Kongo yaituhumu Rwanda kuwaua raia 1,500
1 Januari 2026
Taarifa iliyotolewa na serikali ya Kongo siku ya Jumatano imesema vifo hivyo vimetokea wakati kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda lilipoanzisha mashambulizi mapya upande wa mashariki.
Kundi hilo lilifanya mashambulizi makali yaliyoliwezesha kuukamata mji muhimu wa Uvira. Mji huo upo karibu kabisa na mpaka wa taifa jirani la Burundi.
Hujuma hizo zilitokea siku chache baada ya serikali za Kongo na Rwanda kutia saini mkataba wa kusitisha vita chini ya upatanishi wa Marekani mnamo Disemba 4.
"Idadi ya awali ya raia waliopoteza maisha kutokana na operesheni za Rwanda, ambazo zimejumuisha matumizi ya mabomu na droni tangu mwanzoni mwa Disemba, imefikia zaidi ya 1,500," imesema taarifa ya serikali ya Kongo.
Kongo yadai Rwanda imeongeza wanajeshi upande wa mashariki
Kongo pia imeituhumu serikali mjini Kigali kwa kupeleka "bataliani nyingine tatu" za wanajeshi wake kwenye mkoa wa Kivu Kusini, kwa lengo la kusonga mbele hadi kwenye "eneo la kimkakati la Kalemie".
Eneo hilo linapatikana kwenye jimbo la kusini mashariki mwa Kongo lenye utajiri mkubwa wa madini la Tanganyika.
Tangu M23 ilipoanza tena mashambulizi yake dhidi ya vikosi vya serikali ya Kongo mwaka 2021, kundi hilo limefanikiwa kuchukua udhibiti wa eneo kubwa la ardhi upande wa mashariki unajulikana kwa utajiri mkubwa wa maliasili.
Ushahidi unaonesha Rwanda imekuwa ikiliunga mkono kundi hilo kijeshi na kifedha.
Mamia kwa maelfu ya watu wazikimbia nchi zao kunusuru maisha na kwa jumla masharika ya kimataifa yanasema hali ya kibinadamu imedhoofika mno mashariki mwa Kongo.
Mashaka yagubika ahadi ya M23 kuondoka Uvira
Washington imeituhumu Rwanda kwa kukiuka mkataba wa amani uliosifiwa na Rais Donald Trump wa Marekani kuwa mkataba wa "kimiujiza" licha ya mashambulizi ya M23.
Marekani ilitoa shinikizo kubwa kwa M23 ambayo siku chache baada ya kuukamata mji wa Uvira ilitangaza kuwa itawaondoa wapiganaji wake.
Hata hivyo, wakaazi wa mji huo na vikosi vya usalama vya Kongo vimeripoti kwamba wapiganaji wa M23 wanaovalia mavazi ya kiraia wamebakia kwenye mji huo huku Marekani na serikali ya Kongo zimetilia mashaka ahadi ya kundi hilo kuwa limeondoka Uvira.
Kukamatwa mji wa Uvira kulitokea karibu mwaka mmoja tangu M23 ilipochukua udhibiti wa miji ya Goma na Bukavu ambayo ni miji mikuu ya mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Mike Waltz amekosoa kile amekitaja kuwa "ukubwa na mbinu za kificho" zinazotumiwa na Rwanda kujihusisha na ukosefu wa utulivu mashariki mwa Kongo, akiituhumu nchi hiyo kuwa na wanajeshi wapatao 7,000 kwenye eneo hilo.
Idadi ya waliokimbia mapigano yakaribia milioni 1
Kulingana na Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 800,000 wameikimbia Kongo na kuingia nchi jirani ya Burundi kufuatia kuzidi mashambulizi ya M23.
Ukosefu huo wa usalama umesababisha watu wengine nusu milioni kuwa wakimbizi wa ndani nchini Kongo na karibu wote ni kutoka jimbo la Kivu Kusini.
serikali mjini KIgali imesisitiza mara zote kwamba inaandamwa na kitisho kikubwa kwa uwepo wa makundi yenye silaha mashariki mwa Kongo yaliyohusika na mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994.
M23 yenyewe pia inakanusha madai yote ya kuwa na mafungamano na Rwanda na kundi hilo limesisitiza kwamba lengo lake ni kuiangusha serikali ya Felix Tshisekedi wa Kongo.