1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yaingia siku ya pili ya uchaguzi wenye vurugu

Saleh Mwanamilongo
21 Desemba 2023

Wapiga kura katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanamiminika tena vituoni leo Alhamisi, katika uchaguzi mkuu ambao umekubwa na matatizo ya vifaa na usafiri ambayo yalisababisha baadhi ya vituo kutofunguliwa

Demokratische Republik Kongo Wahllokal in Kinshasa
Karibu watu milioni 44, walitarajiwa kupiga kura, lakini wengi hawakufanya hivyoPicha: Alain Uyakani/Xinhua/IMAGO

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi CENI, Denis Kadima amesema zoezi la upigaji kura limeongezwa hadi Alhamisi katika baadhi ya vituo vya kupigia kura kwasababu ya kuchelewa kuanza kwa zoezi hilo. "Tumefadhahishwa kuona kwamba kulikuwa na visa vya uharibifu katika baadhi ya maeneo kote nchini, lakini wananchi walionyesha kuvutiwa na uchaguzi na kwangu imenipa matumaini.‘‘

Soma pia: Zoezi la uchaguzi lanedelea DR Kongo

Vituo vyote vya kupigia kura vilikusudiwa kufungwa saa kumi na moja lakini kwa sababu vingi vilichelewa,tume ya uchaguzi imerekebisha ratiba. Wasimamizi wa vituo hivyo wameambiwa kuhakikisha vinasalia wazi kwa saa 11 baada ya upigaji kura kuanza. Hata hivyo, baadhi vinaweza kukaa wazi kwa muda mrefu zaidi kwani lazima mtu wa mwisho kwenye foleni aruhusiwe kupiga kura, bila kujali wakati.

Baadhi ya vituo vya kupigia kura havikufunguliwaPicha: Zohra Bensemra/REUTERS

Upinzani wasema uchaguzi huo ni kichekesho

Mwenye kiti wa Tume ya uchaguzi amesema hatua hiyo haitaathiri matukio ya uchaguzi. Upinzani tayari umelalamikia uchaguzi huona kuuita wenye vurugu na uliojaa kasoro. Kwenye taarifa ya pamoja ya wagombea watano wa kiti cha urais wameuita uchaguzi huo kama kichekesho. Wagombea hao wakiwemo Martin Fayulu, Denis Mukwege na Floribert Anzuluni wametaka uchaguzi urudiwe na kuweko na tume mpya ya uchaguzi. Theodore Ngoy msemaji wa wagombea hao amesema kilichofanyika jana Jumatano nchini Kongo sio uchaguzi. Rais Felix Tshisekedianatafuta muhula wake wa pili na wa mwisho wa miaka mitano, na anashindana na wagombea wengine 26 kwenye uchaguzi huo. 

‘‘Zoezi la uchaguzi lilikuwa ni jaribio la uchaguzi ambao matokeo yake yatawahusisha baadhi ya watu waliopiga kura katika baadhi ya vituo vya uchaguzi. Kwa hiyo tunawataka raia wa Kongo, Tume ya uchaguzi, serikali inayoondoka  na jamii ya kimataifa kufahamu kwamba ifikapo asubuhi ya Alhamisi ya tarehe 21, desemba  kwamba uchaguzi uliotarajiwa Desemba 20 haukufanyika kulingana na katiba ya  sheria ya uchaguzi."

Soma pia: Wasifu wa Moise Katumbi

Tshisekedi anatafuta muhula wa pili na wa mwishoPicha: AFP

Raia wa Kongo walijitokeza kwa wingi mapema hapo jana  kushiriki zoezi la upigaji kura. Lakini kulikuwa na visa kadhaa vya ucheleweshaji wa zoezi hilo. Sababu kubwa ni ukosefu wa vifaa vya kupigia kura katika majimbo yote 26 ya Kongo. Waangalizi wa uchaguzi kutoka makanisa ya Kikatoliki na Kiprotestanti nchini walisema theluthi moja ya vituo vya kupigia kura kote nchini havikufunguliwa. Na asilimia 45 ya vituo vilivyofungua milango yake vilikabiliwa na mataizo ya mashine ya kupigia kura.

Majina yakosekana kwenye daftari

Matazizo mengi yalitokea pia pale wapiga kura walipokosa kuona majina yao kwenye daftari la kupigia kura.

Hapa mjini Kinshasa vituo vya kupigia kura vilibaki wazi hadi saa tano usiku. Kidole cha lawama kinaelekezwa kwa tume ya uchaguzi ambayo licha ya dola bilioni moja na laki mbili milioni ilishindwa kuaanda uchaguzi unaoaminika.

Kongo ni takriban mara nne ya ukubwa wa Ufaransa, lakini haina miundombinu ya kimsingi - hata baadhi ya miji yake kuu haijaunganishwa na barabara. Umoja wa Mataifa, Misri na nchi jirani ya Kongo-Brazzaville zilisaidia kusafirisha nyenzo za uchaguzi katika maeneo ya mbali. Lakini hata hivyo bado kunamaeneo ambayo vifaa vya uchaguzi bado kuwasili.

Takriban watu milioni 44 walijiandikisha kupiga kura, kufuatia kampeni iliyotawaliwa na hali mbaya ya ukosefu wa usalama katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.