1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yafutilia mbali mradi wa vitambulisho vya elektroniki

6 Septemba 2024

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imefutilia mbali mradi wa dola bilioni 1.2 wa kuanzisha mfumo wa kitaifa wa vitambulisho vya kielektroniki.

Bendera ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mbele ya bunge la nchi hiyo
Bendera ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya KongoPicha: Dreamstime/Igorhirsc/Panthermedia/IMAGO

Richard Ilunga, mkurugenzi mkuu wa Ofisi ya Kitaifa ya Utambulisho wa Idadi ya Watu nchini Kongo, ONIP, amesema kuwa mradi huo ulifutiliwa mbali kufuatia mkutano wa Agosti 12, uliohusisha mashirika mbalimbali ya serikali na wawakilishi kutoka kampuni zinazoshirikiana za Idemia-Afritech, lakini aliposhinikizwa, alikataa kutoa sababu za kufutiliwa mbali kwa mkataba huo.

Matokeo ya uchunguzi wa ubadhirifu yachapishwa

Hatua hiyo inakuja siku tatu baada ya shirika la habari la Bloomberg na lile lisilojipatia faida la Lighthouse Reports kuchapisha uchunguzi ulioangazia madai ya ubadhirifu wa fedha unaozunguka msururu wa miradi ya vitambulisho iliyofeli nchini Kongo.

Benki ya Dunia ilikataa kuchangia ufadhili wa mradi huo kwa sababu ya ukosefu wa mchakato wenye ushindani wa zabuni. Mnamo 2023, watumishi wa umma katika shirikika la ONIP,  walitoa waraka wa siri ambao ulisambazwa ndani na ambao ulionekana na Bloomberg News na Lighthouse.

Kandarasi ingeweza kugeuka kuwa ulaghai mkubwa

Waraka huo uliangazia vipengele vya kuzua hofu katika pendekezo kutoka kwa Idemia na Afritech, ikiwa ni pamoja na ongezeka kubwa la bei la wazi na hatari kwamba kandarasi hiyo ingeweza kugeuka kuwa ulaghai mkubwa.

Jean-Claude Mputu, msemaji wa shirika la kupambana na rushwa la ''Congo is Not to Sell Picha: privat

Jean-Claude Mputu, msemaji wa shirika la kupambana na rushwa la ''Congo is Not to Sell '' - yaani Kongo sio ya kuuzwa, amesema mkataba ulihitimishwa chini ya mazingira yakutatanisha:

Mnamo mwezi Juni mwaka huu, Mkaguzi Mkuu wa Fedha, shirika la uangalizi wa serikali yaKongo, lilitoa matokeo ya uchunguzi wa ndani ambao ulizua wasiwasi kuhusu gharama ya mradi huo na kubaini kuwa mbinu iliyopendekezwa ya kufadhili mfumo huo ilikuwa kinyume cha sheria au kutowezekana.

Rais Felix Tshisekedi aagiza maelezo ya kina kuhusu kandarasi

Muda mfupi baada ya ripoti hiyo kuchapishwa, Rais Felix Tshisekedi alitoa taarifa akisema anataka maelezo ya kina kuhusu kandarasi hiyo kutoka kwa waziri wa mambo ya ndani.

Kwa dola bilioni 1.2, gharama iliyotarajiwa ya mfumo wa vitambulisho vya Kongo na miundombinu inayosaidia ilikuwa zaidi ya mara tatu ya makadirio ya awali ya ONIP.

Kongo haina mfumo wa vitambulisho vya kitaifa, jambo linalofanya iwe vigumu kwa raia kufungua akaunti za benki, kupata hati rasmi au kujiandikisha kupiga kura.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW