1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yajiandaa kwa ziara ya papa

25 Januari 2023

Katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Kinshasa, waumini wanaminika kwenye vibanda vilivyojengwa kwenye viwanja vya makanisa kununua fulana na tishu zilizopambwa na sura ya papa Francis, kabla ya ziara yake.

Papst Franziskus I Weihnachtsbotschaft „Urbi et Orbi"
Picha: Yara Nardi/REUTERS

Kumbukumbu za Papa zimekuwa bidhaa zinazouzwa sana katika mji huo kabla ya safari ya siku nne ya Papa mzaliwa wa Argentina katika nchi hiyo yenye imani kubwa ya kidini ya Afrika ya kati, itakayoanza Januari 31.

Watu wengi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaiona ziara ya papa kama fursa ya kutuliza hali ya wasiwasi mashariki mwa nchi, ambako waasi wa M23 wameteka maeneo mengi tangu mwaka jana na kuzusha mgogoro wa kibinadamu.

Berthe Baleweya, mwanamke ambaye alifika katika kanisa kuu la Notre-Dame du Congo la Kinshasa kununua kitambaa cha nta chenye mada ya Francis, aliiambia AFP kwamba kuvaa sanamu ya papa itakuwa "baraka kubwa".

Soma pia: Papa Francis alaani Iran kuwanyonga waandamanaji

Emmanuelle Wemu, ambaye anaendesha kikundi cha misaada cha Kikatoliki, tayari amenunua na kurekebisha chapa yake ya nta iliyopambwa kwa uso wa papa. "Natarajia ujumbe wa amani kutoka kwake, katika wakati huu ambapo DRC iko katika machafuko," alisema.

Zaidi ya waumini milioni moja wanatarajiwa kuhudhuria misa ya wazi katika uwanja wa ndege wa Ndolo mjini Kinshasa mnamo Februari 1, sehemu kubwa katika jiji kuu la zaidi ya watu milioni 15.

Mji wa Kinshasa umo katika harakati za kumkaribisha Papa Francis kuanzia Januari 31, 2023.Picha: Junior Kannah/AFP/Getty Images

Kongo ni taifa la kikatoliki lenye watu zaidi ya milioni 90, maskini sana licha ya utajiri mkubwa wa madini.

Ziara ya Mashariki mwa Congo yaahirishwa

Papa Francis alipangiwa kuwasili DRC Julai mwaka jana, lakini safari hiyo iliahirishwa kwa sababu za kiafya. Wengi pia walivumisha kuwa kuongezeka kwa mzozo mashariki mwa Kongo -- ambako papa alikuwa akitarajiwa kuzuru -- kulisababisha kufikiria upya.  

Kundi la waasi la M23, ambalo linadaiwa kuungwa mkono na Rwanda, limefanya mashambulizi dhidi ya jeshi la Kongo na hivi karibuni limefika umbali wa maili kadhaa kutoka Goma, kitovu cha kibiashara cha zaidi ya watu milioni moja na mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Papa Francis hapangiwi tena kwendamashariki mwa Kongo, kulingana na ratiba yake mpya, lakini atakutana na wahanga wa mzozo huo akiwa Kinshasa.

Wengine wamekata tamaa. Gelo Mandela, mratibu wa vijana katika dayosisi ya Goma, alisema vijana wanakata tamaa kwamba jiji hilo halipo tena katika ratiba. "Tulikuwa tayari," alisema. Mfanyakazi wa misaada Emmanuelle Wemu alisema anatumai ziara ya papa italeta maridhiano na Rwanda.

Soma pia: Papa Francis: Wakumbukeni wanyonge na maskini

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya DRC na jirani yake mdogo umeingia kwenye mwamba tangu kuzuka kwa mgogoro wa M23 mwishoni mwa 2021. Rwanda inakanusha kuwaunga mkono waasi. Usalama wa Papa Francis huko Kinshasa pia unasalia kuwa wa wasiwasi, hasa kwa sababu ya tishio la wanamgambo kutoka mashariki.

Rais wa Kongo katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kinshasa.Picha: Nicolas Maeterlinck/Belga Photo/AFP/Getty Images

Kundi la Allied Democratic Forces, ambalo kundi la Dola la Kiislamu IS, linadai ni tawi lake, lilishambulia kanisa la Pentekoste mashariki mwa Kongo Januari 15, na kuua watu 14. ADF hadi sasa inaendesha operesheni mashariki mwa DRC tu, zaidi ya kilomita 1,500 (maili 930) kutoka mji mkuu.

 Maombi ya kumpokea Papa 
Kipindi cha siku tatu cha maombi -- kinachojulikana kama triduum -- kinapangwa katika kanisa kuu la Notre-Dame du Kongo kabla ya kuwasili kwa Francis.

Mkesha pia utafanyika katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Ndolo usiku wa Januari 31, kabla ya misa ya upapa asubuhi inayofuata, kulingana na Padre Camille Esika, kasisi wa kanisa kuu.

Soma pia: Umoja wa Mataifa wabaini shughuli za M23 mashariki mwa DRC

Kati ya watu milioni moja na  milioni 1.5 wanatarajiwa kusherehekea misa katika eneo la hekta nane (ekari 20). Kazi za maandalizi zinaendelea. "Siku hiyo, kuwepo na mvua au hakuna, kutakuwa na tukio," alisema Jesus-Noel Sheke, mratibu wa kiufundi wa mradi huo.

Kote mjini Kinshasa, mabango na ishara za kumkaribisha papa tayari zinaning'inia kwenye majengo. Ziara yake inaashiria safari ya kwanza ya Papa nchini humo tangu Papa John Paul II mwaka 1985.

Papa Francis aongoza mazishi ya Papa Benedict

02:16

This browser does not support the video element.

Justin-Marie Bayala, mwalimu aliyehudhuria misa ya hivi karibuni katika Kanisa Kuu la Notre-Dame du Congo, kama ilivyo kwa wengi, alielezea matumaini makubwa. "Tunathubutu kuamini kwamba atatuletea amani ya kudumu,” Bayala alisema.

Chanzo: AFPE