1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Kongo yatangaza waasi wa Mobondo kuwa kundi la kigaidi

Byobe Malenga30 Desemba 2025

Serikali ya Kongo yatangaza waasi wa Mobondo kusini magharibi mwa nchi kuwa kundi la kigaidi, huku machafuko ya kikabila yakiongezeka na usalama wa taifa ukitetereka.

Kundi hili limehusishwa na mfululizo wa mashambulizi dhidi ya raia na majeshi ya serikali
Mobondo ni kundi la wanamgambo linaloendesha machafuko katika magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) tangu mwaka 2022Picha: ALEXIS HUGUET/AFP

Kundi la waasi la Mobondo limeibuka upya, na kusababisha hofu ya kutokea kwa machafuko makubwa katika mji mkuu Kinshasa. Video zilizosambaa mitandaoni zinawaonyesha wanamgambo hao wakiwa wamefunga vitambaa au fulana nyekundu vichwani, wakidai kupigania mageuzi nchini.

Wiki iliyopita pekee, zaidi ya watu sabini waliuawa katika mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na waasi hao, hali inayozidi kuhatarisha usalama wa raia. Kufuatia hali hiyo,jeshi la DRC limelitangaza rasmi kundi la Mobondo kuwa la kigaidi, kama anavyofafanua hapa Kapteni Anthony Mwalushayi, msemaji wa jeshi katika mkoa wa Bandundu.

 "Jambo la kwanza nataka kusema ni kwamba hii ni harakati ya kigaidi. Kwa nini nasema ni harakati za kigaidi? Kwani mimi na wewe tumeona unyama unaofanywa na vikundi hivi vya waasi katika kijiji cha Nkana, kijiji cha Nkuma Nkero, na katika baadhi ya vijiji vilivyoko kando ya mto Koumou, ambako wanawake hawakubakwa tu bali pia kukatwa vichwa, ambapo miili ya binadamu iliuawa tu.
Uliona picha za wanawake hawa ambao walikuwa wakiishi maisha ya kawaida hadi Mopondo alipofika na kuteketeza kijiji. Lakini kabla ya kuzichoma moto nyumba hizo, walichukua hatua ya kuwakusanya wanawake wote waliokuwapo, wakawafungia ndani ya nyumba, na kuichoma moto. Hili halikubaliki katika nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, nchi ya kidemokrasia",
alisema Mwalushayi, Msemaji wa Jeshi la Kongo.

 "Kundi la Mobondo sasa linalenga kuyumbisha taasisi za Jamhuri"

Mamia ya watu wameripotiwa kuuawa, na familia nyingi zimelazimika kuyahama makazi yao kufuatia machafuko ya wanamgambo hao wakikabilaPicha: Alexis Huguet/AFP

Kwa mujibu wa jeshi, wapiganaji wa Mobondo wanatumia mbinu zinazofanana na zile za waasi wa ADF, ikiwemo kuwaua raia kwa kuwakatakata viungo, kuwadunga mikuki na kutumia visu. Kapteni Mwalushayi ameonyesha masikitiko makubwa, akidai kuwa baadhi ya waasi hao wanadaiwa kupata msaada kutoka kwa maafisa fulani wa serikali walio karibu na uongozi wa juu wa nchi.

"Jeshi lako, kupitia huduma zake za kijasusi, linafanya kazi ya kuanzisha uhusiano kati ya vuguvugu hizi za waasi, Mobondo, na waasi wengine kote nchini. Tuna taarifa zinazoonyesha mawasiliano fulani kati ya vuguvugu la waasi katika eneo la mashariki mwa DRC na vuguvugu hili la Mobondo, ambalo sasa linalenga kuyumbisha taasisi za Jamhuri. Hatari iliyopo ni kwamba watu walio wengi nyuma ya Mobondo, narudia, mara nyingi pia wako nyuma ya Rais wa Jamhuri. Wakati wa mchana, wanafanya kama wana-kondoo, na usiku, wao ndio wanaoendesha Mobondo, kwa sababu wana uwezo wa kufanya hovyo", aliongeza Mwalushayi.

Wachambuzi wa siasa wanasema serikali ya DRC ilichelewa kuchukua hatua za haraka kudhibiti mgogoro huo. Wanaonya kuwa endapo hali hii haitashughulikiwa ipasavyo, usalama utaendelea kuzorota. Asani Kizunguluka, mchambuzi wa siasa nchini Kongo, ameiambia DW kwamba tatizo la wanamgambo wa Mobondo huenda likasabisha utata mkubwa.

"Tunaona sasa hivi makumi ya watu wamekufa, hali sio nzuri. Itikadi za hawa wanamgambo wa Mobondo hazikuanzia hapa Kinshasa, lakini serikali haijachukulia kwa uzito tatizo hilo. Hili ni tatizo kubwa ambalo linaweza kuzusha utata mnamo siku za usoni", alisema Kizunguluka. 

Kongo: Wanawake Goma wajitosa kwenye bodaboda

03:07

This browser does not support the video element.

Katika maeneo ya Kwamouth mkoani Bandundu Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hali ya usalama bado ni tete.

Mapigano ya kikabila kati ya jamii za Wateke na Wayaka yamesababisha vifo vya maelfu ya watu, huku familia nyingi zikikimbia makazi yao, hasa katika mji wa Bangata, ulioko takriban kilomita 150 kutoka mji mkuu Kinshasa.