1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yaanza kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi

23 Desemba 2023

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetoa matokeo machache ya mapema ya uchaguzi mkuu uliorefushwa na kusababisha baadhi ya wagombea wa upinzani kulalamikia udanganyifu na kudai urudiwe. Unaonyesha Tshisekedi anaongoza

Wahlen in der DR Kongo
Uchaguzi wa Kongo ulikumbwa na hitilafu za vifaa na changamoto za usafiri katika baadhi ya maeneo ya masharikiPicha: THOMAS MUKOYA/REUTERS

Matokeo ya awali kutoka kwa maelfu kadhaa ya wapiga kura wa jamii ya Wakongo walioko nje ya nchi yanaonyesha Rais Felix Tshisekedi anaongoza dhidi ya wapinzani wake. Matokeo hayo ni kutoka kwa raia wanaoishi Afrika Kusini, Ubelgiji, Ufaransa, Canada na Marekani.

Soma pia: CENI: Matokeo ya uchaguzi DRC kutangazwa kwa hatua

Tume huru ya uchaguzi CENI imesema matokeo ya kura zilizopigwa nchini Kongo na karibu wapiga kura milioni 44 waliosajiliwa yataanza kutolewa kuanzia leo Jumamosi.

Tshisekedi anatafuta muhula wa pili madarakaniPicha: AFP

Katika kikao cha waandishi habari katika mji mkuu Kinshasa, Rais wa CENI Denis Kadima kwa mara nyingine alipinga ukosoaji wa upinzani na waangalizi huru kuwa uchaguzi huo uliorefushwa ulikuwa na vurugu na ulikosa uhalali. Kikiuzungumzia uchaguzi huo kwa mara ya kwanza jana Ijumaa, kikundi cha uangalizi wa uchaguzi cha Marekani, Kituo cha Carter, kilisema kulikuwa na ukosefu wa Imani katika mchakato huo, hali iliyotokana kwa sehemu na chaguzi za awali, Pamoja na mianya katika uwazi, hasa kuhusiana na daftari la wapiga kura.

Upigaji kura kwa baadhi ulirefushwa hadi Ahamisi, na kusababisha wagombea watano wa upinzani kuitisha uchaguzi mpya, wakisema kuongezwa kwa muda huo ni kinyume cha katiba.

Upinzani na makundi huru ya uangalizi wa uchaguzi ya Kikongo wamesema upigaji kura ulifanyika katika njia ambayo huenda ikaathiri uaminifu wa matokeo.

Soma pia: Chama cha FCC chadai Tshisekedi ameuvuruga uchaguzi wa Kongo

Tume ya CENI imeweka kituo kikuu cha matokeo mjini Kinshasa kiitwacho Basolo – kumaanisha Ukweli katika lugha ya Kilingala – ambapo inasema matokeo kutoka kila kituo cha kupigia kura yatatangazwa hadharani pindi yanapoingia. Hili limekuwa sharti kuu la upinzani na mashirika ya kiraia, ambayo yanasema ukosefu wa uwazi katika chaguzi zilizopiga uliwezesha udanganyifu.

Uchaguzi DRC 2023: Matokeo ya awali yasubiriwa

02:39

This browser does not support the video element.

CENI imeweka Desemba 31 kuwa tarehe ya mwisho ya kutoa matokeo kamili ya muda, lakini haijulikani kama hili litabadilika kutokana na kurefushwa ambako hakukutarajiwa kwa zoezi la upigaji kura.

Kituo cha Carter kimetoa wito kwa tume kuchapisha matokeo katika ngazi ya mitaa na kuyaweka matokeo ya vituo vya kupigia kura kwenye tovuti yake ili kuhakikisha kuwa mchakato huo unaaminika.

Mgombea wa upinzani Moise Katumbi, ambaye timu yake imekuwa ikifuatilia zoezi la kuhesabu kura, alisema Alhamisi kuwa matokeo hayo mpaka sasa yanamuonyesha akiwa kifua mbele.

Ujumbe wa uangalizi kutoka Kanisa Katoliki la Kongo lenye nguvu kubwa umewapeleka Zaidi ya waangalizi 25,000 kufanya ujumlishaji wake wa matokeo ya uchaguzi. Walifanya hivyo pia wakati wa uchaguzi wa 2018, walipopinga matokeo yaliyotolewa na CENI.

Uchaguzi huu utaamua kama Tshisekedi atahudumu kwa muhula wa pili baada ya miaka mitano ya kwanza madarakani kuambatana na matatizo ya kiuchumi na kukithiri kwa ukosefu wa usalama katika eneo la mashariki mwa Kongo linalokumbwa na uasi

Reuters, afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW