1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yaanzisha mazungumzo na Zambia kufungua mpaka

12 Agosti 2024

Kongo imeanza mazungumzo na Zambia siku chache baada ya taifa hilo jirani upande wa kusini kutangaza kuufunga mpaka wake na Kongo ambao ni lango muhimu la usafirishaji bidhaa baina ya nchi hizo mbili.

Mji wa Kasumbalesa katika mpaka wa Zambia na Kongo
Zambia ilikifunga kituo cha mpakani na Kongo baada ya kuzuka maandamano mpakani hapoPicha: Jonas Gerding/DW

Mnamo siku ya Jumamosi, Waziri wa Biashara wa Zambia Chipoka Mulenga alitangaza kuufunga kwa muda mpaka huo baada ya kuzuka maandamano kwenye mji wa mpakani wa Kasumbalesa. Maandamano hayo yalifanywa na wasafirishaji bidhaa waliokuwa wakipinga uamuzi wa Kongo wa kuzuia kuingizwa vinywaji na vileo kutoka Zambia .

Taarifa iliyotolewa na wizara ya biashara ya Kongo, imesema mazungumzo kati ya serikali ya nchi hiyo na Zambia yanafanyika ili kuwezesha kufunguliwa kwa eneo hilo la mpaka haraka iwezekanavyo.

Soma pia: Zambia yaagizia maelfu ya tani za mahindi kutoka Tanzania

Wawakilishi wanapanga kukutana mjini Lubumbashi kutafuta suluhisho la kudumu juu ya mahusiano ya kibiashara kati nchi ya nchi hizo jirani.

Kongo iliyo mzalishaji mkubwa wa pili duniani wa madini ya shaba inatumia njia za mataifa jirani ikiwemo Zambia kusafirisha malighafi hiyo kimataifa.