1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yahofia janga la binaadamu kufuatia uvamizi wa Rwanda

Jean Noël Ba-Mweze
15 Septemba 2023

Serikali mjini Kinshasa imeonya tena jana juu ya janga la kibinaadamu linalosababishwa na inachokiita uvamizi wa Rwanda nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Waziri wa muwasiliano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Patrick Muyaya Katembwe ameonya juu ya janga la kibinaadamu kutokana na uvamizi wa Rwanda nchini humo
Waziri wa muwasiliano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Patrick Muyaya Katembwe ameonya juu ya janga la kibinaadamu kutokana na uvamizi wa Rwanda nchini humoPicha: Dirke Köpp/DW

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inatoa matamshi hayo kuelekea mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wiki ijayo mjini New York, huku pia ikiitolea wito jumuiya ya kimataifa kuwawekea vikwazo zaidi wahusika. 

Waziri wa mawasiliano Patrick Muyaya na wa sheria Rose Mutombo walitoa hoja yao dhidi ya Rwanda katika mkutano wa habari mjini Kinshasa hapo jana, wakirejea madai kwamba Rwanda imekuwa ikiunga mkono waasi wa kundi la M23 wanaoongozwa na Watutsi, ambayo Kigali imekanusha mara kwa mara. 

Waasi hao wameteka maeneo makubwa ya mkoa wa Kivu Kaskazini, kwenye mpaka wa mataifa hayo mawili, tangu kuanzisha vita tena mwishoni mwa mwaka 2021, baada ya miaka kadhaa ya kukaa kimya.

Soma Pia: Jeshi DRC laishutumu Rwanda kupanga mashambulizi Kivu Kaskazini

Waziri Muyaya alizungumzia kile alichokiita uthibitisho usiyo na shaka wa shuguli za uhalifu zinazoendeshwa na jeshi la Rwanda pamoja na wafuasi wao wa M23. Akiwasilisha taarifa za waraka wa awali kuhusu sula hilo, alisema mzozo huo umewalaazimisha zaidi ya watu milini 2.3 kuyakimbia makazi yao na kuacha mamia ya shule zikiwa zimeharibiwa au kukaliwa kimabavu.

Waasi wa M23 katika picha iliyopigwa Januari 6, 2023 wakiwa wanaondoka kwenye kambi ya Rumagabo. Waasi hawa wanashutumuiwa kwa visa vya umwagaji damu wakisaidiwa na Rwanda.Picha: Guerchom Ndebo/AFP

Wakati akikaribisha uungwaji mkono wa kidiplomasia wa hivi karibuni, Muyaya ametoa wito wa hatua za nguvu zaidi za kimataifa kwa mzozo huo, akisema  "Tunahitaji sauti ya pamoja kupinga mashambulizi na ghasia zinazoendelea na ni lazima hatua kali zaidi zichukuliwe na nchi washirika."

Mzozo kwenye eneo hilo unazidisha ugumu wa kuwaandikisha wapiga kura.

Mzozo huo pia umefanya iwe vigumu kuongeza watu katika maeneo yalioathirika kwenye orodha ya wapigakura, jambo litakaloathiri uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Desemba.

Soma Pia: Mukwege akosoa matayarisho uchaguzi DRC

Kwa upande wake, waziri wa sheria Rose Mutombo, alisema tayari amewasilisha mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, na Mahakama ya Afrika ya Haki za Kibinadamu. Lakini hali inaonekana bado inaendelea kuzorota katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa M23 mkoani Kivu Kaskazini.

Jean-Claude Bambaze, kiongozi wa shirika la kiraia katika katika eneo la Rutshuru alisema "Wakazi wanaishi kwa hofu hofu na woga sana. Mapambano ni makali sana na utekaji nyara unaendelea na mauaji pia ni mengi sana. Padri mkuu wa parokia ya Karambi alinusurika kutekwa nyara na gari lake lilipigwa risasi. Hali inazidi kuwa mbaya badala ya kuimarika."

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa pia wameituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 na mnamo mwezi Julai, Umoja wa Ulaya ililaani hatua ya Rwanda kuwepo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW