1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yaishutumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23

Jean-Noel Ba Mweze26 Mei 2022

Wakati jeshi la serikali ya Kongo (FARDC) likiendeleza mapambano dhidi waasi wa M23, serikali mjini Kinshasa imesema kuwa inafuatilia ili kuthibitisha tuhuma kwamba Rwanda ndiyo inawaunga mkono waasi hao.

Mai-Mai Milizen im Kongo
Picha: Dai Kurokawa/dpa/picture alliance

Tangazo la serikali ya Kongo limetolewa jana Jumatano jioni, baada ya kikao cha baraza la usalama kilichofanyika hapa mjini Kinshasa kuhusu hali ya usalama mkoani Kivu Kaskazini.

Mkutano huo ambao umefanyika wakati mapambano baina ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 yakiendelea kwa umbali wa kilomita chache kutoka Goma, mji mkuu wa mkoa huo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Soma pia →Tshisekedi akamilisha ziara yake Burundi

''Hatufikirii kuwa M23 wana nguvu hizo kijeshi''

Wapiganaji wa M23 wameshambulia ngome ya jeshi ya RumangaboPicha: Dai Kurokawa/dpa/picture alliance

Lakini idadi ya wapiganaji na vifaa vya kivita upande wa waasi ni miongoni mwa dalili nyingi zinazosababisha shutuma dhidi ya Rwanda. Hata hivyo DRC imeapa kutoruhusu kupoteza hata sentimeta moja ya eneo lake, kama alivyoeleza Patrick Muyaya, Waziri wa mawasiliano ambae pia ni msemaji wa serikali ya Kongo.

''Kwa yale ambayo wanajeshi wameyaona kwenye mapambano, hatufikirii kuwa M23 wana nguvu hizo kijeshi. Hiyo inathibitisha  tuhuma zetu. Vikosi vyetu  vimehimizwa tena ili kuhakikisha eneo letu inalindwa vyema. Lazima  tusimame wote ili kusiwe na  kikundi au nchi yoyote itakayojaribu kuchukua sentimita hata moja ya eneo letu.'',alisema Muyaya.

Soma pia →Nia ya Uganda kuondoa wanajeshi DRC yazusha maoni mseto

Upinzani wa kisiasa waomba hatua zaidi 

Zaidi ya raia 8,000 wamevuka mpaka wa Uganda Picha: Emmanuel Lubega/DW

Upinzani pia umelaumu shambulio hilo ukisema kwamba M23 ni kama tu mkono unaotumiwa na Rwanda ili kuichokoza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Na kuhusu hayo, chama cha upinzani cha ECIDE, kinachoongozwa na Martin Fayulu, kinapanga kuwahamasisha Wakongomani ili kuunga mkono jeshi la taifa dhidi ya shambulio hilo kutoka nchi jirani, kama alivyojulisha Jean-Baptiste Kasekwa, mubunge wa chama ECIDE.

'' Tumetangaza kuliunga mkono kikamilifu jeshi la FARDC na tumejitolea kukemea unyanyasaji unaofanywa na Rwanda dhidi ya nchi yetu, pia kukemea ushirikiano wote popote unapotoka na hasa ukimya wa serikali ya Kinshasa, wakati ushuhuda wa wakazi mashariki ukithibitisha uwepo wa wageni.'', alisema Kasekwa.

Hii sio mara ya kwanza kwa Rwanda kulaumiwa kuunga mkono uasi hapa nchini Kongo. Miezi michache iliyopita, Rais wa Rwanda Paul Kagame alitishia kupeleka vikosi vyake  mashariki mwa Kongo ili kuwafuata maadui zake.