamilisha rasimu hiyo, ambayo itasainiwa na wakuu wa nchi baadaye. Rasimu hiyo yenye kurasa 17 imeandaliwa baada ya nchi hizo kusaini makubaliano ya amani mjini Washington mwezi Juni, katika mazungumzo yaliyoandaliwa na serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump. Makubaliano hayo yanalenga kumaliza mapigano yaliyosababisha vifo vya maelfu na kuvutia uwekezaji wa mabilioni ya dola kutoka mataifa ya Magharibi katika eneo lenye utajiri wa madini kama tantalum, dhahabu, cobalt, shaba, na lithium.
Rasimu hiyo imefuatia mkataba wa awali uliokubaliwa mwezi Agosti, na inaeleza hatua za utekelezaji na mifumo ya uratibu. Makubaliano hayo yalisisitiza ushirikiano katika sekta za nishati, miundombinu, mnyororo wa usambazaji wa madini, hifadhi za kitaifa, na afya ya umma.
Hadi kufikia sasa Kongo, Rwanda, na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani hawakujibu maombi ya maoni yaliyowasilishwa na shirika la habari la Reuters.
Hatua za kufikia mageuzi ya kiuchumi
Kwa mujibu wa rasimu hiyo, pande husika zitajitolea kushirikiana na Marekani na washirika wengine wa kimataifa kuendeleza hatua za udhibiti na mageuzi ya ziada "ili kupunguza hatari kwa uwekezaji wa sekta binafsi kwa njia ya gharama nafuu,” kupunguza biashara haramu na kuongeza uwazi katika sekta ya madini.
Pia Rwanda na Kongo zitakubali kutumia mifumo ya uwazi kutoka nje, ikiwemo kutekeleza mwongozo kutoka Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), miongoni mwa mengine.
Rasimu hiyo inataka ukaguzi wa migodi kufanywa na washirika wengine, na kushirikiana na sekta binafsi kuendeleza maeneo maalum ya kiuchumi ya mipakani.
Mfumo huo pia unaweka utaratibu wa uratibu, ikiwemo ratiba ya mkutano wa kila mwaka wa ngazi ya juu kuhusu ujumuishaji wa kiuchumi wa kikanda, pamoja na mikutano ya kamati ya usimamizi na vikundi vya kiufundi.
Kinshasa na Kigali, kama sehemu ya makubaliano ya Juni ya mjini Washington, walikubaliana kuzindua mfumo wa ujumuishaji wa kiuchumi wa kikanda ndani ya siku 90. Katika makubaliano hayo, pande hizo ziliahidi kutekeleza mpango wa mwaka 2024 ambao unatarajiwa kuona wanajeshi wa Rwanda wakiondoka mashariki mwa Kongo ndani ya siku 90. Operesheni za kijeshi za Kongo dhidi ya kikundi cha FDLR, ambacho kinajumuisha masalia ya jeshi la zamani la Rwanda na wanamgambo waliohusika na mauaji ya kimbari ya 1994, zinatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi hicho hicho.
Changamoto za makubaliano hayo
Hata hivyo, kuna wasiwasi kuwa ratiba ya utekelezaji inaweza kukumbwa na vikwazo.
"Mojawapo ya vikwazo vikuu vya kukamilisha na kusaini makubaliano haya ya kikanda ni kwamba michakato mingine ya amani imesimama," alisema mwanadiplomasia wa Magharibi ambaye hakutaka kutajwa jina lake, akiongeza kuwa Rwanda haijatoa wanajeshi wake na operesheni dhidi ya FDLR bado hazijaanza.
Mwanadiplomasia huyo alisema juhudi tofauti za upatanishi kati ya serikali ya Kongo na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, kupitia mchakato wa Doha, zinakumbwa na ugumu. Waasi wa M23 waliteka miji mikubwa miwili mashariki mwa Kongo na maeneo yenye migodi yenye faida kwa kasi kubwa mapema mwaka huu.
"Bila maendeleo ya kiusalama, washirika na hata wahusika wenyewe watapata ugumu kujitolea kwa ushirikiano wa kiuchumi,” alisema mwanadiplomasia huyo kwa masharti ya kutotajwa jina.
Afisa mmoja wa Kongo aliliambia shirika la habari la Reuters mwezi huu kuwa Kinshasa "haiwezi kuzingatia ushirikiano wa kiuchumi na Rwanda ilhali jeshi lake linashikilia sehemu ya ardhi yetu.”
Serikali ya Kinshasa inaona uporaji wa utajiri wa madini yake kama kichocheo kikuu cha mzozo kati ya vikosi vyake na waasi wa M23 mashariki mwa Kongo. Katika makubaliano ya mwezi uliopita, Rwanda na Kongo walithibitisha kuwa kila nchi ina "mamlaka kamili ya kieneo” juu ya uchimbaji, usindikaji, na usafirishaji wa rasilimali zake asilia, na walitambua umuhimu wa kuendeleza uwezo wa usindikaji wa madini ndani ya kila nchi.
Chanzo : Reuters