1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yatangaza serikali mpya baada ya kucheleweshwa

29 Mei 2024

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeiteuwa serikali mpya, na hivyo kuhitimisha mkwamo ambao umeikumba nchi hiyo katika sintofahamu ya kisiasa kwa miezi kadhaa.

Waziri mkuu mpya wa Kongo Judith Suminwa Tuluka akiwa na Rais Tshisekedi
Rais Tshisekedi alimteuwa Judith Suminwa Tuluka kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke nchini KongoPicha: Xinhua News Agency/picture alliance

Katika tangazo lililotolewa mapema leo na msemaji wa serikali Tina Salama na kurushwa na televisheni ya taifa RTNC, baraza hilo jipya lina mawaziri 54 ikilinganishwa na 57 katika serikali iliyopita. Mwanasheria Guy Kabombo Muadiamvita ameteuliwa kuwa waziri wa ulinzi - wadhifa muhimu ikizingatiwa mgogoro mbaya kabisa wa miaka miwili kati ya Kongo na waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo. Doudou Fwamba Likunde ameteuliwa waziri wa fedha na Kizito Pakabomba atasimamia wizara muhimu ya madini. Akirejelea kucheleweshwa kuundwa serikali, mkurugenzi wa mawasiliano wa rais Erik Nyindu alisema ilichukua muda kwa pande tofauti katika muungano tawala kufikia maelewano.

Rais Felix Tshisekedi alishinda muhula wa pili baada ya uchaguzi wa mwishoni mwa mwaka wa 2023 ambao uliupa muungano wa Union Sacre wingi mkubwa wa viti bungeni. Lakini malumbano ya ndani ya kugombania nyadhifa yakachelewesha kuundwa kwa baraza jipya la mawaziri. Rais hatimaye alimtangaza Judith Suminwa kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke nchini Kongo na aliyekuwa mkuu wake wa utumishi Vital Kamerhe kuwa spika wa bunge na hivyo kusafisha njia ya kuteuliwa serikali.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW